Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-19 16:26:54    
Usingizi wa kisayansi wajenga afya

cri

Kwa kawaida, usingizi unachukua theluthi moja ya muda wa maisha yote kwa binadamu, na unahusiana kwa karibu na afya ya watu. Usingizi bora na wa kutosha ni msingi muhimu wa afya. Lakini watu wengi hawafahamu sayansi ya usingizi. Kwa mfano, binadamu anahitaji usingizi kwa saa ngapi? Ni kwa vipi anaweza kuuboresha usingizi? Inafaa kulala kidogo adhuhuri? Katika kipindi hiki cha elimu na afya, tutayajibu maswali yako kuhusu usingizi.

Kwanza, tuwafahamishe kidogo kuhusu usingizi. Utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa, usingizi wa binadamu wakati wa usiku unaundwa na marudio ya vipindi vinne au vitano. Kila kipindi kina sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni usingizi mwepesi (shallow sleep), ya pili ni usingizi mzito (Non Rapid Eye Movement (NREM) sleep), ya tatu ni usingizi wenye kuchezacheza kwa mboni za macho (Rapid Eye Movement (REM) sleep). Baada ya kumalizika kwa sehemu hizo, binadamu huingia tena kwenye usingizi mwepesi na kuanza mzunguko mpya.

Je ni usingizi wa saa ngapi unaofaa zaidi kwa binadamu kila siku? Mkurugenzi wa taasisi ya usingizi ya China ambaye pia ni profesa wa elimu ya fiziolojia wa chuo kikuu cha udaktari cha Anhui Bi. Zhang Jingxing alisema:

"muda wa kutosha wa usingizi kwa siku unatofautiana miongoni mwa watu. Kwa wastani, watu wazima wanahitaji usingizi wa saa 7.5 kila siku. Lakini kwa kawaida watu wanalala saa 6 hadi 9 kila siku. Usizingitie saa ngapi unapaswa kulala kila siku, ila kama utajisikia vizuri katika siku ya pili, basi umepata usingizi wa kutosha."

Kwa jumla, muda wa usingizi unategemea mahitaji ya mwili, na unaweza kuurekebisha kutokana na maono wako, lakini si kwamba muda mrefu zaidi wa uzingizi ni bora zaidi. Utafiti umeonesha kuwa, usingizi wa kupita kiasi unaleta madhara kwa mwili na huenda unaweza kuathiri urefu wa maisha.

Hivyo usingizi wa namna gani ni bora zaidi? usingizi bora unategemea kiasi cha muda wa kipindi cha usingizi mzito. kwa watu wazima wa kawaida, kipindi hicho kinachukua asilimia 15 hadi 20 ya muda wote wa usingizi. Binadamu wakiwa kwenye kipindi cha usingizi mzito, mwili unarekebishwa upya na uhai unafufuliwa.

Profesa Zhang Jingxing aliainisha kuwa, usingizi bora unahitaji tabia nzuri ya usingizi.

"kipindi cha usingizi mzito kitafikia kiasi cha kutosha endapo hutakuwa na mawazo moyoni. Na ni vyema kulala kabla ya saa 4 usiku. Kwa sababu binadamu huanza kuingia kwenye hali ya usingizi saa 4 hivi, kipindi cha usingizi mzito huanzia nusu ya kwanza ya usiku, hali hiyo inahusiana na nyuzijoto ya mwili wa binadamu. Kama ukichelewa kulala, basi kipindi cha usingizi mzito kitapungua."

Profesa Zhang pia aliainisha kuwa, kulala kidogo adhuhuri ni tabia nzuri. Kwa sababu toka asubuhi hadi usiku nguvu ya mwili inaendelea kutumiwa, usingizi mdogo wakati wa adhuhuri unasaidia kupunguza uchovu. Lakini Profesa Zhang alipendekeza kutolala kwa muda mrefu adhuhuri:

"usilale kwa muda mrefu sana, dakika 10 hadi nusa saa inatosha. Kwa sababu ukilala kwa muda mrefu na kuingia kwenye usingizi mzito, itachukua muda kurudisha ufahamu wa kawaida kutoka usingizini kwa kuwa ufahamu hutoweka kikamilifu wakati wa usingizi mzito."

Halafu tujadili kidogo kuhusu masuala kadhaa tutakayayokuta katika usingizi. matatizo ya usingizi yapo ya aina 80 hadi 90 tofauti, kati yao tatizo la kukoroma na kupoteza usingizi ni ya kawaida kabisa. Takwimu husika zinaonesha kuwa, asilimia 20 hadi 30 ya watu wa China wanasumbuliwa na tatizo la kukoroma, na zaidi ya asilimia 40 ya watu wazima wa China wana tatizo la kupoteza usingizi kwa kiasi tofauti. Matatizo hayo yanaathiri vibaya afya ya mwili na roho ya watu. Bw. Deng na Bw. Yang wenye tatizo la kukoroma walisema:

"nimekumbwa na tatizo la kukoroma kwa miaka 5 au 6, nikikoroma hupiga kelele kubwa sana, tatizo hilo limeathiri usingizi wangu, nahisi kizunguzungu mchana. kutokana na kuathiriwa na tatizo hilo kwa muda mrefu, uwezo wangu wa kukumbuka mambo umepungua."

"labda kwa sababu za kikazi, nilikuwa ninasafiri mbali mara kwa mara, hata nilisafiri kwa saa 24 bila kulala hata kidogo. kutokana na hali hiyo, nilianza kupoteza usingizi. wakati huo sikujali tatizo hilo, hivi sasa ninalala kwa saa 3 au 4 kila siku. Nikiwa ni dereva, kutokana na tatizo hilo nina wasiwasi wakati wa kuendesha gari."

Basi tutafanyaje kutatua matatizo hayo? Kwanza tujadili tatizo la kupumua usingizini, yaani tatizo la kukoroma. Naibu mkurugenzi wa idara ya kupumua katika hospitali ya umma ya chuo kikuu cha Beijing Bw. Han Fang alisema,

"kimsingi, kukoroma ni dalili muhimu ya tatizo la kupumua usingizini, lakini si kila mtu anayekoroma ana tatizo hilo. Takwimu husika zimeonesha kuwa, robo ya watu wanaokoroma wana tatizo la kupumua usingizini, na pia kwa wale wanaokoroma na wasio na tatizo hilo, wanaweza kuendelea kuwa na tatizo hilo."

Bw. Han Fang alisema, hivi sasa kuna mbinu nzuri ya kutibu tatizo la kupumua usingizini, njia moja ni matibabu kwa kutumia mashine ya kupumua, nyingine ni matibabu ya upasuaji. Njia hizo mbili zinaweza kutibu vizuri tatizo hilo.

Mwisho, tujadili tatizo la kupoteza usingizi. kuna ufafanuzi bayana kuhusu upimaji na matibabu ya tatizo hilo. Tatizo la kupoteza usingizi linawapata watu ambao hawaridhiki na muda au ubora wa usingizi wao na maisha yao ya mchana huwa yameathiriwa.

Kuna vyanzo vyingi vinavyosababisha tatizo hilo, vikiwemo vyanzo vya kisaikolojia, vya mazingira na magonjwa mengine. Hivyo jambo muhimu katika kutibu tatizo hilo ni kutafuta chanzo halisi. Aidha, ni bora zaidi tatizo hilo likitibiwa mapema zaidi, na watu wenye tatizo hilo lazima waende kupata matibabu hospitalini, wala kamwe wasinunue na kutumia ovyo dawa za usingizi, kwani matumizi ya ovyo ya dawa hizo yanaleta madhara kwa afya.