Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-20 20:56:29    
Waliotegemea misaada ya chakula sasa wabadilika kuwa watu wenye uwezo

cri

Mkoa unaojiendesha wa kabila la Wauyghur wa Xinjiang upo kwenye sehemu ya mpaka wa kaskazini na magharibi mwa China. Kijiji cha Daxi mkoani humo kinapakana na jangwa la Taklimakan. Katika lugha ya Kiuyghur, Daxi ina maana ya "bahari ya chumvi". Hapo awali kijiji hicho kilichopo kwenye wilaya ya Weili, kusini mwa mkoa wa Xinjiang kilijulikana kwa kuwa na watu wengi maskini. Lakini hivi karibuni, inasemekana kuwa asilimia 20 ya watu wa huko wamenunua magari, na nusu yao wanatumia simu za mkononi. Ili kuthibitisha habari hizo, hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alitembelea kijiji cha Daxi.

Mwandishi wetu wa habari alipokuwa karibu na kijiji cha Daxi kinachopakana na jangwa, alishangazwa jinsi alivyoona. "Naona misitu iliyoko nje ya kijiji inakikinga kijiji dhidi ya jangwa. Ndani ya kijiji, nyumba safi za wakazi zimepangwa vizuri, ua wa kila nyumba umejaa maua na majani. Katika ua wa baadhi ya familia, yameegeshwa magari na motokaa mpya. Mashambani kuna miti ya matunda ya aina mbalimbali kama vile mapeasi na zabibu, pamba nyeupe pia inaonekana mashambani. Hali ambayo inaonyesha kuwepo kwa mavuno makubwa."

Baada ya kushuhudia hali hiyo, ni vigumu kuamini kuwa miaka 20 iliyopita, watu wa kijiji cha Daxi walikuwa wanategemea chakula cha misaada kutoka serikalini. Wakati huo huo, Waweiwur wanaochukua asilimia 80 ya idadi ya wakazi wa kijiji hicho, walikuwa wafugaji na wapandaji wa miti ya matunda, na wakulima wengine wa kabila la Wahan walikuwa wanajihusisha na kilimo cha mboga na pamba. Kwa kuwa ardhi ya huko ni ya chumvi, hata kama wanakijiji wakichapa kazi kwa mwaka mzima, walishindwa kujitosheleza kwa chakula. Wanakijiji hao walimwambia mwandishi wa habari kuwa, ni kada Muyghur wa huko Bw. Shawur Mangrik ndiye aliyegeuza hali duni ya kijiji cha Daxi.

Bw. Shawur Mangrik mwenye umri wa miaka 60 aliwahi kuwa mfanyabiasahra, na ni mtu mwenye busara. Miaka 20 iliyopita alichaguliwa kuwa mkurugenzi wa Kamati ya kijiji cha Daxi. Baada ya kufanya utafiti kwa makini, mkurugenzi huyo aliona kwamba, hali mbaya ya kimaumbile si chanzo kikuu cha umaskini kwa watu wa kijiji cha Daxi.

"Wakati ule kulikuwa na watu 920 katika kijiji chetu, ambao walikuwa wanashikilia mtazamo wa zamani, kufuatia njia za zamani kutatua matatizo mbalimbali na kupata ufanisi mdogo. Walikuwa wanalima mashamba bila kutumia teknolojia ya kisasa, kwa uhakika hali hii haiwezi kuleta mavuno."

Mkurugenzi Mangrik alidhamiria kubadilisha mtizamo wa wanakijiji. Aliwachagua vijana wenye mtazamo mpya kuwa wajumbe katika kamati ya kijiji, na kuwaalika wataalamu kuwafundisha wakulima ujuzi wa kilimo, hata kuwasaidia mashambani. Mbali na hayo alipendekeza kwa wanakijiji kufundishana na kusaidiana. Matokeo ya moja kwa moja ya juhudi zake yameonesha kuwa, wanakijiji wakabadilika na kuwa hodari katika shughuli za ufugaji na kilimo cha miti ya matunda, na pia wakawa hodari katika kilimo cha mboga na pamba.

Bw. Mangrik pia alianzisha semina kwa wanakijiji. Alisema, "Katika kijiji chetu yalianzishwa mafunzo ya kusoma na kuandika kwa wakulima. Katika majira ya baridi ambapo shughuli za kilimo zinapungua sana, wanakijiji walishiriki kwenye mafunzo, wakifahamishwa mambo makubwa ya nchini na ya kimataifa, hususan habari za sayansi na teknolojia ya kilimo. Hadi kufikia mwaka 1997, kijiji chetu kilikuwa hakina mtu asiyejua kusoma wala kuandika."

Baada ya kupata habari nyingi kutoka nje na ujuzi mwingi wa sayansi na teknolojia, baadhi ya vijana wenye elimu wa kijiji cha Daxi walitambua kuwa, hawawezi kujipatia pesa kwa kutegemea kilimo na ufugaji tu. Walikusanya habari za masoko kutoka sehemu mbalimbali mkoani Xinjiang, pia walianzisha kiwanda cha kusaga unga, kiwanda cha kutengeneza matofali, shamba la mifugo, soko la mazao ya kilimo na kituo cha kilimo cha mboga ndani ya vibanda vyenye hali ya joto. Shughuli hizo zilipamba moto kwa haraka kwa kuwa, zinategemea maliasili ya huko, zinahitaji vitega uchumi vidogo na mazao yanayohusika yana soko kubwa.

Kijana Mohamed Shawur mwenye umri wa miaka 35 anajulikana kwa uhodari wa kuchuma pesa katika kijiji cha Daxi. Kijana huyo alisema baada ya kushiriki kwenye mafunzo kadhaa yaliyoandaliwa na kamati ya kijiji, mavuno ya shamba la pamba la familia yake yaliongezeka na hivyo mapato yaliongezeka. Kuanzia hapo kila mwaka alikuwa ananunua na kusoma vitabu vya elimu ya kilimo na mifugo. Hivi sasa anafahamu kutumia mtandao wa Internet kujipatia habari za teknolojia, akisaidiwa na fundi wa kilimo, si kama tu anapanda pamba, bali pia anapanda mapeasi, na kuweka vitega uchumi katika kujenga mashamba ya mifugo yenye hali ya juu, ili kuendeleza shughuli za ufugaji.

Mbali na hayo, Bw. Mohamed anaeneza ujuzi na teknolojia miongoni mwa wanakijiji wenzake. Kutokana na pendekezo lake, wanakijiji wenye elimu ya sekondari wanatakiwa kushiriki kwenye mafunzo ya sayansi na teknolojia yanayofanyika kwa miezi miwili kila mwaka wakati wa majira ya baridi.

Kutokana na uhimizaji wa vijana kadhaa waliojipatia pesa, watu wa kijiji cha Daxi walibadilika sana. Kijana Mohamed alisema, hapo awali wanakijiji walipokutana walipenda kulalamikia umaskini na ugumu wa maisha, lakini hivi sasa wanazungumzia teknolojia na kubadilishana mbinu za kujipatia fedha.

Miaka mitatu iliyopita, Bw. Mohamed Shawur alipewa tuzo ya kijana ya May 4, ambayo ni tuzo ya kwanza kwa vijana hapa nchini China, na alikutana na viongozi wa taifa. Kijana huyo alipokumbusha tukio hilo, alionekana kusisimka sana.

Alisema, "Siku hiyo rais Hu Jintao alinishika mkono na kuniuliza, 'Je, unatoka kabila dogo mkoani Xinjiang?' Nilimjibu, 'Naam, natoka kijiji cha Daxi, mkoani Xijiang.' Rais aliongeza kuwa, 'Wewe ni kada anayetoka eneo la vijiji, unapaswa kuwaongoza wanakijiji wenzako kuchapa kazi, na msisahau kuendelea kujifunza.' Nilimwambia, 'Nafuata agizo lako. Hakika nitakaporudi maskani yangu, nitajifunza bila kusita na kuwaongoza watu wenzangu kufanya kazi kwa bidii."

Hivi sasa kati ya familia 310 katika kijiji cha Daxi, familia karibu 70 zimenunua magari, kila familia ina motokaa, na zaidi ya nusu ya wanakijiji wanatumia simu za mikononi. Mwaka 2004, wastani wa mapato ya wanakijiji ulikuwa Renminbi Yuan 6,300, sawa na dola za kimarekani 800 hivi. Kijiji cha Daxi kimebadilika kuwa kijiji kilichoendelea kuliko vingine katika sehemu ya kusini ya mkoa wa Xinjiang.

Idhaa ya Kiswahili 2006-04-20