Rais Hu Jintao wa China tarehe 19 huko Seattle, Marekani aliandaliwa tafrija ya adhuhuri na watu wa sekta za viwanda na biashara na marafiki wa jimbo la Washington na mji wa Seattle, ambapo alitoa hotuba muhimu akieleza vilivyo sera na mapendekezo ya China juu ya maendeleo ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani.
Tangu China na Marekani zianzishe uhusiano wa kibalozi mwaka 1979, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili umeendelea kwa kasi, ambapo thamani ya biashara ya pande hizo mbili ziliongezeka zaidi ya mara 80. Rais Hu alisisitiza kuwa, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara unaoendelea kwa haraka kati ya China na Marekani umeleta manufaa halisi kwa wananchi wa nchi hizo mbili. Uzoefu umeonesha kuwa, ushirikiano huo ni nguzo kubwa katika maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Rais Hu Jintao alidhihirisha kuwa, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili uliendelea kwa haraka kwenye sekta mbalimbali, hivyo kuwepo kwa matatizo kadhaa ni hali ya kawaida, kwani ushirikiano wa kunufaishana na kutafuta maendeleo ya pamoja siku zote ni mwelekeo mkuu katika uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani. Pande hizo mbili zinapaswa kufanya majadiliano na mazungumzo katika hali ya usawa na kupanua ushirikiano wa kunufaishana ili kutatua kwa mwafaka matatizo yanayotokea.
Kuhusu hali isiyo ya uwiano ya biashara kati ya nchi hizo mbili ambayo inafuatiliwa sana na upande wa Marekani, rais Hu alisema:
China inashikilia sera ya kupanua mahitaji nchini, na kuichukua sera hiyo kuwa msingi wa kusukuma mbele maendeleo ya uchumi na jamii. China itaongeza ruhusa kwa bidhaa na huduma za Marekani kuingia kwenye soko la China, wakati huo huo China inaitaka Marekani ichukue hatua katika kupunguza vizuizi kwa bidhaa za China zinazouzwa nchini humo na kupunguza vitendo vyake vya uhifadhi wa kibiashara, na kuitaka Marekani ihimize bidhaa za Marekani ziiuzie China ili kusaidia kutatua hali isiyo ya uwiano ya biashara kati ya nchi hizo mbili.
Kuhifadhi hakimiliki ya ujuzi ni maslahi ya pamoja ya nchi mbalimbali duniani, pia ni mahitaji ya China katika kuzifungulia mlango zaidi nchi za nje, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha uwezo wa kufanya mavumbuzi kwa kujitegemea. Juu ya hayo, rais Hu Jintao alisisitiza:
China inashikilia kithabiti msimamo wa kuhifadhi hakimiliki ya ujuzi na kupiga vita vitendo vya kurudufu bidhaa. China itaendelea kukamilisha mfumo wa sheria wa uhifadhi wa hakimiliki ya ujuzi, kuongeza nguvu ya kutekeleza sheria, kutoa adhabu kwa vitendo vya aina mbalimbali vya ukiukwaji wa hakimiliki ya ujuzi, na kulinda haki na maslahi waliyo nayo watu wa nchi mbalimbali wenye hakimiliki ya ujuzi nchini China.
Kiwango cha ubadilishaji wa fedha za Renminbi za China pia ni suala moja linalofuatiliwa sana na upande wa Marekani, juu ya hilo rais Hu Jintao alisema:
China siku zote inawajibika kwa makini, ikithibitisha utaratibu wa ubadilsihaji wa fedha zake unaolingana na hali halisi ya maendeleo ya uchumi na jamii ya China na hali ya utulivu ya uchumi na fedha ya dunia nzima. China itasukuma mbele mageuzi ya mambo ya fedha na kukamilisha utaratibu husika kwa kudumisha utulivu wa kimsingi wa ubadilishaji wa fedha za Renminbi katika kiwango halali na cha uwiano.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Microsoft Bwana Bill Gates, Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya ndege za abiria ya Boeing Bwana Alan Mulally na marafiki wa sekta mbalimbali wa China na Marekani wapatao 600 walihudhuria tafrija hiyo ya adhuhuri.
Bwana Bill Gates katika risala yake alisema, China inayofungua mlango na yenye usitawi italeta manufaa kwa nchi mbili za Marekani na China na dunia nzima kwa ujumla. Ameeleza imani yake kuwa ziara hiyo ya rais Hu Jintao hakika itaongeza maelewano na mawasiliano kati ya nchi hizo mbili.
Idhaa ya Kiswahili 2006-04-20
|