Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-21 16:51:43    
Tofauti kati ya Russia na Marekani kuhusu suala la nyuklia la Iran imekuwa ya wazi zaidi

cri

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Bw. Mikhail Kamynin tarehe 20 huko Moscow alitangaza kuwa Marekani haina msingi wowote wa kisheria kuitaka Russia isimamishe ushirikiano na Iran katika kituo cha umeme cha nyuklia kilichopo Bushenr nchini Iran. Wachambuzi wanaona kuwa hii inadhihirisha kwamba tofauti kati ya nchi hizo mbili imekuwa ya wazi zaidi kadiri suala la nyuklia la Iran linavyozidi kuchelewa kutatuliwa.

Marekani ilitoa maombi hayo baada ya mkutano wa wajumbe wa nchi za Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani kufanyika tarehe 18 bila matokeo yoyote. Mjumbe wa Marekani aliyehudhuria mkutano huo ambaye ni naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Nicholas Burns tarehe 19 aliitaka Russia isimamishe ushirikiano wa kinyuklia na Iran, huku akitaka nchi zote zisimamishe kutoa msaada wa bidhaa zenye matumizi ya aina mbili kwa Iran.

Kuhusu maombi hayo aliyosema naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Bw. Kamyinin alisema, ni Baraza la Usalama la Umoja wa wa Mataifa tu ndio inayo haki ya kusimamisha ushirikiano wa nchi fulani na nchi nyingine katika nyanja fulani, lakini mpaka sasa baraza hilo halijatoa uamuzi wowote kuhusu ushirikiano wa kinyuklia wa Iran na nchi nyingine. Aliongeza kusema, teknolojia ya kituo cha umeme cha nyuklia kilichopo katika Bushenr haiwezi kutengeneza silaha za nyuklia, na kwamba kituo hicho hakina uhusiano wowote na shughuli za kusafisha uranium.

Sambamba na hayo, baada ya mkuu wa jeshi la Russia Yuri Baluyevsky alipozungumza na jemadari mkuu wa jeshi la muungano la Ulaya la NATO Richard Johns tarehe 19 alisema, iwapo Marekani itashambulia Iran, Russia haitaunga mkono upande wowote. Na kwamba Russia itaendelea kutekeleza mkataba wa kutoa makombora ya kukinga anga kwa Iran. Mkataba huo ulitiwa saini mwishoni mwa mwaka jana, thamani yake ni dola za Kimarekani bilioni 1.4. Kwa mujibu wa mkataba huo, Russia itasaidia Iran mfumo wa seti 30 za makombora dhidi ya mashambulizi ya anga. Mfumo huo unaweza kulinda vituo muhimu vya kijeshi nchini Iran vikiwa ni pamoja na vituo vilivyopo katika Tehran na Bushenr.

Mkataba wa Kutoenea kwa Silaha za Nyuklia ni kanuni ya kimsingi inayokubalika duniani. Kwa hiyo, kuipinga Iran kutengeneza silaha za nyuklia ni msimamo wa pamoja wa jumuyia ya kimataifa. Lakini kwa njia gani na namna ya kulishughulikia suala la nyuklia la Iran ni jambo linalohusu maslahi na sera za mataifa mbalimbali. Russia inafuata kanuni za kimtaifa za demokrasia na amani na inatetea kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia, na Marekani inashikikilia kuiwekea Iran vikwazo na hata kutumia nguvu za kijeshi.

Wachambuzi wanaona, tofauti kati ya Russia na Marekani kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la Iran imedhihirisha malengo ya mkakati na maslahi tofauti ya nchi hizo. Marekani inajitahidi kushirikisha mataifa makubwa kwa lengo la kushinikiza na kuzuia Iran isipate silaha za nyuklia ili kulinda maslahi yake binafsi na kuhakikisha nafasi yake ya ubabe duniani. Kutokana na kuwa Russia ina maslahi yake makubwa ya kiuchumi na kimkakati nchini Iran inatofautiana na Marekani na kupinga kuiwekea Iran vikwazo na kutumia nguvu za kijeshi, na kwa kupitia juhudi zake za diplomasia yenye uhuru wa kujiamulia mambo inaweza kuongeza athari yake duniani na kurudisha na kuhifadhi sura yake ya taifa kubwa duniani. Kwa hiyo, Russia na Marekani ingawa zina msimamo wa namna moja kwa kiasi fulani lakini kwa undani kila moja ina lengo lake. Kutokana na hayo, mbele ya tatizo sugu la nyuklia la Iran, Russia na Marekani zitaendelea kuhitilafiana.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-21