Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-21 19:40:46    
Rais Hu Jintao atoa mapendekezo 6 juu ya kusukuma mbele ushirikiano wa kiujenzi kati ya China na Marekani

cri

Rais Hu Jintao wa China ambaye yuko Marekani kwa ziara ya kiserikali tarehe 20 usiku huko Washington alitoa hotuba kwa makundi ya kirafiki ya Marekani, ambapo alitoa mapendekezo 6 juu ya kusukuma mbele ushirikiano wa kiujenzi kati ya China na Marekani.

Usiku wa siku hiyo, wajumbe zaidi ya 900 kutoka katika Kamati ya biashara ya Marekani na China, Kamati ya uhusiano kati ya Marekani na China, Shirikisho la wafanyabiashara la Marekani na Taasisi ya Brookings Institution walikusanyika pamoja na kumwandalia karamu ya usiku, watu wengine mashuhuri wa Marekani wakiwemo waziri wa kazi wa Marekani Bibi Elaine Chao , na waziri wa zamani wa mambo ya nje Bwana Henry Kissinger na wengineo pia walihudhuria karamu hiyo.

Bwana Kissinger alipotoa risala alisema, kama hakuna ushirikiano barabara kati ya Marekani na China, basi ni vigumu kutimiza utaratibu mzuri wa kimataifa ulio mkamilifu. Bwasna Kissinger aliisifu China kwa kushika njia ya maendeleo ya amani, na kusifu sana ziara hiyo ya rais Hu Jintao nchini Marekani. Alisema:

Mheshimiwa rais, ziara yako hii itaimarisha zaidi urafiki kati ya Marekani na China, na nchi hizo mbili zitafanya juhudi kwa pamoja ili kutoa mchango kwa amani na maendeleo ya dunia.

Baadaye rais Hu Jintao alipotoa hotuba alisema, China inafuata kithabiti njia ya maendeleo ya kiamani, itakusanya nguvu zote kufanya ujenzi nchini, na kutafuta maendeleo kwa moyo wote, ambapo itajitahidi kulinda amani ya dunia na kusukuma mbele maendeleo ya pamoja. Alisema:

Jukumu la sasa la dharura zaidi la China ni kukusanya nguvu katika kuendeleza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi siku hadi siku. China inahitaji zaidi kupata mazingira ya amani ya kimataifa. Ni matumaini yetu kuwa, China itajiendeleza kwa kupitia juhudi za kulinda amani, na maendeleo ya China pia yatahimiza amani ya dunia.

Rais Hu Jintao aliongeza kuwa, Katika miaka 27 iliyopita tangu China na Marekani zianzishe uhusiano wa kibalozi, kwa ujumla uhusiano kati ya nchi hizo mbili unaendelea siku hadi siku. Urafiki wa China na Marekani ni matumaini ya pamoja ya wananchi wa nchi hizo mbili, na ushirikiano wa kunufaishana ni chaguo sahihi la nchi hizo mbili. Nchi hizo mbili zinapaswa kuzingatia na kushughulikia uhusiano kati yao kwa mtizamo wa kimkakati na kutafuta ushirikiano wa kunufaishana, ili kuhakikisha ushirikiano wa kiujenzi uendelee kwenye njia sahihi iliyo ya utulivu. Juu ya hayo, rais Hu Jintao alitoa mapendekezo 6 kama yafuatayo:

Kuongeza maelewano, kupanua maoni ya pamoja na kujenga ushirikiano wa kiujenzi wa muda mrefu ulio wa utulivu; kushika fursa na kupanua mtizamo, kuimarisha na kuongeza msingi wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara; kufuata kanuni, kutimiza ahadi na kushughulikia mwafaka kwa suala la Taiwan kwenye msingi wa taarifa tatu za pamoja za China na Marekani; kufanya majadiliano mara kwa mara, kukabiliana na changamoto, na kuimarisha mawasiliano na uratibishaji katika masuala makubwa ya kimataifa na kikanda; kufundishana, kusaidiana na kuongeza maingiliano ya kirafiki kati ya wananchi wa China na Marekani; kuheshimiana, kutendeana kwa usawa, na kushughulikia migongano kwa mtizamo sahihi.

Rais Hu Jintao pia alijulisha malengo makuu ya maendeleo ya China katika siku zijazo.

Mwishoni rais Hu Jintao alinukuu maneno aliyosema rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt kwamba, dunia inaweza kubadilika kutokana na juhudi za binadamu, na juhudi za binadamu zinaweza kuvumbua mambo mengi mapya na mazuri zaidi. Ameeleza imani yake kuwa, kujenga dunia yenye amani ya kudumu na usitawi wa pamoja kunahitaji uhusiano wa China na Marekani unaoendelea vizuri katika hali ya utulivu.

Idhaa ya Kiswahili 2006-04-21