Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-21 20:47:22    
Wasikilizaji wa Kenya waionavyo uhusiano kati ya China na Kenya

cri

China na Kenya zina historia ndefu ya urafiki, mawasiliano ya kiutamaduni kati ya nchi hizo mbili yalianza wakati msafiri mkubwa wa China Bw. Zheng He alipoongoza kikosi kikubwa cha merikebu kufika Kenya kabla ya miaka 600 iliyopita. Katika miaka zaidi ya 40 iliyopita tangu China na Kenya zianzishe uhusiano wa kibalozi, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili umeimarishwa, na urafiki na maelewano kati ya watu wa nchi hizo mbili pia umezidishwa. Ifuatayo ni mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari wa Kenya Bwana Ali Hassan na baadhi ya wasikilizaji wetu wa huko Kenya kuhusu uhusiano kati ya China na Afrika.

Bw. Mradi E. Mradi ni mfanyabiashara wa huko Nairobi, alitoa maelezo yake kuhusu ushirikiano uliokuwepo kati ya China na Afrika na faida ambazo mkenya anazipata kutoka kwa China. Akisema:

"Sisi sote tunajua kwamba China ni dola kubwa, China ina idadi kubwa ya watu na eneo kubwa la ardhi, China ina athari kubwa katika jukwaa la kimataifa na Umoja wa Mataifa. China ilikuwa nchi kubwa na itakuwa nchi kubwa duniani. Lakini kama sisi tujuavyo, propaganda zilizotolewa na vyombo vya habari vya nchi za magharibi na mambo ya utawala wa makoloni ya magharibi yalikuwa yameharibu historia nyingi ya sehemu nyingine. Lakini sasa wachina wenyewe wamefanya bidii waje katika ulimwengu wa kisiasa, walete mambo ya kisasa. Sisi tumepata msaada mwingi kutoka kwa China, wametusaidia mambo mengi kama kujenga studio. Sisi tungependelea kwamba, China pia watusaidie kwa mambo ya shule na mambo ya elimu, kutuwezesha kuuza bidhaa zetu kule nchini China. Na kwa sasa tuombe kwamba wachina waangalie sana upande wa siasa. Hapa Kenya kama sisi sote tunavyojua, rais wetu na nchi yetu sasa yapata taabu kutoka nchi za magharibi, kwa hiyo serikali yetu imetoa sera ya kuelekea mashariki. Mimi kama mmoja wa wakenya ningeomba nchi za mashariki hasa China waje watusaidie sisi tutoke katika hii balaa, na tuwezeshe sisi tujenge taifa letu ili tufaidi sisi sote."

Bwana Swai Mdoe ni mtangazaji na mhariri wa habari wa kituo cha televisheni cha Kenya KTN. Alisema, hajafika China, lakini wachina wengi wamefika Kenya, wameleta biashara, hata kuzindua kituo cha FM huko Nairobi, hayo ni mwelekeo mzuri. Akisema:

"Wachina wamefanya mambo mengi nchini Kenya, wamejenga madaraja, wamejenga mabarabara, na wamejenga uwanja wa michezo wa Kasarani. Usingekuwa na uhusiano mzuri, wasingekuja wachina wengi ambao wameleta bidhaa na kufungua vituo vingi vya biashara hapa jijini na sehemu mbalimbali nchini."

Bwana UK kwa maneno yake mwenyewe ni kijana anayetafuta masoko, alisema kuwa, kuzinduliwa kwa kituo cha FM cha Radio China Kimataifa kunaleta faida nzuri kwa sababu sasa kuna ushirikiano mkubwa kati ya China na Kenya, hasa kwa mambo ya biashara. Akisema:

"Mimi kama mpenzi wa biashara nitafaidika sana kwa kujua yanayotendeka kati ya nchi yetu na China, na vile ninaweza kujua wafanyabiashara na bidhaa kutoka Uchina kuja Kenya."

"Nikiangalia maisha yangu ilivyo, vitu vitakavyonifurahisha zaidi ni mambo ya biashara, hasa biashara kati ya Kenya na China. Wanatuletea bidhaa za bei nafuu, ndiyo watu wanaanza kupenda wachina kwa sasa, siku moja ningependa kuwa agent ya wafanyabiashara wa China hapa Kenya. Niliwahi kufanya kazi Tanzania na nimeweza kuhusiana na wafanyabiashara wa China kule, naona japokuwa China ina utamaduni tofauti na sisi, lakini wachina ni watu wenye busara, sioni ugumu wa kuwasiliana nao."

Idhaa ya Kiswahili 2006-04-20