Milipuko mitatu ilitokea tarehe 24 usiku kwenye sehemu maarufu ya utalii iliyoko katika penisula ya Sinai nchini Misri, Dahab milipuko hiyo iliua watu zaidi ya 30 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 150. Milipuko hiyo imeleta pigo kubwa kwa hali ya usalama na sekta ya utalii nchini Misri, ambayo imekumbusha mfululizo wa milipuko iliyotokea katika eneo la Sharm el-Sheikh.
Milipuko hiyo ilitokea karibu katika wakati mmoja mnamo saa 1 usiku wa tarehe 24 kwenye soko la watalii, migahawa na supa-maketi za mji wa zamani wa Dahab. Habari zinasema, milipuko hiyo imetokana na mabomu yaliyotegewa wala siyo mashambulio ya kujitoa muhanga.
Milipuko hiyo ilitokea katika siku kuu ya kijadi ya Misri inayojulikana kama Sham al Naseem Festival, na siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya ukombozi ya penisula ya Sinai ya Misri, na siku chache kabla ya hapo zilikuwa siku kuu ya kidini ya wayahudi na siku kuu ya wakristo Pasaka, hivyo watu wa Misri walikuwa katika mapumziko ya siku nyingi na kufurahi shamrashamra za siku kuu, ambazo ziliwavutia watalii wengi wa kutoka nchi za nje. Mji wa Dahab uko umbali wa kilomita 85, kaskazini ya Sharm el-Shaikh, mji maarufu wa shughuli za utalii nchini Misri, na pia ni mahali pa kupumzika kwa watalii. Milipuko ilipotokea, kulikuwa na watembea kwa miguu na watalii wengi, hivyo milipuko ilisababisha vifo na majeruhi wengi wakiwemo baadhi ya watalii wa nchi za kigeni.
Shughuli za kuwaokoa majeruhi zilifanyika kwa haraka na kuongozwa moja kwa moja na waziri mkuu wa Misri Bw. Ahmed Nazif, waziri wa mambo ya ndani naye alifika Dahab kwa haraka. Msemaji wa wizara ya afya ya Misri siku hiyo alisema, katika muda wa saa chache baada ya milipuko kutokea, magari zaidi ya 80 ya wagonjwa yaliwakimbiza majeruhi hospitalini, wakati ndege iliyochukua vikundi vitatu vya madakatari ilikwenda Sharm el-Sheikh. Licha ya hayo, kikundi cha wataalamu wa kesi za jinai na milipuko pia walifika mahali palipotokea milipuko kufanya uchunguzi.
Rais Hosni Mubarak wa Misri aliagiza idara husika kujitahidi kuwaokoa majeruhi walioumizwa katika milipuko hiyo. Alieleza huzuni na masikitiko yake kuhusu watu waliopoteza maisha yao katika milipuko na kutoa salamu za rambirambi kwa jamaa za watu waliojeruhiwa na waliopoteza maisha katika milipuko hiyo. Alisisitiza, watu wa Misri lazima watawapata na kuwaadhibu vikali wale magaidi waliozusha matukio ya milipuko. Nchi nyingi zikiwemo Israeli, Joden, Palastina, Katar, Libya, Syria na Marekani, zilitoa salamu za pole kwa Misri kwa shambulio hilo la kigaidi.
Milipuko hiyo iliyotokea Dahab ni shambulizi la tatu kutokea ndani ya mwaka mmoja na nusu uliopita. Mfululizo wa milipuko iliyotokea mwezi Okatoba mwaka 2004 mjini Taba, mji ulioko kwenye sehemu ya mpaka nchini Misti uliua watu 34 na kuwajeruhi watu zaidi ya 150, ambao wengi wao walikuwa raia wa Israeli waliokwenda kupumzika katika mji wa Taba. Mwezi Julai mwaka uliopita, milipuko mikali ilitokea tena kwenye Sharm el-Shaikh, mji maarufu wa shughuli za utalii ulioko kando ya bahari ya Sham nchini Misri, milipuko hiyo mitatu iliyotokea katika muda mfupi kwenye sehemu zenye watu wengi iliua watu 67 na kujeruhi watu zaidi ya 200. kitu kinachopaswa kutupiwa macho ni kuwa siku ile iliyotokea milipuko kwenye Sharm el-Seikh ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya miaka 53 tangu iasisiwe nchi ya Misri, na siku inayofuata ya siku iliyotokea milipuko safari hiyo kwenye mji wa Dahab, ni siku ya maadhimisho ya ukombozi wa Sinai. Hivi sasa bado hakuna chama au mtu yeyote aliyetangaza kuhusika na milipuko hiyo, lakini ni dhahiri kwamba magaidi waliofanya mashambulizi hayo walichagua kwa makusudi siku zenye umuhimu mkubwa.
|