Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-26 16:50:05    
Kwa nini Iran inatishia kwa kueneza teknolojia ya nyuklia?

cri

Kiongozi wa kiroho wa Iran Ali Khamenei tarehe 25 mwezi huu alipokutana na rais wa Sudan Omar Al-Bashir alisema, "Iran itaeneza uzoefu, elimu na teknolojia ya wanasayansi wa Iran kwa nchi nyingine". Wachambuzi wanaona kuwa Iran inasema hayo ikilenga kuzionya nchi za magharibi kutafakari zaidi zinapojaribu kuitiishia Iran wakati ambapo siku ya tarehe 28 imekaribia kabla ya mratibu mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki Bw. Baradei kutoa ripoti kuhusu suala la nyuklia la Iran.

Sanjali na Bw. Khamenei, siku hiyo pia mjumbe wa kwanza wa Iran wa mazungumzo ya suala la nyuklia Bw. Ali Larijani alisema, kama Iran itaadhibiwa na Baraza la Usalama, itasimamisha uhusiano wake na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na kujitoa kutoka "mkataba wa kutoenea kwa silaha za nyuklia", na kwamba hata Iran ikishambuliwa kijeshi, pia haitaacha mpango wake wa nyuklia ila tu kuufanya upango huo ulio wazi sasa uwe wa kichini chini. Siku moja kabla ya siku hiyo, rais wa Iran Mahmoud Ahmadine kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, nchi za magharibi zisikosee kufikiri kwamba zinaweza kushinikiza Iran kwa kupitia Baraza la Usalama, na Baraza la Uslama linapaswa kutatua suala la nyuklia la Iran kwa mujibu wa sheria. Iwapo nchi za magharibi zitajaribu kuinyima Iran haki ya kumiliki nyuklia, basi Iran itazingatia upya sera zake za nyuklia.

Wachambuzi wanaona kuwa sababu za Iran kuchukua msimamo mkali kama huo ni kwamba hivi sasa haijakiuka "kizingiti cha nyuklia", na Baraza la Usalama haliwezi kuichukulia hatua. Kwa sababu: Kwanza, Iran bado inaonekana inafuata "mkataba wa kutoenea kwa silaha za nyuklia", na kukubali ukaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki. Kwa hiyo, kinadharia Iran ina haki ya kusafisha uranium.

Pili, Iran inaona nchi za magharibi zinaibagua Iran katika suala la nyuklia. Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni unaonesha kwamba, 85.4% ya watu wa Iran wanaona njia nzuri ya kutatua suala la nyuklia la Iran ni kuendelea na shughuli za nyuklia. Wanasema, nchi za Israel, Afrika ya Kusini, India na Pakistan, zote zimekubaliwa kimya kimya na jumuyia ya kimataifa kuwa na nyuklia, hata Marekani na India zimetia saini ushirikiano wa nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia, Ufaransa pia itatangaza kusaidia Libya mradi wa nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Nchi nyingi kama hizo zinaruhusiwa, kwa nini Iran isiruhusiwe? Huu ni ubaguzi wa nchi za magharibi kwa Iran.

Tatu, Baraza la Usalama lina maoni tofauti kuhusu suala la nyuklia la Iran, kwa hiyo si rahisi kwa Marekani kupata azimio la kuiadhibu Iran kutoka Baraza hilo. Russia inapinga moja kwa moja kuiadhibu Iran kutokana na mambo ya siasa na maslahi yake makubwa ya kiuchumi. Licha ya Russia, katika miaka ya karibuni, Iran karibu imeshirikisha mataifa yote makubwa kwenye soko lake la mafuta na "kuyaunganisha pamoja kwenye maslahi", kila mataifa hayo yanapotakiwa kufanya uamuzi kuhusu suala la Iran, kila moja huzingatia kwa makini maslahi yake.

Aidha, Marekani hakika haitavumilia Iran iendelee na teknolojia yake ya nyuklia, kwa sababu inachukulia Iran kuwa ni moja ya "nchi za uovu" na ni chimbuko la ugaidi. Kadhalika, Marekani inaona, pindi Iran ikidhibiti teknolojia ya nyuklia, nchi nyingine zenye tamaa na nyukia zitafuata, kama hivyo ndivyo mfumo wa kimataifa wa kutoenea kwa silaha za nyuklia utabaki kwa maneno tu. Kutokana na sababu hizo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Rice alipozungumza na Khamenei tarehe 25 alionesha wasiwasi kuhusu Iran kutaka kueneza teknolojia ya nyuklia. Magazeti ya Ulaya yanaona kuwa, nia ya tangazo kama hilo la Iran ni kuzionya nchi za magharibi, hasa Marekani, zisichukue hatua bila ya kuwa makini.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-26