Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-27 15:35:18    
Suala la nyuklia la Iran limekwama vibaya

cri

Kwa mujibu wa taarifa ya mwenyekiti wa Baraza la Usalama iliyopitishwa tarehe 29 Machi, tarehe 28 mwezi huu ni siku ya mwisho kwa Iran kusimamisha shughuli zote za kusafisha uranium. Katika muda wa mwezi mmoja, Iran kwa mara nyingi ilikataa taarifa hiyo, na nchi za magharibi, hasa Marekani, zilishughulika sana kidiplomasia kwa ajili ya kuiadhibu Iran. Hivi sasa dalili nyingi zinaonekana kwamba suala la nyuklia la Iran limekwama vibaya.

Taarifa ya mwenyekiti wa Baraza la Uslama imesema, mratibu mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki atawasilisha ripoti mpya kwenye Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na Baraza la Usalama kuhusu suala la nyuklia la Iran katika siku ya tarehe 28. Siku hizi, vyombo vya habari vinafanya ufafanuzi na makadirio, kwamba ripoti hiyo itakuwaje. Magazei mengi yanaona kwamba ripoti hiyo haitasaidia Iran. Kwa sababu, Iran licha ya kuwa haijasimamisha shughuli zake za kusafisha uranium, tena tarehe 11 mwezi Aprili ilitangaza kuwa imefanikiwa kupata uranium safi kwa kiwango cha chini.

Siku chache zilizopita, maofisa wa Iran walionesha msimamo mkali katika nyakati na mazingira tofauti. Tarehe 26 rais Mahmoud Ahmadine alisisitiza kwamba Iran haitarudi nyuma mbele ya taarifa ya Baraza la Usalama iliyotaka Iran kusimamisha shughuli za kusafisha uranium. Kiongozi wa kiroho wa Iran Ali Khamenei katika siku hiyo pia alisema, "Marekani lazima ifahamu ikisahmbulia Iran itapata hasara katika kila pembe ya dunia, na Iran italipiza kisasi mara dufu kujibu mashambulizi yake."

Katika siku hiyo, ujumbe ulioongozwa na mwenyekiti wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ulifanya mazungumzo na naibu mratibu mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki huko Vienna na kujadiliana namna ya kutatua suala la nyuklia la Iran. Wanadiplomasia wa Vienna waliona kuwa, mazungumzo hayo hayakupata matokeo yoyote ya maana, lakini huenda yakaathiri ripoti itakayowasilishwa kwenye Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na Baraza la Usalama.

Hivi sasa, vyombo vya habari vinafuatilia zaidi Marekani itachukua hatua gani kuukabili msimamo mkali wa Iran. Marekani inaichukulia Iran kama ni moja ya "nchi za uovu" duniani. Katika ripoti kuhusu "Mkakati wa Usalama wa Taifa" iliyotolewa na ikulu hivi karibuni, rais Bush alisema kinaganaga kwamba "Iran ni tishio kubwa kwa Marekani". Kwa mtazamo wa mbali, "kutuliza" Iran ni moja ya malengo ya mkakati ya Marekani katika Mashariki ya Kati, kwa hiyo Marekani hakika itachukua hatua za kila aina ikiwemo "ushambulizi wa ghafla wa kijeshi".

Lakini wataalamu walio wengi wanaona kuwa, hivi sasa Marekani haina uwezo wa kuishambulia Iran kwa nguvu za kijeshi. Kwa sababu, kwanza, Iraq imekwisha kuizamisha Marekani ndani ya matope isiweze kujinasua, wananchi wa Marekani hawatakubali serikali ya Marekani ichukue hatua za kijeshi bila ya uhakika wa ushindi. Na cha muhimu zaidi ni kuwa, ingawa hivi sasa matendo ya Iran yamekaribia mstari wa mwisho wa Marekani, hata hivyo shughuli za kusafisha uranium nchini Iran bado zinakuwa katika kipindi cha utafiti; Pili, usafi wa uranium nchini Iran bado ni wa kiwango cha chini, na uranium inayoweza kutumika katika kutengneza silaha za nyuklia lazima uwe safi wa kiwango cha juu. Kwa hiyo, rais Bush na maofisa wengine walisema, hivi sasa Marekani inapendelea kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia, lakini pia inasisitiza kuwa haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi.

Wachambuzi wanaona kwamba, kwa sababu Russia, China na nchi nyingi nyingine zinatofautiana na nchi za magharibi, hasa Marekani, katika suala la nyuklia la Iran, haitakuwa rahisi kwa Baraza la Usalama kufikia maoni ya namna moja katika muda mfupi. Kwa kukabiliwa na sakama la suala hilo la nyuklia la Iran, kila upande unapaswa kuwa na subira na kulikabili suala hilo kwa makini na tahadhari, kushikilia njia ya mazungumzo na kuendelea kufanya juhudi kutatua suala hilo kwa njia ya amani.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-27