Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-27 16:19:36    
Wanawake wazee na kundi la ngoma la "machweo mazuri"

cri

Wanawake wazeeWachina wanapenda kipindi cha uzee ni kama machweo. Hivi sasa katika mji wa Tangshan, uliopo kaskazini ya China kuna kundi moja la ngoma liitwalo "machweo mazuri" ambalo linawavutia watu kutokana na ngoma yake maalumu, na wachezaji ngoma wote ni wanawake wazee wenye wastani wa umri wa karibu miaka 70 . Mwezi Januari mwaka huu, wazee hao walialikwa na kituo cha televisheni cha taifa la China kucheza ngoma kwenye kipindi maalumu cha tamasha la mkesha wa mwaka mpya wa jadi wa China, jambo ambalo limefanya kundi la "machweo mazuri" lijulikane kote nchini.

Ngoma maalumu ya kundi hilo inaitwa ngoma ya Piying. Piying ni aina ya mchezo maarufu wa jadi wa sanaa unaojulikana kwa Wachina. Katika mchezo huo wa sanaa, ngozi za punda na ng'ombe huwa zinatumika kutengeneza vikaragosi, na wachezaji wanachezea vikaragosi hivyo nyuma ya pazia huku mwangaza ukipitia kwenye vikaragosi na kupata kivuli kinachooneshwa kwenye pazia. Ngoma ya Piying ni ngoma ya kuiga umaalumu wa vitendo vya vikaragosi vya mchezo huo.

Wazee wa kundi la ngoma la "machweo mazuri" waliwavutia watu wengi kwa kucheza ngoma ya Piying, ambayo ina midondo dhahiri na vitendo vinavyowachekesha watu. Msichana Zhang Xiaole alisema, "Kundi la 'machweo mazuri' linawavutia watu sana. Nilitizama ngoma ya Piying kwa mara ya kwanza, na niliiona kuwa na mtindo tofauti na ule wa ngoma nyingine. Pia nimevutiwa na wanawake wazee wanaocheza ngoma hiyo. Bila kujali umri wao mkubwa, wanaweza kucheza vizuri ngoma kweli. Wao ni hodari."

Miongoni mwa wachezaji 12 wa kundi la "machweo mazuri", Bibi Gao Lan mwenye umri wa miaka 74 ni mkubwa zaidi kuliko wengine, yeye pia ni kiongozi wa kundi hilo. Akikumbusha kwa nini alijiunga na kundi la ngoma baada ya kustaafu, alisema "Lengo moja ni kufanya mazoezi ya kujenga mwili, na lingine ni kuondokana na upweke."

Baada ya kustaafu, Bibi Gao Lan alikuwa akipitia kipindi fulani cha upweke. Baadaye kilianzishwa chuo kikuu cha wazee mjini Tangshan, Bibi Gao Lan alijiandikisha kwenye mafunzo ya dansi katika chuo kikuu hicho. Mzee huyo alikuwa na mpango wake wa kuwafundisha dansi aliyojifunza wanawake wenzake waliofanya mazoezi ya kujenga mwili kwa pamoja. Alisema "Kila siku nilishiriki kwenye mafunzo ya dansi, halafu niliwafundisha wenzangu ambao tulifanya mazoezi ya kujenga mwili kwa pamoja wakati wa asubuhi. Nilifurahi sana kuwa nao na pia nilipenda kuwafundisha, kwa vile nilikuwa napenda dansi tangu utotoni mwangu."

Siku nenda siku rudi, watu waliomfuata mzee Gao Lan kujifunza dansi waliongezeka. Miaka 10 iliyopita, Bibi Gao Lan na wanawake wenzake walianzisha kundi la ngoma la "machweo mazuri". Katika mwaka wa kwanza baada ya kuanzishwa kwa kundi hilo, walipewa tuzo katika mashindano ya kitaifa ya ngoma ya wazee. Tuzo hiyo ya kitaifa iliwasisimua na kuwatia moyo sana. Na kuanzia hapo walikuwa na hamu ya kufanya maonesho rasmi jukwaani.

Nafasi ilikuja mwaka 1997 ambapo mji wa Tangshan ulitaka kuunda kundi la sanaa la wazee. Wazee wa kundi la "machweo mazuri" walijiandikisha mara moja. Lakini walishindwa kuchaguliwa kutokana na kukosa mafunzo ya kitaaluma.

Kutokana na tukio hilo, wazee hao walitambua upungufu wao kuwa wanapaswa kufundishwa na walimu wenye taaluma na ni lazima wawe na ngoma maalumu. Mchezaji mmoja wa kundi la "machweo mazuri" alikuwa akifundishwa ngoma ya Piying na mwalimu Fan Jincai, kwa hiyo wazee hao walikwenda kwa mwalimu huyo kumwomba awafundishe. Lakini mwalimu Fan alikuwa hapendi kukubali ombi hilo mwanzoni.

Bw. Fan Jincai alisema, "Wanawake hao wazee walipokuja, nilikuwa nimebuni na kucheza ngome ya Piying kwa miaka 11. Niliwaanglia na kutambua kuwa, wao walikuwa si wasanii wa dansi waliopokea mafunzo ya kitaaluma, nilidhani ningewafundisha hakika wangevuruga kazi yangu. Lakini walikuwa wakinifuata wakati wote na kunioneshea nia imara ya kujifunza kutoka kwangu, popote nilipokwenda walinifuata. Nikaguswa sana na moyo wao."

Hatimaye mwalimu Fan alikubali kuwafundisha wanafunzi hao, ambao walikuwa na umri mkubwa zaidi kuliko yeye. Katika mazoezi yaliyofuata, mwalimu Fan alishuhudia na kuguswa na moyo wa kuchapa kazi wa wazee hao. Ingawa mwalimu alipunguza ugumu wa ngoma hiyo kwa kulingana na hali halisi ya wazee hao, hata hivyo mazoezi yalikuwa ni magumu sana kwa wanafunzi hao wazee. Miongoni mwao, Bibi Gao Lan mwenye umri mkubwa zaidi kuliko wengine alikuwa anakabiliwa na shida kubwa zaidi, kwa hiyo alifanya bidii zaidi. Alisema,

"Siku nyingine nilifanya mazoezi huku nikipika chakula. Nyumbani nilikuwa narudiarudia vitendo vya ngoma mara kwa mara, hata nilitembea huku nikicheza vitendo vya ngoma."

Mwandishi wetu wa habari alitambua kuwa, wazee hao walipocheza ngoma, sura zao zilikuwa zinaonesha furaha kubwa na kuwavutia sana watu. Bibi Gao Lan alieleza, "Nacheza ngoma kwa moyo, na kuonesha hali ya maisha yangu. Nilipocheza ngoma, niliwaza moyoni mwangu kuwa, angalieni maisha yangu yenye furaha."

Idhaa ya kiswahili 2006-04-27