Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-28 20:51:33    
Rais Hu Jintao wa China alihutubia Bunge la Nigeria

cri

Rais Hu Jintao wa China tarehe 27 alilihutubia bunge la Nigeria, ambapo alifafanua kikamilifu sera na mapendekezo ya China kuhusu kuendeleza uhusiano kati ya China na Afrika.

Mwaka huu China na nchi za Afrika zitaadhimisha miaka 50 tangu pande hizo mbili kuanzisha uhusiano wa kibalozi. Katika ziara ya kwanza ya rais Hu Jintao kwa mwaka huu, amezitembelea nchi tatu za kiafrika, ambazo ni Morocco, Nigeria na Kenya, nchi hizo zipo kaskazini, magharibi na mashariki mwa bara la Afrika. Hii ni ishara kuwa, China inatilia maanani kuendeleza uhusiano na Afrika.

Katika hotuba ya rais Hu Jintao kwenye bunge la Nigeria, aliweka bayana madhumuni ya ziara yake hiyo. Alisema, "Safari hii nimekuja barani Afrika kwa lengo la kuzidi kuielewa Afrika, kuihisi Afrika na kujifunza kutoka kwa bara hilo. Ningependa kurithi urafiki wa jadi kati ya China na Afrika, kuongeza uaminifu, ushirikiano wa kunufaishana, kusukuma mbele maendeleo ya pamoja, na kushirikiana pamoja na nchi za Afrika katika kujenga uhusiano mpya wa kiwenzi na kimkakati."

Rais Hu Jintao aliyakumbusha maendeleo yaliyopatikana katika uhusiano wa China na Afrika katika miaka 50 iliyopita. Tangu mwaka 1955 ulipofanyika mkutano wa Bandung, viongozi wa China mpya na nchi za Afrika walishikana mikono kwa mara ya kwanza, mpaka mwaka 2005 katika maadhimisho ya miaka 50 ya mkutano wa Bandung, ambapo China na nchi za Afrika zilikubaliana kujenga uhusiano mpya wa kiwenzi na kimkakati. Alisema katika muda wa nusu karne iliyopita, China na nchi za Afrika siku zote zimekuwa zikiaminiana, kuelewana na kuungana mkono.

Rais Hu Jintao alisema "Historia imeshuhudia minara mmoja baada ya mingine wa urafiki wa China na Afrika. Sisi kamwe hatutasahau maendeleo yaliyopatikana katika uhusiano na Afrika miaka 50 iliyopita."

Rais Hu Jintao alisisitiza kuwa, kutokana na hali ilivyo sasa duniani, nchi mbalimbali zinazidi kutegemeana, na maslahi yao yanahusiana kwa karibu, ambapo watu wa nchi mbalimbali wanatumaini kushirikiana na kusaidiana, ndiyo maana wanaweza kunufaika kwa pamoja na fursa za maendeleo, kukabiliana kwa pamoja na changamoto na kupata maendeleo kwa pamoja.

Kwa ajili ya kurithi urafiki wa jadi kati ya China na Afrika na kuendeleza uhusiano mpya wa kiwenzi na kimkakati, rais Hu Jintao wa China alitoa mapendekezo manne, akisema "Tuongeze uaminifu kisiasa, tupanue ushirikiano wa kunufaishana kiuchumi, kutilia maanani kufundishana kiutamaduni na kuimarisha ushirikiano katika mambo ya usalama."

Akifafanua mapendekezo hayo manne, rais Hu Jintao alisisitiza kuwa, China itaendelea kutoa misaada kwa nchi za Afrika, misaada inayolingana na uwezo wa China, na China inashikilia sera hiyo bila kutikisika.

Rais Hu Jintao pia alieleza hali ya uchumi wa China na malengo ya maendeleo. Alisema China bado ni nchi inayoendelea, na katika muda mrefu China iko katika kipindi cha mwanzo cha ujamaa. Katika mchakato wa kulijenga taifa, wananchi wa China siku zote wanashikilia kanuni za amani, maendeleo na ushirikiano. Alisema China inatekeleza sera ya kidiplomasia ya amani iliyo ya kujitawala na kujiamulia mambo, China inafuata njia ya kujiendeleza kwa amani, na kushikilia mkakati wa kufungua mlango kwa kunufaishana. Watu wa China wakishirikiana na watu wa nchi nyingine duniani, watajenga dunia yenye amani ya kudumu, ustawi wa pamoja na masikilizano.

Rais Hu Jintao wa China alisema "Ukweli wa mambo umeonesha na utaendelea kuonesha kuwa, maendeleo ya China ni maendeleo ya amani, kufungua mlango na ya ushirikiano. Maendeleo ya China hayatatishia mtu yeyote bali yatailetea dunia nafasi na fursa nyingi za maendeleo."

Wabunge wa Nigeria waliosikiliza hotuba ya rais Hu Jintao walieleza maoni yao, wakisema "Tumeanza kutambua kuwa China na Nigeria zinasimama kwenye mstari mmoja. Tunafurahia mapendekezo ya rais hu Jintao, na tunatarajia maendeleo zaidi ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili."

"Hotuba ya rais Hu imeonesha kuwa, China inaisaidia Nigeria kukuza sekta mbalimbali, hotuba hiyo pia ni ishara ya uhusiano imara kati ya nchi hizo mbili."