Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-28 21:05:04    
Ziara ya kiserikali ya Rais Hu Jintao wa China nchini Kenya

cri

Rais Hu Jintao wa China amewasili Nairobi tarehe 27 kwa ziara ya kiserikali nchini Kenya. Kuhusu ziara hiyo ya rais Hu Jintao, balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli alipohojiwa na waandishi wetu wa habari alisema, urafiki kati ya China na Kenya ulianzia tangu enzi na dahari. Mwaka 1405 baharia maarufu wa China Bwana Zheng He aliongoza kikosi cha merikebu kusafiri baharini, ambapo walifika pwani ya bahari ya Afrika ya mashariki na kati, kutembelea miji yenye bandari ya Mombasa na Malindi. Tarehe 13 Desemba mwaka 1963, siku mbili tu tangu Kenya ipate uhuru wake, ilianzisha uhusiano wa kibalozi na China, tokea hapo, uhusiano kati ya China na Kenya umeendelea siku hadi siku. Hivi sasa maendeleo ya uhusiano huo yako kwenye kiwango kizuri zaidi katika historia. Balozi Guo alisema:

katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa China na Kenya wametembeleana mara kwa mara na kupata mafanikio dhahiri.

Balozi Guo alisema, katika miaka 50 iliyopita, mabadiliko mengi yalitokea duniani, nchini China na barani Afrika, lakini msingi wa ushirikiano kati ya China na Afrika haubadiliki, pande hizo mbili zina matumaini makubwa ya kuenzi zaidi urafiki wa jadi kati ya China na Afrika katika hali ya historia mpya, ili kupata maendeleo ya pamoja. Aidha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Kenya umendelea kwa haraka. Balozi Guo alisema:

Mwaka 2005, thamani ya biashara kati ya China na Kenya ilifikia dola za kimarekani milioni 475, hili ni ongezeko la zaidi ya mara mbili kuliko mwaka 2003. Na maingiliano kati ya China na Kenya kwenye sekta za utamaduni na elimu pia yanaongezeka siku hadi siku.

Na balozi wa Kenya nchini China Bibi Ruth Solotei alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari kuhusu ziara ya rais Hu Jintao wa China nchini Kenya alisema:

" Safari ya rais Hu Jintao nchini Kenya inaonesha kuwa nchi zetu mbili zina uhusiano mzuri wenye umuhimu mkubwa. Tunaona ziara hiyo itasaidia sana uhusiano kati ya Kenya na China. Mwaka jana Kenya na China zilianzisha kwa pamoja Chuo cha Confucius katika Chuo kikuu cha Nairobi Kenya, Radio China kimataifa CRI sasa inatangaza Kenya kupitia masafa ya FM, tuna wanafunzi wanaosoma na kujifunza mchezo wa sarakasi kila mwaka nchini China, mwaka jana China ilisema itaongeza udhamini wa masomo kwa nchi za Afrika, tunatarajia wanafunzi wa Kenya watapata nafasi ya kusoma katika vyuo vikuu nchini China

Tunatarajia kuwa katika ziara hiyo ya rais Hu Jintao, Kenya na China zitasaini mikataba mbalimbali katika sekta mbalimbali za uchumi, elimu, utamaduni na nyingine zinazoweza kuwanufaisha wnanachi wa Kenya. Pia tunatarajia kuwa, viongozi wetu wa Kenya na China watazungumza mambo mengi kuhusu nchi zote mbili kama mambo ya Umoja wa Mataifa na mambo ya usalama duniani. Ziara hiyo italeta mwelekeo mpya kwa kuimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Kenya

Kutokana na maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Kenya , makampuni mengi ya China yameanzisha na yanataka kwenda kuanzisha shughuli zao nchini Kenya, Balozi Solotei alipozungumzia hilo alisema

Wawekezaji wa China wasiwe na wasiwasi, wakienda Kenya watakuwa katika hali ya usalama. Nchini Kenya kuna soko kubwa, makampuni ya China yanaweza kuuza bidhaa nchini Kenya. Aidha, kwa kuwa Kenya imejiunga na mkataba wa Agoa, kampuni za China pia zinaweza kutengeneza nguo nchini Kenya na kuuza nchini Marekani kwa njia ya Agoa. Kampuni za China zinakaribishwa kuwekeza nchini Kenya katika sekta za teknolojia, ujenzi wa nyumba, barabara, na kadhalika.

Makampuni mengi ya China yanataka kuwekeza nchini Kenya. Kenya itachukua hatua kuyawezesha makampuni hayo ya China kuanzisha biashara nchini Kenya ili kuleta manufaa kwa nchi zote mbili.