Baada ya mkurugenzi mkuu wa shirika la nishati ya atomiki duniani IAEA Bwana Mohamed El Baradei kuwasilisha ripoti kuhusu suala la nyuklia la Iran kwenye baraza la IAEA na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, misimamo ya Marekani na Iran inafuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Bwana Hamid Reza Asef tarehe 30 Aprili alionya kuwa, kama baraza la usalama litachukua hatua kali dhidi ya Iran, Iran itachukua hatua zinazolingana. Siku hiyo, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice alionya kuwa, Marekani huenda itachukua hatua ya kuiwekea Iran vikwazo nje ya utaratibu wa baraza la usalama. Marekani na Iran zimeanzisha mvutano mpya kuhusu suala la nyuklia la Iran.
Ripoti iliyotolewa na mkurugenzi mkuu wa IAEA Bw. Baradei inasema, Iran haikufuata agizo la baraza la usalama la kuitaka iache shughuli za kusafisha uranium katika siku 30. Chini ya shinikizo la jumuiya ya kimataifa, serikali ya Iran ilieleza kuwa, itatoa ratiba yake katika wiki tatu zijazo, na kujibu hatua kwa hatua mashaka yaliyotolewa na IAEA, wakati huo huo itawaruhusu wakaguzi wa IAEA wakague zana za nyuklia za Iran, lakini baraza la usalama linapaswa kurejesha suala la nyuklia la Iran litatuliwe kwenye shirika la nishati ya atomiki duniani. Lakini sharti hilo la Iran linakataliwa kabisa na Marekani. Msemaji wa Ikulu ya Marekani tarehe 29 Aprili alitoa taarifa akisema, serikali ya Iran inapawa kuacha nia yake ya kumiliki silaha za nyuklia, ama sivyo Marekani itashikilia kuwasilisha suala hilo kwenye baraza la usalama. Wakati huo huo, Marekani na Uingereza ziko mbioni kutunga azimio la kuiwekea Iran vikwazo.
Jumuiya ya kimataifa imeona kuwa, mjumbe mkuu wa mazungumzo ya nyuklia wa Iran, ambaye pia ni katibu wa kamati kuu ya usalama ya Iran Bwana Ali Larijani tarehe 30 Aprili alisema, Iran itaendelea na utafiti na kufanya shughuli za kusafisha uranium, kama nchi husika za magharibi zikitaka kuitilia Iran shinikizo, Iran itabadilisha uamuzi wake wa kufanya ushirikiano na IAEA.
Wachambuzi wameona kuwa, hatua kali zitakazochukuliwa na baraza la usalama ni vikwazo dhidi ya Iran vitakavyohimizwa na nchi za magharibi ikiwemo Marekani, lakini Bw. Asef hakutaja Iran itachukua hatua gani ya kuitikia. Watu wanakumbuka kuwa, kiongozi mkuu wa Iran Bwan Hameneyi aliwahi kusema kuwa, kama Marekani itathubutu kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, basi maslahi yote ya Marekani katika sehemu mbalimbali duniani yatakuwa katika lengo la kulipizwa kisasi.
Bi. Rice wa Marekani tarehe 30 April aliilaani Iran kwa kucheza mchezo na jumuia ya kimataifa katika suala la nyuklia. Akidai kuwa, kabla ya hapo, Iran ilikuwa na muda wa kutosha wa kutekeleza mpango wa kuacha shughuli za kusafisha uranium kutokana na agizo la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Alisema, Marekani bado inaweza kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia mbalimbali za kidiplomasia kwa kupitia baraza la usalama, na baraza la usalama likichelewa kuchukua hatua husika, maofisa waandamizi wa Marekani bado hawajaacha uwezekano wa kushambulia kijeshi Iran.
Lakini wataalamu wameona kuwa, hivi sasa Marekani bado haina uwezo wa kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran wakati inapokabiliana kwa nguvu zote na shughuli za Iraq. Serikali ya Bush ikitaka kuanzisha vita nyingine, haitaungwa mkono na wananchi wake. Kwa hivyo rais Bush na maofisa waandamizi wa nchi hiyo wanataka kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia.
Habari zinasema kuwa, baraza la usalama litafanya mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran tarehe 3 Mei, na mawaziri wa mambo ya nje wa China, Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani watafanya mkutano tarehe 9 Mei huko New York, ili kujadiliana kuhusu ripoti iliyokabidhiwa na Bw. Baradei na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Iran.
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-01
|