Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-02 20:15:43    
Kiongozi wa ujenzi wa vijiji vipya Bw. Wu Renbao

cri

Ili kupunguza tofauti kati ya miji na vijiji, na kuongeza pato la wakulima, serikali ya China inahimiza ujenzi wa vijiji vipya, kuziunga mkono sehemu za vijijini kuboresha miundo-mbinu na kuinua kiwango cha uzalishaji mazao ya kilimo, ambapo waliibuka viongozi wengi waliowaongoza wakulima ili waweze kuondokana na umaskini. Katika kipindi hiki cha leo tutawafahamisha mkuu wa kijiji Bw. Wu Renbao, ambaye kijiji anachoongoza kiko mbele katika harakati za kujenga vijiji vipya nchini China.

Bw. Wu Renbao aliwahi kuwa katibu wa chama wa tawi la kijiji cha Huaxi, mkoa wa Jiangsu, sehemu ya mashariki ya China, kubadilisha sura ya kijiji cha Huaxi na kuwasaidia wakulima kuishi maisha mazuri ni lengo lake. Katika miaka 48 alipokuwa katibu wa chama, kijiji cha Huaxi kilibadilika kuwa kijiji tajiri, pato la kijiji limezidi Renminbi bilioni 30 kwa mwaka na kuwa na kampuni 8 ambazo hisa zake zinauzwa kwenye soko la hisa.

Mtu akiingia kijijini Huaxi, anaona kama ameingia kwenye maonesho ya nyumba za hali ya juu, hivi sasa eneo analoishi mwanakijiji hata lile dogo kabisa linafikia mita za mraba 400, wakati baadhi yao wenye nyumba kubwa, eneo linaweza kufikia mita za mraba 600. Kitu kinachofanya watu kupendezwa zaidi ni kuwa kila familia ya wakulima ina motokaa. Wanakijiji walimwanbia mwandishi wetu wa habari kuwa watu matajiri ni wengi katika kijiji cha Huaxi, tena wako watu wenye Yuan milioni zaidi ya 10. Bibi Wu Guiqing ana nyumba nzuri yenye gorofa mbili, bwawa la kuogelea na egesho la magari, yeye alisimama mbele ya nyumba yake na kusema kwa furaha,

"Familia yetu ina watu wanne, watoto wawili mimi na mume wangu. Fedha ya kununua nyumba hii nimeshalipa kabisa, bado nina Yuan milioni kadhaa ambazo zimehifadhiwa benki. Tumenunua magari matatu."

Baada ya kusikiliza maelezo ya dada Wu, mwandishi wetu wa habari alikuwa na shauku kubwa ya kuona nyumba ya Bw. Wu Renbao, akiwa mkuu wa kijiji, nyumba yake ingekuwa nzuri na kubwa zaidi. Lakini ni kinyume na alivyotarajia kwani watu wa familia ya Bw. Wu Renbao wanakaa katika nyumba moja ya zamani. Wanakijiji walisema, toka miaka ya 70 ya karne iliyopita hadi hivi sasa kijiji cha Huaxi kilijenga nyumba za awamu tano. Wanakijiji wengi wamehamia nyumba mpya mara nne, makazi yao yamekuwa bora zaidi na zaidi, lakini Bw. Wu Renbao hakutilia maanani kuboresha makazi ya familia yake. Mwandishi wetu wa habari alifika nyumbani kwa Bw. Wu Renbao, aliona samani zake ni za bei rahisi sana, lakini picha zilizobandikwa ukutani kuhusu mbadiliko ya kijiji chao katika miaka miongo kadhaa iliyopita, zilikuwa nyingi.

Alipokuwa na mazungumzo na Bw. Wu Renpan, mwandishi wetu wa habari hakuamini huyo ni mzee mwenye umri wa miaka karibu 80, macho yake maangavu na maongezi yake yenye matiki safi, vinafanya watu kuona kuwa ana imani kubwa juu ya maendeleo ya kijiji cha Huaxi katika siku za baadaye. Alipoeleza siri ya maendeleo ya kijiji cha Huaxi, Bw. Wu Renbao alisema, kuwasaidia wanakijiji kunufaika kutokana na maendeleo ya uchumi ni msingi wa kuleta maendeleo ya muda mrefu.

"Yakitokea manufaa, waache wananchi wafaidike kwanza, ikitokea shida, maofisa wapige moyo konde na kuzikabili kwanza, Kufanya hivyo ndipo umma utakapoweza kuhamasishwa."

Katika maisha yake, Bw. Wu Renbao anajiweka kiwango cha chini, lakini mbele ya kazi anafuata kiwango cha juu. Wanakijiji walisema, katika muda wa miaka 48 iliyopita hakufanya makosa makubwa katika kutekeleza sera za serikali, bali aliweza kufanya uamuzi sahihi kutokana na yeye kuelewa kwa usahihi sera za serikali. Mwezi Agosti mwaka 2003, Bw. Wu Renbao aliitisha mkutano wa dharura wa viongozi wa kijiji cha Huaxi, aliweka kanuni tatu za kusimamisha kwa haraka ujenzi wa miradi mipya, viwanda vilivyoko hivi sasa vinatakiwa kuendesha kwa makini shughuli zake, na kuharakisha ujenzi wa miradi ambayo imekwisha anzishwa. Kwa kufuata kanuni hizo, kiwanda cha chuma cha pua cha Huaxi hakitapanuliwa tena kwa kufuata mpango uliowekwa, kiwanda cha nyuzi za madini cha kijiji hicho pia kilitakiwa kufungwa, hatua hiyo ilisababisha malalamiko mengi, watu wengi hawakuelewa hatua iliyochukuliwa na Bw. Wu Renbao. Naibu katibu wa chama wa kamati ya kijiji cha Huaxi Bw. Yang Yongchang alipoeleza hali ya wakati ule alisema,

"Kwa nini watu hawakumwelewa? Kwa sababu hali ya uchumi wa kijiji cha Huaxi ilikuwa nzuri sana, mwaka ule tulisema, tutatimiza lengo la kuwa na pato la Renminbi bilioni 10 kutokana na mauzo katika mwaka 2003. Kwa nini katibu wa zamani alitaka kusimamisha kwa haraka shughuli za kiwanda?

Kuhusu wasiwasi wa watu wengi, Bw. Wu Renbao alitoa maelezo kwa moyo wa uvumilivu. Alisema, wakati ule serikali ya China ilishatangaza kufanya udhibiti kwa kutumia mpango mkuu wa taifa, kuzuia kasi ya ongezeko la uwekezaji wa mali zisizohamishika lililoongezeka kwa haraka kupita kiasi na kupunguza hatari zilizotokea katika ukuzaji wa uchumi. Kutokana na sera za serikali, Bw. Wu alifanya uamuzi huo baada ya kukadiria kiwanda cha kijiji. Mambo yalikwenda kama alivyotarajia Bw. Wu, kabla ya kutimia muda wa mwaka mmoja, serikali ilitoa kwa mfululizo sera za aina mbalimbali, lakini uchumi wa kijiji cha Huaxi licha ya kutoathiriwa, ulipata maendeleo makubwa ya kudumu kutokana na kanuni tatu alizotoa Bw. Wu Renbao.

Bw. Wu Renbao alipotathimini chanzo cha kuweza kutangulia vijiji vingine, alisema, ni kutokana na yeye kufuatilia habari za aina mbalimbali katika miaka mingi iliyopita. Bw. Wu hataki watu wengine kuingilia shughuli zake za kila siku. Mnamo saa 12 na nusu asubuhi anasikiliza habari za Radio ya umma ya serikali kuu na kusoma gazeti la "Renminribao"; mnamo saa 1 usiku, hakosi kuketi kuangalia kipindi cha habari cha Televisheni ya serikali kuu, alifanya vivyo hivyo kwa miaka miongo kadhaa. Aidha, Bw. Wu anapenda kuwatembelea wanakijiji wa kijiji chao, mara kwa mara alijitokeza kijijini, kiwandani au nyumbani kwa mwanakijiji bila kutoa taarifa kabla. Bw. Wu Xieen alichaguliwa kuwa mkuu wa kijiji baada ya Bw. Wu Renbao kustaafu, alisema, Bw. Wu Renbao ana uwezo mkubwa wa kufanya uchambuzi juu ya mambo.