Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-02 21:38:57    
Barua 0430

cri

Jenifa Mnyambwa wa S.L.P 1005, Morogoro, Tanzania ametuletea barua akisema, kwa mara ya kwanza anajitokeza katika kipindi cha sanduku la barua, CRI, kwa madhumuni ya kuomba uanachama wa kudumu. Ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuvutiwa mno na vipindi vyetu vyenye maadili bora na vyenye manufaa kwa wasikilizaji, kama vile vipindi vya daraja la urafiki kati ya China na Afrika, kuwa nami jifunze Kichina n.k. Hivyo anaahidi kudumisha ushirikiano nasi. Anatoa shukrani kwa msikilizaji wa muda mrefu wa Redio China Kimataifa Bw. Onesmo H. Mponda kwa kumpa maelekezo juu ya kujiunga na matangazo yetu, pamoja na taratibu nyingine za kuwasiliana na Redio China Kimataifa. Mwishoni alitoa pongezi kwa CRI, na kwa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili.

Tunamkaribisha kwa mikono miwili kuwa mwanachama wetu wa kudumu, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza vizuri vipindi vyetu na kutuletea maoni na mapendekezo yake.

Mussa A. Mstaphar wa S.L.P 280, Tarime - Mara, Tanzania katika barua yake kwanza alitoa salamu za dhati kwa idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa. Anaamini kuwa Idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa itaendelea vema na shughuli za kila siku na masaa yote katika kuwajulisha wasikilizaji habari za matukio mbalimbali yanayotokea katika mataifa na ulimwengu kwa ujumla. Alisema hali yake siyo nzuri kwa sasa, kwa sababu karibu mwezi mmoja sasa hakusikiliza matangazo yetu, kutokana na redio yake aliyokuwa akisikilizia iliibiwa, na sasa hana redio ya kusikiliza. Na kufuatia hali ngumu ya maisha itamchukua muda mrefu kidogo kurudi hewani na kuwa pamoja na Idhaa ya Kiswahili. Pamoja na yote hayo atajaribu kupata habari kutoka kwa rafiki yake wa Klabu ya Kemogemba Bw. Ras Ngogo. Alisema labda kama Bw. Ngogo atajitokeza mfadhili wa kuweza kumfadhili japo kiredio kidogo toka China atafurahi sana. Na atamwombea dua na kumtakia kila la kheri na mafanikio mema daima.

Mwishoni anawatakia wafanyakazi wa Redio China Kimataifa kila la kheri na mafanikio mema na idumu Redio China Kimataifa.

Tunamshukuru msikilizaji wetu huyo Mussa Mstaphar kwa barua yake na pia tunasikitishwa na hali yake na kuibiwa radio, kweli shida yake si kubwa lakini pia si ndogo, kwani imemfanya hawezi kusikiliza vipindi vyetu. Jambo hili limetukumbusha kuwa tunasikitishwa siku zote na hali ya mwaka jana, kwamba Bwana Ngogo alipata nafasi ya kwanza katika shindano la chemsha bongo, angepata zawadi ya redio, lakini kutokana na kosa letu, mpaka sasa hajapata zawadi hiyo. Tunasubiri kupata fursa ya kumzawadia, hapa tunamwomba Bwana Ngogo atuelewe, asiwe na wasiwasi, tutajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo.

Abubakari S. Omary wa P.O.Box 1345, Musoma, Mara, Tanzania ni kijiana mwenye umri wa miaka 18, alituandikia barua akisema anavutiwa sana na vipindi vya salamu, jifunze lugha ya Kichina. Anapenda sana kujifunza utamaduni wa China na mengineyo. Alisema huko Mosoma wasikilizaji wanapata matangazo ya Redio China Kimataifa vizuri kabisa. Mambo wanayojifunza kupitia Idhaa ya Kiswahili ni mengi sana, na anaomba tuzidishe juhudi.

ISSA. S. O. Mnosse wa P.O.Box 770, Kahama, Shinyanga, Tanzania anatuandikia barua akisema, yeye ni kijana wa Tanzania wenye umri wa miaka 16. Amevutiwa sana na vipindi vya Idhaa ya Kiswahili, na hasa kipindi cha jifunze Kichina na kipindi cha salamu. Alisema kweli wafanyakazi wa Redio China Kimataifa wamefanya mambo makubwa na mazuri. Lakini huko Kahama wasikilizaji wanaipata matangazo yetu kwa shida. Hivyo alituma ombi lake kwa Redio China Kimataifa, na alisema atafurahi sana endapo atajibiwa na ombi lake litakubaliwa.

Kuhusu suala hilo kweli wasikilizaji wetu wengi wa Tanzania wametuletea barua wakilalamika kuhusu usikivu mbaya wa matangazo yetu katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania, sisi tumetoa ripoti kwa ofisi husika, walisema kuwa watajitahidi kutatua tatizo hilo.