Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-03 21:22:21    
Chuo kikuu cha Fudan chajaribu kupata wanafunzi wapya kwa njia ya usahili

cri

Hivi karibuni wahitimu 300 wa sekondari ya juu wa mji wa Shanghai wamesajiliwa na chuo kikuu cha Fudan cha Shanghai kwa njia ya usahili bila kushiriki kwenye mtihani wa kitaifa wa China wa kujiunga na vyuo vikuu. hii ni mara ya kwanza kufanya usahili huo katika historia ya elimu ya China.

Msichana Zhang Moran ni mwanafunzi mhitimu wa shule moja ya sekondari ya juu ya Shanghai. Hivi karibuni alishiriki kwenye usahili wa kujiunga na chuo kikuu cha Fudan alikuwa mmoja miongoni mwa wanafunzi zaidi ya elfu moja waliosahiliwa na hatimaye Bi Zhang alifaulu usahili huo na kujiunga na chuo hicho maarufu. Bi. Zhang Moran alisema, tofauti na mtihani wa maandishi, usahili unaweza kuonesha kikamilifu zaidi uwezo wa jumla wa wanafunzi.

"naona mwanfunzi akipata nafasi ya kwanza katika mtihani wa maandishi, haimaanishi kuwa ana uwezo mkubwa zaidi wa jumla. Hivyo usahili ni wa lazima kwa kuwa unaweza kuonesha uwezo wa kuwasiliana na watu wengine."

Miezi miwili iliyopita, chuo kikuu cha Fudan kilitoa taarifa kuhusu usajili wa wanafunzi wapya kwa njia ya usahili. Kutokana na kuwa chuo kikuu hicho ni maarufu sana nchini China, basi mara baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo, wanafunzi zaidi ya 6000 walijiandikisha kushiriki kwenye usahili huo. Kabla ya usahili huo, chuo kikuu cha Fudan kiliandaa mtihani mmoja rahisi, ukiwa na masomo ya lugha ya Kichina, hisabati, lugha ya Kiingereza na kompyuta, na kupata orodha ya wanafunzi wapatao elfu moja watakaoshiriki kwenye usahili huo kutokana na matokeo ya mtihani huo.

Chuo kikuu cha Fudan pia kilishirikisha maprofesa zaidi ya mia moja na tume ya wataalamu ya usahili. Maprofesa hao wote wanafanya kazi katika chuo kikuu cha Fudan na wote ni wataalamu katika taaluma zao zikiwemo sanyasi ya kijamii, teknolojia na sayansi na elimu ya maadili. Wakati wa kufanya usahili, wanafunzi walichagua maprofesa watano kwa bahati nasibu na kufanyiwa usahili wa dakika 15 na kila profesa, na mweshowe maprofesa hao walichagua wanafunzi 300 waliopata matokeo mazuri katika usahili na kujiunga na chuo kikuu hicho.

Mwanafunzi mmoja aliyeshiriki kwenye usahili huo alidokeza kuwa, maswali ya maprofesa ni pamoja na "tafadhali toa mfano kuthibitisha wewe ni mtu mwenye kubeba wajibu." "kama wewe ni meya wa jiji la Shanghai, ni kwa vipi utatatua suala la msongamano wa magari barabarani jijini humo?" na "ukipewa fedha za kutosha kuandaa shughuli moja kubwa, utafanyaje?"

Naibu mkuu wa chuo kikuu cha Fudan Bw. Cai Dafeng alisema, akiwa msimamizi wa chuo kikuu, si kama tu anataka kujua kiwango cha ujuzi na uwezo wa kitaaluma wa wanafunzi, bali pia anataka kujua wao ni watu wa namna gani, wana uzoefu na mitizamo gani ya maisha, ambayo haiwezekani kujulikana kwa njia ya mtihani wa zamani wa maandishi, hivyo chuo kikuu cha Fudan kiliandaa usahili huo ili kuchunguza kikamilifu uwezo wa jumla wa wanafunzi. Bw. Cai Dafeng alisema:

"tunataka kutimiza malengo kadhaa kwa njia ya usahili, kwanza tunataka kufahamu fikra za wanafunzi, hasa mitizamo yao ya kijamii na ufahamu wao kuhusu wajibu wa kijamii; pili, tunataka kufahamu uwezo wao wa kufanya utafiti, pia tunazingatia uzoefu wao katika shughuli za kijamii."

Nchini China wanafunzi wanatakiwa kufanya mtihani wa taifa Ili kujiunga na vyuo vikuu. Mtihani huo unalenga kupima uwezo wa wanafunzi hao. Hivyo ili kupata matokea mazuri katika mtihani huo, wanafunzi wengi wanatilia maanani tu matokeo ya masomo na kupuuza maendeleo ya jumla, hali hiyo imesababisha kutokea kwa wanafunzi wenye uwezo dhaifu wa jumla wanaoweza tu kupata matokeo mazuri katika mitihani.

Naibu mkuu wa chuo kikuu cha Fudan Bw. Cai Dafeng alisema, utaratibu huo wa mtihani ingawa unaweza kuongeza ustadi wa wanafunzi wa China kufanya mitihani lakini unawapunguzia uwezo wa kujifunza kwa kujitegemea na kutumia ujuzi katika mazoezi, na pia umesababisha upungufu wa kimantiki, kushuka kwa kiwango cha maadili na kupungua kwa uwezo wa kukabiliana na jamii. Hivyo chuo kikuu cha Fudan kinataka kuelekeza wanafunzi wa shule za sekondari na hata shule za msingi wabadilishe mitizamo yao ya kujifunza kupitia majaribio hayo ya kufanya usahili katika usajili wa wanafunzi wapya, ili kuwawezesha wanafunzi watilie maanani kuinua uwezo wa uvumbuzi na wa kufanya mazoezi.

 

Mwanafunzi mhitimu wa shule ya sekondari Wang Tianyu alishiriki kwenye usahili huo. Ingawa alishindwa kujiunga na chuo hicho, lakini aliona kuwa usahili huo umefanya awe na maoni mapya kuhusu mtihani wa taifa na mbinu zake za kujifunza. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, haisaidii hata kidogo kufanya maandalizi ya muda mfupi kwa ajili ya usahili kama huo, majibu ya maswali yaliyoulizwa na maprofesa hata hayapatikani katika vitabu vya kiada, bali yanalenga kupima uwezo na mtizamo wa kujifunza wa wanafunzi.

"naona maandalizi muhimu katika kufanya usahili lazima yaanze kufanywa kuanzia mwaka wa kwanza na wa pili katika shule za sekondari, wala si wiki moja tu kabla ya usahili. Wanafunzi wakitaka kupita usahili, mbali na kuzingitia masomo shuleni, pia wanapaswa kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii ili kuinua uwezo wa jumla kutokana na uzoefu wa shughuli hizo."

Njia hiyo mpya ya kusajili wanafunzi wapya imekubaliwa na wanaelimu, vyombo vya habari na wazazi wengi wa wanafunzi. Wanaona kuwa, hiyo imefanya usajili wa wanfunzi wa vyuo vikuu uwe na njia mbalimbali, pia inasaidia kuelekeza shule za sekondari na za kimsingi ziimarishe elimu ya kuinua uwezo wa jumla.

Lakini baadhi ya watu wanaona kuwa, itapoteza usawa kama njia hiyo ikitumika kwa wanafunzi wa vijijini ambao wanaishi katika mazingira mabaya na wanakabiliwa na tatizo la kiuchumi. Kuhusu hali hiyo, Bw. Cai Dafeng alisema, usajili huo wa wanafunzi kwa njia ya usahili ni jaribio moja la mageuzi ya mtihani ya taifa ya kujiunga na vyuo vikuu. Imefahamika kuwa, njia hiyo mpya inatekelezwa kwa wanafunzi mjini Shanghai tu, na idadi ya wanafunzi waliosajiliwa kwa usahili inachukua asilimia 10 tu katika wanafunzi wote wapya wa chuo kikuu hicho wa mwaka jana.