Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-03 20:09:25    
Suala la nyuklia la Iran bado liko kwenye njia ya utatuzi wa kidiplomasia

cri

Mkutano wa Paris uliohudhuriwa na wajumbe wa nchi sita za China, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Russia na Ujerumani ulimalizika tarehe 2 usiku, ambao haukuweza kufikia makubaliano kuhusu suala la nyuklia la Iran. Mawaziri wa nchi hizo sita wataendelea kufanya mazungumzo kuhusu suala hilo tarehe 9 huko New York. Wachambuzi wameona kuwa, ingawa Iran inashikilia msimamo imara, lakini bado imeonesha unyumbufu wake ili suala hilo liweze kutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la nishati ya atomiki duniani IAEA Bwana Mohamed El Baradei kwenye ripoti yake iliyowasilishwa tarehe 28 Aprili katika shirika hilo na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa aliainisha kuwa, Iran haikuacha shughuli za kusafisha uranium ndani ya siku 30 zilizowekwa kutokana na taarifa ya mwenyekiti wa baraza la usalama iliyotolewa tarehe 29 mwezi March, lakini ripoti hiyo haikutoa ushahidi wa kutosha ulioweza kuthibitisha kuwa Iran ina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Kwenye mkutano huo, Marekani ilizihimiza nchi nyingine ziliunge mkono baraza la usalama kupitisha azimio litakaloishurutisha kisheria Iran iache shughuli za kusafisha uranium kutokana na utaratibu husika wa katiba ya Umoja wa Mataifa, yaani wakati amani ya kimataifa inapohatarishwa au vitendo vya uvamizi vinapotokea, baraza la usalama linaweza kuchukua hatua za lazima pamoja na mbinu za kijeshi ili matakwa ya jumuiya ya kimataifa yatekelezwe ipasavyo. Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, mjumbe wa China, ambaye pia ni msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China Bwana Cui Tiankai alisema, lengo la mkutano huo ni kubadilishana maoni kwa ipasavyo kuhusu suala la nyuklia la Iran, China inatetea suala hilo litatuliwe kwa njia ya kidiplomasia. Hivi sasa, japo nchi tatu za Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zinakubali baraza la usalama lipitishe azimio lenye msimamo kithabiti kuhusu suala la nyuklia la Iran, lakini pia zinasisitiza suala hilo litatuliwe kwa mazungumzo ya kidiplomasia.

Iran imeonesha misimamo ya aina mbili kuhusu suala hilo. Waziri wa mambo ya nje wa Iran Bwana Manouchehr Mottaki tarehe moja Mei alisisitiza kuwa, Iran haitaacha shughuli za kusafisha uranium. Makamu wa rais wa Iran, ambaye pia ni mwenyekiti wa shirika la nishati ya atomiki la nchi hiyo Bwana Gholam Reza Aghazadeh tarehe 2 Mei alitangaza kuwa, Iran imefaulu kupata asilimia 4.8 ya uranium safi. Habari nyingine zinasema, kama baraza la usalama litarudisha suala hilo litatuliwe kwenye mfumo wa IAEA, basi Iran itakubali zana zake za nyuklia zikaguliwe kwa ghafla.

Wachambuzi wameona kuwa, hivi sasa suala la nyuklia la Iran liko katika hali nyeti. Kama baraza la usalama litaiwekea Iran vikwazo mapema, si kama tu litaathiri uhusiano wa kawaida wa kiuchumi na nishati kati ya Iran na nchi nyingi, bali pia litasimamisha ushirikiano kati ya Iran na jumuiya ya kimataifa, na kuleta tishio kubwa kwa juhudi za jumuiya ya kimataifa za kutoeneza kwa silaha za nyuklia.

Kwa upande wa Marekani iliyohangaishwa na hali ya nchini Iraq, bado haina uwezo wa kuanzisha vita nyingine. Kwa upande mwingine, uranium iliyosafishwa nchini Iran bado ina uzito mdogo, bado haiwezi kutumiwa kutengeneza silaha za nyuklia. Hivyo suala la nyuklia la Iran bado lina muda wa kutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia.

Habari zinasema, Marekani na Umoja wa Ulaya zitawasilisha muswada wa azimio wenye msimamo kithabiti zaidi kuliko taarifa ya mwenyekiti wa baraza la usalama iliyotolewa tarehe 29 mwezi March kwenye baraza la usalama.

Wachambuzi wameona kuwa, nchi wanachama wa baraza la usalama bado zina tofauti kubwa kuhusu hatua zitakazochukuliwa kuhusu suala la nyuklia la Iran, hivyo hakuna uwezekano mkubwa kwa baraza la usalama kupitisha azimio la kuiwekea Iran vikwazo hivi karibuni. Hivi sasa suala la nyuklia la Iran bado liko kwenye njia ya kutatuliwa kwa mazungumzo ya kidiplomasia.

Idhaa ya Kiswahili  2006-05-03