Kuanzia miaka ya 60 ya karne iliyopita, madawa ya kulevya yalikuwa yameenea duniani kama ugonjwa wa tauni, ambapo idadi ya watu wanaotumia madawa ya kulevya inaongezeka siku hadi siku, na athari zilizoletwa na madawa hayo yamezidi kuwa mbaya siku hadi siku. Ripoti iliyotolewa na ofisi husika ya Umoja wa Mataifa kuhusu upigaji marufuku wa madawa ya kulevya duniani mwaka 2005 inaonesha kuwa, mwaka 2005, thamani ya biashara haramu ya madawa ya kulevya duniani ilifikia dola za kimarekani bilioni 322, ambayo inalingana na asilimia 0.9 ya jumla ya thamani ya uzalishaji mali ya nchi mbalimbali duniani. Watu milioni 200 duniani waliwahi kutumia madawa ya kulevya zaidi ya mara moja. Hakuna nchi yeyote duniani iliyoweza kuepukana na usumbufu wa madawa ya kulevya, hivyo nchi mbalimbali zinapaswa kushirikiana ili kutatua suala hilo la kimataifa.
Kushamiri kwa madawa ya kulevya si kama tu kumehatarisha moja kwa moja afya ya binadamu, bali pia kumeleta athari mbaya kwa maendeleo ya uchumi na jamii ya nchi mbalimbali.
Katika miongo kadhaa iliyopita, nchi mbalimbali duniani zilikuwa zimepata mafanikio makubwa katika kupambana na madawa ya kulevya, hasa zimefikia maoni ya pamoja katika kuzidisha ushirikiano wa kimataifa, hasa kati ya nchi zinazozalisha na zinazotumia madawa ya kulevya kwa wingi. Nchi nyingi zinazozalisha madawa ya kulevya ni nchi zinazoendelea, ambapo nchi nyingi zinazotumia madawa hayo ni nchi zilizoendelea, hivyo zinapaswa kufanya juhudi za pamoja katika kutokomeza uzalishaji na kuteketeza chimbuko la matumizi ya madawa ya kulevya. Katika miaka ya karibuni, nchi mbalimbali zimeimarisha ushirikiano katika sekta hiyo kwa kusaini makubaliano ya pande mbili mbili, pande nyingi na ya kikanda, na kupata mafanikio kadhaa katika jitihada za kupambana na madawa ya kulevya.
Mwaka 2004, idara za utekelezaji sheria za nchi za Amerika ya kati na sehemu ya Caribbean na Marekani zilishirikiana kuwakamata wahalifu muhimu 354 wa madawa ya kulevya, na kukamata tani 26.5 ya madawa ya kulevya aina ya cocaine na fedha taslimu zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 86. Mwaka huo huo, Mexico, Marekani na mkoa wa utawala maalum wa Hongkong wa China zilianzisha kwa pamoja kampeni ya kupambana na madawa ya kulevya, kugundua na kuharibu kundi moja kubwa lililoingiza fedha haramu kwenye mzunguko wa fedha na kusafirisha aina nyingi za madawa ya kulevya, kuwakamata wahalifu 90 waliofanya magendo ya madawa ya kulevya, na kukamata kiasi kikubwa cha cocaine, bangi na heroin na fedha taslimu.
Amerika ya kusini ni kituo kikubwa kabisa cha kuzalisha cocaine duniani. Mwaka 2005, Marekani na nchi za Ulaya ziliendelea kuzisaidia kifedha nchi za Amerika ya kusini kupambana na tatizo la madawa ya kulevya. Mwezi Mei mwaka jana, nchi zilizo karibu na mto Mekong zilisaini taarifa zikiamua kufanya ushirikiano katika kupambana na madawa ya kulevya kwa njia ya kiteknolojia na kifedha. Mwezi Oktoba mwaka jana, mkutano wa pili wa kimataifa wa ushirikiano wa kupambana na madawa ya kulevya kati ya nchi za kusini mashariki mwa Asia na China ulifanyika hapa Beijing, ambao ulipitisha taarifa ya Beijing na pendekezo la kuanzisha kampeni ya kikanda ya kupambana na uhalifu wa madawa ya kulevya.
China siku zote inatilia maanani kufanya ushirikiano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya. China imeshiriki katika shughuli nyingi za kimataifa na kikanda katika kupambana na madawa ya kulevya. Hadi leo, China imesaini makubaliano ya pande mbili mbili na nchi zaidi ya kumi katika kufanya ushirikiano wa kupammbana na dawa za kulevya, upashanaji habari na utekelezaji wa sheria.
Hivi sasa, jumuiya ya kimataifa imetambua kwa kauli moja umuhimu wa kupiga marufuku madawa ya kulevya. Kujenga dunia yenye afya, ustaarabu na usitawi ni matumaini ya pamoja ya watu wa nchi mablimbali. Lakini kutokana na hali ilivyo ya hivi sasa, mapambano dhidi ya madawa ya kulevya bado yana safari ndefu..
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-04
|