Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-05 21:22:15    
Serikali ya China kuboresha uwanja wa kimataifa wa michezo wa Kasarani

cri

Ziara ya rais wa Jamhuri ya watu wa China mheshimiwa Hu jintao iliyofanyika mwishoni mwa mwezi Aprili barani Afrika, ilikuwa ya kufana na yenye manufaa makubwa kwa mujibu wa wakazi wa bara hilo. Rais Hu Jintao aliweza kuzitembelea nchi za Nigeria, Morocco na Kenya barani Afrika miongoni mwa nchi nyingi za bara hilo.

Nchi ya Kenya ilikuwa miongoni mwa nchi hizo ambao zilinufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na ziara hiyo ya rais Hu Jintao. Pamoja na ufadhili wa mambo mengi ikiwemo uchimbaji wa madini na mafuta, ukarabati wa barabara, kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, ni kuwa serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pia imo mbioni kuukarabati uwanja wa michezo wa kimataifa wa Kasarani.

Hata kabla ya ziara ya rais wa China nchini Kenya, ni kuwa Redio China Kimataifa ambayo inasikika mjini Nairobi nchini Kenya kwenye masafa ya 91.9 FM, ilikuwa imeutembelea uwanja huo na kubaini kuwa ulihitaji msaada mkubwa kutoka kwa serikali ya China, kwa minajili ya kuboresha hadhi yake.

Na wasimamizi wa uwanja huo uliojengwa na serikali ya China mwaka 1987 kwa ajili ya mashindano ya bara Afrika, maarufu kama All Africa Games, wamefaulu sana kutokanana na ziara hiyo ya rais Hu Jintao.

Kulingana na Naibu Mkurugenzi katika kitengo cha Ufundi wa Halmashauri inayosimamia viwanja nchini Kenya, ni kuwa kwenye ziara hiyo ya rais Hu Jintao ambapo pia alikuwa ameandamana na waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai, aliyetenga wakati wake mbali na shughuli nyingi ili kuuzuru uwanja huo wa Kasarani.

Licha ya kufanya mazungumzo ya muda na waziri mwenzake wa biashara wa Kenya Bw. Mukhisa Kituyi, Bw. Bo aliweza kuutembelea uwanja wa Kasarani na kutathimini baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho katika uwanja huo wa Kasarani.

Naibu Mkurugenzi wa Usimamizi wa uwanja wa Kasarani Bw. Komora amesema kuwa, wanasubiri kazi ya kuukarabati uwanja wa Kasarani kuanza hivi punde, kulingana na maafikiano na mazungumzo waliyofanya na waziri Bo.

Kwa mujibu wa Bw. Komora ni kuwa, serikali ya China inafanya maandalizi kabambe pamoja na wahandisi na mafundi wenye ujuzi wa hali ya juu na kazi ya kuukarabati uwanja itaanza wakati wowote kuanzia sasa.

Bw. Komora ameendelea kusema kuwa, 'Uwanja wetu wa michezo wa kimataifa wa Kasarani utapata sura mpya kabisa, ambapo tutaimarisha sehemu ya kuchezea, ambayo tayari imechakaa. Aidha, tunapanga kujenga upya jukwaa la kukaliwa kwa wageni mashuhuri wanapokuwa wakishuhudi michezo katika uwanja wetu wa kimataifa wenye shughuli nyingi za kimichezo za humu nchini za kimataifa.'

Bw. Komora ameongeza kusema kuwa sehemu ya kompyuta yenye kuonyesha timu mbalimbali zinazocheza pamoja na mabao na matokeo, yaani score board kwa kimombo, pia itafanyiwa ukarabati.

Kadhalika, paa la uwanja huo pia litatengezwa ili kuzuia usumbufu ambapo mashabiki wamekuwa wakiupata wakati wa mvua. Naibu huyo Mkurugenzi amedokeza kuwa zipo baadhi ya sehemu za mapaa za uwanja huo ambazo zinavuja kutokana na ukuukuu wake, na hivyo zitahitaji kuboreshwa upya.

Sehemu ya uogeleaji, hoteli na mabweni pia ni sehemu ambazo zimo katika mpango wa kupewa sura mpya kwenye zoezi hilo la kuuboresha uwanja wa Kasarani.

Kadhalika, Naibu huyo Mkurugenzi ambaye kwa ushirikiano na seriakali ya China aliweza kuuzuru mji wa Beijing kwa mafunzo kuhusu usimamizi wa viwanja, amesena kuwa wanawasiliana mara kwa mara na wenzao walioko nchini China na kubadilishana mawazo kuhusu jinsi ya kusimamia mradi kama huo wa uwanja mkubwa na wenye shughulin nyingi za kila siku..