Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-05 21:27:14    
Kutafuta njia mwafaka ya ushirikiano kati ya China na Afrika

cri

Shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika lilianzishwa kwa pamoja na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, kituo cha mawasiliano ya kiuchumi na kiteknolojia ya kimataifa cha China na shirikisho la shughuli za Guancai la China, ni jumuiya isiyo ya kiserikali nchini China, hivi sasa lina wanachama zaidi ya 200, ambao wengi wao ni makampuni ya kibinafsi. Lengo la shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika ni kuyaelekeza makampuni ya China jinsi ya kuendeleza shughuli zao kwenye soko la Afrika, kuweka hali nzuri kwa kuhimiza maingiliano na ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia kati ya China na nchi za Afrika, na kusukuma mbele ushirikiano kati ya China na Afrika kwa kufuata hali halisi.

Shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika tangu lianzishwe mwezi March mwaka 2005 limefanya shughuli nyingi za kibiashara. Ili kufahamu vizuri zaidi mazingira ya uwekezaji ya nchi za Afrika, na kuanzisha uhusiano mzuri wa kibiashara na nchi mbalimbali za Afrika, kuanzia mwezi March hadi mwezi Aprili mwaka huu, shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika liliongoza ujumbe wa wanakampuni kufanya ukaguzi wa kibiashara katika nchi nne za Afrika ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkuu wa ujumbe huo, ambaye pia ni mkuu wa idara ya mawasiliano ya ofisi ya ukatibu ya shirikisho hilo Bwana Chu Shundang alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema:

"Safari yetu hii inalenga kuanzisha uhusiano kati ya shirikisho na mashirika ya kuhimiza uwekezaji na makampuni ya nchi za Afrika, jumuiya ya wachina wanaoishi katika nchi za Afrika, ubalozi na ofisi za kiuchumi na kibiashara za China katika nchi za Afrika ili kutoa huduma bora kwa wanachama wa shirikisho letu."

Katika ukaguzi wa siku 22, wajumbe hao walikuwa wametembelea idara na mashirika 30 ya nchi hizo nne, wakifanya makongamano kadhaa ya kibiashara, kufahamishwa hali ya kiuchumi, mazingira na sera za uwekezaji za nchi mbalimbali na kufikia makubaliano ya ushirikiano katika miradi kadhaa.

Bw. Chu Shundang alisema, bara la Afrika lina rasilimali nyingi, lakini miundombinu yake bado ni ya duni, hivyo makampuni ya China yanaweza kujishughulisha katika sekta nyingi, hasa sekta ya kilimo na ujenzi wa miundombinu, kama vile kilimo cha nafaka, ufugaji, utengenezaji wa mitambo ya kilimo na utengenezaji wa mazao ya kilimo. Nchi za Afrika pia zinatumaiini kuwa, wanakampuni wa China watawekeza nchini mwao na kuingiza teknolojia ya China katika nchi za Afrika. Akisema:

"Mbinu ya maendeleo ya makampuni ya vijijini na miji midogo nchini China yanafaa sana kwa nchi za Afrika. Nchi za Afrika zinaagiza bidhaa nyingi kutoka nchi za nje, lakini uwezo wake wa ununuzi ni mdogo, hivyo haifai kuanzisha viwanda vya kiwango kikubwa. Kama teknolojia, vifaa na mitaji ya makampuni ya vijijini na miji midogo ya China yatahamishwa katika nchi za Afrika, italeta manufaa kwa pande zote mbili."

Bw. Chu aliona kuwa, kuanzisha viwanda katika nchi za Afrika kutaleta manufaa zaidi kwa pande zote mbili kuliko kusafirisha bidhaa za China barani Afrika. Kwa upande mwingine, makampuni ya China yanapojiendeleza pia yataleta nafasi za ajira kwa wakazi wa nchi za Afrika na kusaidia kustawisha uchumi wa huko.

Kazi ya shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika si kama tu imeungwa mkono na serikali ya China, bali pia inafuatiliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa. Naibu mkuu wa idara ya mafunzo ya ofisi ya ukatibu ya shirikisho hilo Bwana Ge Kaiyong alisema:

"Shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika ni mradi wa kwanza wa ushirikiano kati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa na shirikisho la kuhimiza shughuli za Guancai la China. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamefanya kazi nyingi katika kutoa maelekezo ya kisera katika kuhimiza uwekezaji katika nchi za Afrika, yanataka kuthibitisha maelekezo yake yanafaa au la kwa maendeleo ya makampuni, kwa hivyo kazi ya shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika inalingana nakazi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa."

Mkutano wa mwaka uliofanywa mwanzoni mwa mwezi March mwaka huu na kamati inayoshughulikia uwekezaji, teknolojia na mitaji ya shirika la biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa na shirikisho la kuhimiza uwekezaji duniani ulimwalika mjumbe wa shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika, ambaye licha ya kujulisha hali ya uzalishaji na kazi ya shirikisho hilo mkutanoni, pia amefanya mazungumzo na wakuu wa mashirika ya kuhimiza uwekezaji ya nchi mbalimbali za Afrika kuhusu jinsi ya kuanzisha ushirikiano wa muda mrefu ili kuhimiza kwa pamoja mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Afrika.

Isitoshe, wakati ujumbe wa shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika ulipofanya ukaguzi wa kibiashara nchini Kenya, shirika la biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa na idara ya kuhimiza uwekezaji ya Kenya zilikuwa zimefanya kongamano maalum kwa ujumbe huo, na kuwafahamisha wajumbe wa China sera na mazingira ya uwekezaji ya Kenya. Baadaye pia zilifanya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya wanakampuni wa China na wa Kenya, ambao walijadiliana njia mwafaka ya ushirikiano.

Bw. Chu Shundang alisema, serikali ya China siku zote inatilia maanani kukuza uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati yake na nchi za Afrika, kubuni mkakati husika wa kuwahimiza wanakampuni wa China kuwekeza katika nchi za Afrika. Lakini wanakampuni wengi wa China bado wanakabiliwa na matatizo ya aina mbalimbali ya kuwekeza vitega uchumi katika nchi za Afrika, kama vile hawafahamu lugha, sheria, mila na desturi, sera na mazingira ya uwekezaji ya nchi za Afrika. Hivyo shirikisho la wafanyakazi wa China na Afrika lina shughuli nyingi za kufanya, jambo la kwanza ni kuwasaidia wanachama wa shirikisho hilo wafahamu hali halisi ya nchi za Afrika, kuweza kugundua nafasi za kibiashara, na jinsi ya kukwepa hatari, ili wajiendeleze vizuri katika nchi za Afrika.

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-05