Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-08 19:07:04    
Milipuko inaongezeka kabla ya serikali mpya ya Iraq kuundwa

cri

Wakati waziri mkuu mpya wa Iraq Bw. Jawad al-Maliki anaposhughulika kufanya mazungumzo ya mwisho na viongozi wa makundi mbalimbali kuhusu mgawanyiko wa madaraka ya serikali, milipuko inazidi kuongezeka nchini Iraq.

Tarehe 7 milipuko mitatu ya mabomu yaliyotegwa ndani ya gari ilitokea katika sehemu ya kaskazini ya mji mkuu wa Iraq, Baghdad, na ilisababisha vifo vya watu 12 na wengine 26 kujeruhiwa. Habari zinasema, milipuko miwili ya mwanzo iliwalenga askari doria wa serikali na askari doria wa polisi, na mlipuko wa tatu ulitokea karibu na chuo cha sheria. Katika siku hiyo mlipuko wa bomu la kujitoa mhanga pia ulitokea katika mji wa Kerbala, kusini mwa Iraq, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 21 na watu 52 kujeruhiwa. Pamoja na hayo, polisi wa Iraq waligundua maiti 50 mjini Baghdad na sehemu ya kusini ya mji huo. Kadhalika, jeshi la Marekani nchini Iraq tarehe 7 lilitangaza kuwa askari mmoja wa Marekani aliuawa katika mashambulizi yaliyofanyika siku hiyo katika jimbo la Anbar, magharibi mwa nchi hiyo.

Kabla ya hapo, tarehe 6 helikopta ya Uingereza ilianguka katika mji wa Basra, mji unaomilikiwa na madhehebu ya Shiya, watu watano waliokuwa ndani ya helikopta hiyo wote walikufa. Polisi nchini Iraq ilidai kwamba helikopta hiyo ilitunguliwa kwa roketi, lakini usemi huo haujathibitishwa na Uingereza. Mgogoro kati ya askari wa Uingereza na wakazi wa Basra uliotokea katika siku hiyo ulisababisha vifo vya raia watano na kumi kujeruhiwa, na baadaye siku hiyo jeshi la Uingereza lilipiga marufuku kutembea ovyo usiku mpaka tarehe 7.

  

Wachambuzi wanaona kuwa hali mbaya hiyo inatokana na sababu tatu:

Kwanza, kundi la al-Qaeda linaloongzwa na Abu Musab al-Zarqawi linajaribu kuharibu mchakato wa kisiasa. Tarehe 22 ya mwezi uliopita, kiongozi wa chama cha "Islamic Dawa" cha madhehebu ya Shiya Jawad al-Maliki aliteuliwa kuwa waziri mkuu mpya, jambo ambalo limekwamua mchakato wa kisiasa, lakini siku tatu tu baadaye, tarehe 25 Aprili Abu Musab al-Zarqawi alitangaza kwenye mtandao wa internet akisema, hataitambua serikali mpya itakayoundwa na kutishia kwamba atafanya mashambulizi mengi zaidi. Jeshi la Marekani linaona kwamba milipuko kadhaa iliyotokea karibu na Baghdad na sehemu nyingine ni vitendo vilivyopangwa na Zarqawi kwa lengo la kuharibi mchakato huo wa kisiasa.

Pili, uhasama kati ya madhehebu ya dini ya Kiislamu ni wa muda mrefu, matukio ya kuuana hayaishi. Polisi nchini Iraq inaona kwamba maiti 50 zilizogunduliwa Baghdad na sehemu ya kusini ya mji huo pengine ni watu waliouawa katika mauaji ya wenyewe kwa wenyewe kati ya madhehebu.

Tatu, watu wa Iraq wanapinga majeshi ya nchi za nje kuikalia nchi yao.

Wachambuzi wanaona kwamba hali mbaya ya usalama nchini Iraq inaharakisha makundi mbalimbali yaunde serikali mpya mapema iwezekanavyo ili kuleta usalama nchini humo. Naibu rais wa Iraq Adil Abd al-Mahdi tarehe 6 alikadiria kwamba serikali mpya itaundwa katika siku chache zijazo, lakini viongozi wengine wanaona kwamba kwa sababu chama cha "Iraqi Front for National Dialogue" ambacho ni chama cha madhehebu ya Shiya kimetoa ombi la wadhifa wa waziri wa mambo ya nje na kusababisha mgogoro kati yake na chama cha Kurdstan Coalition, orodha ya mawaziri itakuwa ni shida kutolewa katika katika mkutano wa bunge utakaofanyika katika Jumatano ya wiki ijayo.

Hali mbaya ya usalama nchini Iraq inaisumbua sana serikali ya Bush. Kwa upande mmoja askari wa Marekani nchini humo wanazidi kuuawa kadiri siku zinavyokwenda, sera za Marekani kuhusu Iraq zinapingwa zaidi na watu wa Iraq. Kwa upande mwingine, hali mbaya ya usalama ni athari mbaya kwa utulivu wa kanda na kuzifanya nchi washirika wa Marekani za Ghuba kuwa na wasiwasi kuhusu vita vya Mashariki ya Kati. Viongozi wa nchi sita za Ghuba kwenye mkutano wa wakuu wa nchi walitumai Marekani itatue suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo badala ya vita, kwani vita vikitokea kati ya Marekani na Iran vitaleta hali mbaya zaidi ya uchumi na usalama kuliko vita vya Iraq.

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-08