Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-09 16:14:00    
China yahimiza maendeleo ya sekta ya ujenzi wa majengo yanayopunguza matumizi ya nishati

cri

Hhivi sasa uchumi wa China unakuwa kwa haraka na kwa utulivu, takwimu mpya zinaonesha kuwa ongezeko la pato la taifa katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu lilizidi lile la kipindi kama hiki cha mwaka uliopita kwa 10%. Katika hali yenye maendeleo ya kasi ya uchumi, sura za miji na vijiji vya China zimekuwa na mabadiliko makubwa, ambapo majengo mengi mapya yamejengwa. Ili kuleta maendeleo mwafaka kati ya ujenzi wa miji na vijiji pamoja na mazingira, na kupunguza matumizi ya rasilimali na nishati, hivi sasa China inajitahidi kuhimiza ujenzi wa majengo ya kijani na kazi za kupunguza matumizi ya nishati katika majengo.

Hivi sasa majengo yanayojengwa kila mwaka ni kiasi cha mita za mraba kati ya bilioni 1.5 na bilioni2, na Inakadiriwa kwamba hadi kufikia mwaka 2020, China itajenga majengo mapya yenye ukubwa wa mita za mraba kiasi cha bilioni 30, ukubwa wa majengo na kasi ya ujenzi ni nadra sana kutokea duniani. Lakini endapo hali ya matumizi ya nishati ya hivi sasa itaendelea vivyo hivyo, basi matumizi ya nishati ya sekta ya majengo katika miaka iliyopita yatachukua karibu nusu ya matumizi ya nishati ya jamii nzima.

Ili kuleta maendeleo mwafaka kati ya ujenzi wa miji na vijiji pamoja na mazingira, serikali ya China imeanza kuhimiza majengo ya kijani. Majengo ya kijani ni majengo ambayo yanatoa nafasi za kuishi na kufanya shughuli kwa raha na usalama, vilevile yanainua ufanisi wa matumizi ya nishati na kupunguza athari kadiri iwezakanavyo juu ya mazingira ya asili. Majengo ya namna hiyo yanatumia vifaa ambavyo binadamu na magari madogo yanaweza kuvisafirisha ili kupunguza matumizi ya nishati zinazohitajiwa katika usafirishaji. Licha ya hayo, kutumia bomba linalonyunyizia maji wakati wa kuoga na kutumia tanki ndogo la maji ya kusafishia choo, kuweka zana za kutumia nishati ya mwangaza wa jua na kukusanya maji ya mvua kwenye mapaa ya nyumba ili kupunguza matumizi ya rasilimali. Waziri wa ujenzi wa China Bw. Wang Guangtao hivi karibuni alisema, kuhimiza kazi za upunguzaji wa matumizi ya nishati kwa sekta ya majengo na kufanya marekebisho dhidi ya majengo ya zamani ni mambo yaliyowekwa katika mpango wa maendeleo wa China katika siku za baadaye.

Upunguzaji wa matumizi ya nishati wa sekta ya majengo na majengo ya kijani ni moja ya mambo yaliyotiliwa mkazo katika mpango wa taifa wa maendeleo ya sayansi na teknolojia wa kipindi kirefu na cha wastani. Hivi sasa licha ya kuweka kanuni za kutaka ujenzi wa majengo kufuata kwa makini kigezo cha usanifu cha kudhibiti matumizi ya nishati, serikali inafanya marekebisho hatua kwa hatua dhidi ya majengo yaliyopo hivi sasa na ya kizamani. Inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2020, China itakuwa imepunguza matumizi ya umeme ya kilowati bilioni 420 na makaa ya mawe tani milioni 260, pamoja na kupunguza utoaji wa hewa unaoifanya dunia kuwa na joto ikiwemo hewa ya carbon dioxide ya tani milioni 846."

Ili kuhimiza maendeleo ya majengo ya kijani, serikali ya China imeweka vigezo vingi vya upunguzaji wa matumizi ya nishati wa majengo na kuweka mifano ya kuigwa ya majengo yenye ukubwa wa mita za mraba karibu milioni 5 katika jumla ya mikoa na miji 19. Licha ya hayo, serikali ya China inaunga mkono utafiti na uenezaji wa teknolojia ya majengo ya kijani, ambapo miradi mingi ya utafiti imepata maendeleo makubwa kutokana na msaada wa serikali, na mafanikio mengi yameshatumika ikiwa ni pamoja na teknolojia ya kutumia maji machafu yaliyosafishwa na kuta za majengo zinazotunza joto katika nyumba.

Takwimu zinaonesha kuwa hivi sasa nchini China kuna majengo ya mita za mraba bilioni 13 kati ya bilioni 40, ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho ya kupunguza matumizi ya nishati. Ikiwa gharama ya marekebisho ni Yuan 200 kwa kila mita za mraba, basi marekebisho ya upunguzaji wa matumizi ya nishati ya majengo yatakuwa na soko kubwa la Yuan trioni 2.6. Nafasi kubwa ya biashara inavutia kampuni nyingi kushiriki utafiti wa teknolojia ya majengo ya kijani na vifaa vya ujenzi. Kwenye maonesho ya vifaa vya majengo ya kijani yaliyofanyika hivi karibuni mjini Beijing, msaidizi wa maneja mkuu wa kampuni ya vioo vya kuta za kijani ya Beijing Bw. Wu Shutian alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa vioo vya kampuni yao vyenye uwazi katikati yake vinapunguza sana matumizi ya nishati:

"Vioo vyenye uwazi katikati vinaweza kuzuia joto lisipite kwenye vioo, hivyo vinafaa kwa majira ya siku za joto na baridi na katika sehemu yoyote duniani. Vioo vya aina hiyo vinaweza kutumika katika sehemu nyingi zikiwa ni pamoja na kuta za vioo za majengo na madirisha."

Bw. Wu Shutian alisema, vioo vya aina hiyo vinaweza kuzuia hasara ya matumizi mengi ya nishati kutokana na kuzuia joto ndani ya nyumba lisitoke kwa kupitia vioo vya madirisha katika majira ya baridi, na kuzuia joto la nje lisiingie ndani katika majira ya joto, hivyo matumizi ya umeme ya viyoyozi na heater yanapungua. Hivi sasa vioo vyenye uwazi katikati vya mita za mraba zaidi ya milioni 100 vimetumika katika majengo mengi maarufu duniani.

Maendeleo ya siku za baadaye ya soko la vifaa vya ujenzi la China yanavutia kampuni nyingi za upunguzaji wa matumizi ya nishati duniani, meneja mkuu wa kampuni maarufu ya taa za majengo ya Delmatic Bw. Stephen Woodnutt alimwambia mwandishi wetu wa habari,

"Soko la majengo ya kijani la China linavutia sana kampuni yetu, mfumo wa taa ya kuleta mwangaza unatumika katika majengo ya umma, biashara na wakazi. Mfumo huu licha ya kuweza kutumika katika majengo mapya, pia unaweza kutumika katika majengo yanayorekebishwa."

Katika upande wa kuhimiza majengo ya kijani na upunguzaji wa matumizi ya nishati, China inafanya ushirikiano wa kimataifa na kujifunza teknolojia na uzoefu wa kimaendeleo duniani. Mradi wa kufanya marekebisho ya kupunguza matumizi ya nishati juu ya majengo ya zamani, ambao umepewa msaada na serikali ya Ujerumani wa Euro milioni 5 umezinduliwa kwenye mji wa Tangshan, mkoani Hebei, kazi muhimu za mradi huo ni kuinua ufanisi wa upunguzaji wa matumizi ya nishati ya majengo kwa kufanya marekebisho juu ya sehemu za majengo zikiwa ni pamoja na kuta, madirisha na mapaa ya majengo na mfumo wa kupasha joto katika majira ya baridi. Hivi sasa wizara ya ujenzi ya China ilisaini mkataba wa ushirikiano na Kampuni ya United Technologies ya Marekani ili kufanya utafiti kuhusu majengo ya kijani na uenezaji wa uzoefu wa upunguzaji wa matumizi ya nishati. Tunaamini kuwa kutokana na jitihada ya pamoja ya serikali, kampuni na sekta ya sayansi na teknolojia, kazi za upunguzaji wa matumizi ya nishati ya majengo ya China zitapata hatua kubwa za maendeleo.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-09