Msemaji wa serikali ya Iran, Bw. Gholamhossein Elham, tarehe 8 huko Tehran alisema, rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran alimwandikia barua rais Bushi wa Marekani na kutoa "mapendekezo mapya" kuhusu utatuzi wa masuala ya kimataifa na kupunguza hali ya wasiwasi duniani. Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa Iran kumwandikia barua rais wa Marekani tangu nchi hizo mbili zilipovunja uhusiano wa kibalozi miaka 20 iliyopita.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari Bw. Elham alisema, waziri wa mambo ya nje wa Iran Manouchehr Mottaki amemwomba balozi wa Uswis nchini Iran apilize baru hiyo kwa Marekani. Alisema, kwenye barua hiyo Bw. Ahmadinejad ametoa mapendekezo mapya kuhusu utatuzi wa masuala ya kimataifa na kutuliza hali ya wasiwasi duniani. Lakini hakusema wazi kama barua hiyo imehusisha suala la nyuklia la Iran, bali alisema tu kwamba "suala la nyuklia la Iran pia ni suala la kimataifa, na masuala ya kimataifa yanamaanisha pia suala la nyuklia la Iran." Katika siku hiyo, mjumbe wa kwanza wa mazongumzo wa Iran Bw. Ali Larijani alipozungumza na waandishi wa habari alisema, "pengine barua hiyo itapiga hatua kubwa ya kidiplomasia", lakini haimaanishi kwamba Iran imelegeza msimamo wake kuhusu suala la nyuklia.
Mwaka 1980 Marekani ilikata uhusiano wa kibalozi na Iran. Katika muda wa miaka 26 iliyopita marais wa nchi hizo mbili hawakuwa na mawasiliano yoyote ya moja kwa moja. Ni jambo la kushangaza kwamba wakati wachambuzi wanapoona ajabu kuhusu rais wa Iran kumwandikia barua rais Bush wa Marekani, bei ya mafuta katika soko la kimataifa imepungua hadi chini ya dola za Kimarekani 70 kwa pipa.
Baada ya "mshangao" na kutafakari kuhusu barua ya rais Ahmadinejad kwa rais Bush, vyombo vya habari vimetoa maoni yao. Redio ya Sauti ya Ujerumani ilisema, "wachambuzi wengi wanaona kuwa ni Marekani na Iran tu, nchi hizo mbili zenye uhasama kwa muda mrefu zitakapofikia maafikiano ndipo suala la nyuklia la Iran litakuwa na matumaini ya kutatuliwa."
Baadhi ya wachambuzi wanaona, katika siku za karibuni, matumaini ya Iran ya kutaka kuzungumza moja kwa moja na Marekani yamekuwa wazi siku hadi siku, barua ya Ahmadinejad kwa Bush imedhihirisha zaidi matumaini hayo. Iran inaelewa fika kwamba katika utatuzi wa suala la nyuklia la Iran nchi yenye kauli ya mwisho sio Umoja wa Ulaya wala Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, bali ni Marekani. Siku chache zilizopita, Iran ilitangaza imefanikiwa kupata uranium safi kwa kiwango cha chini, tangazo hilo pia linachukuliwa kama ni shinikizo kwa Marekani kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Iran.
Pamoja na hayo, Iran inaelewa kwamba Marekani inataka Iran itoe msaada katika suala la usalama wa Iraq. Mwezi Novemba mwaka uliopita, rais Bush alimwagiza balozi wake mjini Baghdad ashauriane na Iran kuhusu hali mbaya ya usalama nchini Iraq. Kwa hiyo Iran inajaribu kuunganisha pamoja suala la nyuklia la Iran na suala la Iraq katika mazungumzo na Marekani. Katika barua hiyo, Iran haikutaja moja kwa moja suala la nyuklia bali imetoa "mapendekezo mapya" kuhusu masuala ya kimataifa kwa ujumla, hii imedhihirisha wazi zaidi kwamba Iran inataka kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani kuhusu suala la nyuklia la Iran pamoja na masuala mengine.
Isitoshe, wakati wa kutoa barua hiyo sio wa kawaida. Wachambuzi wanaona kwamba sababu ya kutoa barua hiyo katika muda wa saa chache kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tano za kudumu katika Baraza la Usalama pamoja na Ujerumani kufanyika ni kwa ajili ya kujaribu kuvutia uungaji mkono kutoka nchi hizo ili kupata matokeo mema ya mkutano huo.
Msemaji wa ikulu ya Marekani Bw. Scott McClellan tarehe 8 alisema, ikulu ya Marekani imepata barua hiyo kutoka kwa ubalozi wa Uswis nchini Iran, lakini hakudokeza yaliyomo ndani ya barua hiyo. Hata hivyo alisema, barua hiyo haikutoa hatua yoyote ya maana kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la Iran. Msaidizi wa rais wa Marekani kuhusu usalama wa taifa Bw. Stephen Hadley alipozungumza na waandishi wa habari alisisitiza msimamo wa Marekani, nao ni kuitaka Iran isimamishe shughuli zote za nyuklia ili kuleta msingi wa kutatua suala hilo kwa njia ya amani.
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-09
|