Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-10 17:53:31    
Satelaiti ya kuchunguza rasilimali za dunia iliyosanifiwa kwa pamoja kati ya China na Brazil yatumika kwenye sekta mbalimbali

cri

Satelaiti ya kuchunguza rasilimali za dunia iliyosanifiwa kwa pamoja kati ya China na Brazil hivi sasa inatumika kwenye sekta mbalimbali. Katika kipindi hiki cha elimu na afya, tunawaelezeni matumizi ya satelaiti hiyo.

Satelaiti ya kuchunguza rasilimali za dunia inatumika katika kuchunguza na kutafiti rasilimali za kimaumbile za dunia kutoka angani. Inaweza kuchunguza miundo ya ndani ya ardhi na rasilimali zilizoko chini ya ardhi, pia inaweza kusimamia rasilimali za misitu, bahari na hewa, na kutoa tahadhari za maafa mbalimbali makubwa ya kimaumbile. Tokea miaka ya 90 ya karne iliyopita, China na Barzil zilianza kushirikiana katika kutafiti na kusanifu satelaiti ya aina hiyo. Mwaka 1999 satelaiti ya kuchunguza rasilimali za dunia No. 1 ilirushwa kwa mafanikio, baada ya miaka minne, satelaiti No.2 ilianza kufanya kazi badala ya satelaiti ya kwanza, na bado inafanya kazi hivi sasa. Bolozi wa Brazil nchini China alisema:

"ushirikiano huo unasaidia China na Brazil kuwa na teknolojia za juu katika sekta hiyo, na kuimarisha uwezo wa nchi hizo mbili katika kusimamia na kutoa tahadhari za maafa na masuala ya mazingira. Satelaiti hiyo ni chombo kizuri katika sekta nyingi na ina umuhimu mkubwa katika kukidhi mahitaji ya maendeleo ya nchi hizo mbili."

Satelaiti hiyo ya No. 2 inachunguza dunia mchana na usiku na kuleta picha kwa kupitia mfumo wa kasi wa kutuma data, data hizo hushughulikiwa na kuwa picha au nyaraka nyingine zinazohitajika. Mkurugenzi wa taasisi ya matumizi ya satelaiti ya kuchunguza rasilimali za dunia ya China Bw. Guo Jianning alisema,

"Satelati No. 2 ina sifa nzuri zaidi na uwezo mkubwa zaidi wa kushughukilia picha kuliko satelati No. 1. matumizi ya data zake pia yamepanuliwa katika sekta mbalimbali. Mikoa na miji yote nchini China imetumia data za satelaiti hiyo."

Imefahamika kuwa, hivi sasa data zinazopatikana kwenye satelaiti hiyo zinatumika katika sekta nyingi, zikiwemo sekta za kilimo, misitu na maji, na zimeleta manufaa dhahiri ya kijamii na kiuchumi. Kwa mfano katika kilimo, satelaiti hiyo inatumika katika kupima eneo linalopandwa mimea, kusimamia hali ya ukuaji wa mimea na kutathimini uzalishaji wa mazao. Mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa remote sensing ya mkoa wa Shanxi Bw. Li Wenke alieleza:

"data zinazopatikana kwenye setelaiti hiyo zina umaalum wake, kwanza ni bei nafuu kuliko satelaiti ya SPOT ya Ufaransa na satelaiti TM ya Marekani, pili ni kwamba tunaweza kupata data mara moja kwa usahihi na ufanisi kutoka kwenye satelaiti hiyo, ya tatu ni kuwa uwezo wake pia unaweza kukidhi mahitaji ya sekta ya kilimo."

Mbali na hayo, China pia inatumia data zinazopatikana kwenye satelaiti hiyo kushiriki kwenye mradi wa kimataifa wa uchunguzi wa rasilimali za ardhi na maji duniani. Katika miaka iliyopita, baraza la jamii na uchumi la Asia na Pasifiki la Umoja wa Mataifa lilianzisha mradi wa usimamizi wa jumla wa rasilimali za ardhi na maji kwenye sehemu zenye ukame, na kutaka kuinua uwezo wa kukabililana na ukame kwenye sehemu hizo. Mtafiti wa taasisi ya matumizi ya remote sensing ya taasisi ya sayansi ya China Bw. Wang Changyao alisema, mbali na China, nchi za Korea ya Kaskazini, Mongolia, Kazakstan, Uzbekistan na Pakistan pia zilishiriki kwenye mradi huo, na kila nchi ilichukua eneo moja kufanya majaribio nchini mwake. China iliweka sehemu ya Shihezi ya Xinjiang kuwa eneo la kufanya majaribio. wakati huo, China imepata mafanikio mengi katika utafiti wa ugawanyaji wa aina za matumizi ya ardhi na mbinu za kugawanya aina za picha kwa kutumia data zilizopatikana kwenye satelaiti hiyo, na mafanikio hayo yalisifiwa na nchi zilizoshiriki kwenye mradi huo.

Mbali na hayo, hivi sasa satelaiti hiyo imeonesha ufanisi wake katika shughuli za kusimamia na kutoa tahadhari za maafa na mipango ya miji. Kwa mfano, mwezi Juni mwaka 2004, maporomoko ya ardhi yaliyotokea katika sehemu ya juu ya mto wa Pali unaopita kwenye mpaka wa China na India, tukio hilo ilitiliwa maanani sana na serikali za nchi hizo mbili. Wakati huo China ilitumia data zilizopatikana kwenye satelaiti hiyo na kusimamia na kutoa tahadhari za maafa hayo. Bw. Wei Chengjie aliyeshiriki kwenye kazi hiyo alisema,

"Tulitumia data zilizopatikana kwenye satelaiti hiyo katika kusimamia moja kwa moja na kwa mfululizo sehemu zilizokumbwa na maafa hayo. Tulitoa taarifa 7 kuhusu hali ya maafa na kufafanua vilivyo hali ya kutokea kwa maafa hayo."

Aidha, China pia ilikusanya data nyingi kwa kutumia satelaiti hiyo, kufanya utafiti kuhusu tsunami iliyotokea mwaka jana kwenye bahari ya Hindi, na kutoa matokeo ya utafiti huo kwa nchi na sehemu zilizoathiriwa na maafa hayo. Mkurugenzi wa kituo cha matumizi ya satelaiti ya uchunguzi wa rasilimali za dunia cha China Bw. Guo Jianning alieleza, ili kuwawezesha watu watumie data za satelaiti hiyo kwa ufanisi zaidi, kuanzia mwezi Aprili, data zinazopatikana kwenye setalaiti hiyo zimetolewa bure kote nchini, na China pia inatoa data hizo kwa nchi kadhaa, zikiwemo Malaysia, Viet Nam na Iran. Bw. Guo Jianing alisema, kutokana na uwezo mkubwa wa setalaiti hiyo, imeanza kufuatiliwa na jumuiya ya kimataifa:

"hivi sasa nchi nyingi duniani zinataka kuweza kutumia data zinazopatikana kwenye setalaiti hiyo. China imeamua kwa hatua ya mwanzo kufanya majaribio ya kutumia na kugawa data hizo nchini Australia, Canada na Norway mwaka huu."

Imefahamika kuwa, hivi sasa China na Brazili zinashirikiana katika kusanifu satelaiti ya aina hiyo ya No. 3 na No. 4 zenye uwezo mkubwa zaidi, na matumizi yake yatakuwa na mustakabali mzuri zaidi na kuhudumia sekta nyingi zaidi.

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-10