Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-10 20:10:59    
Hali ya kukwama kuundwa kwa serikali ya Iraq inatazamiwa kutatuliwa

cri

Waziri mkuu mpya wa Iraq Bw. Nouri al-Maliki tarehe 9 alitangaza kuwa, ingawa mawaziri wa wizara za biashara na mawasiliano ambazo ni idara nyeti katika ukarabati wa uchumi hawajachaguliwa, lakini makudi yote yamekubali nyadhifa za uwaziri wa mambo ya ndani na ulinzi wa taifa zitolewe kwa watu wasio na chama na wasio na uhusiano wowote na makundi ya wanamgambo. Mawaziri wa mafuta, fedha na mambo ya nje wamekwisha chaguliwa, na muundo wa serikali umemalizika kwa 90%. Kwa makadirio, orodha ya mawaziri itawasilishwa kwenye bunge ndani ya wiki hii.

Vyombo vya habari vinaona kwamba kuwapa watu wasio na chama nyadhifa za uwaziri wa mambo ya ndani na ulinzi wa taifa ni uamuzi wa busara kwa ajili ya kukwamua hali ya kukwama kuundwa kwa serikali katika muda uliodumu wa miaka mitano na umehakikisha usalama katika ukarabati wa taifa, kwa sababu wizara hizo mbili zinatawala jeshi la serikali na askari polisi nchini Iraq, na madhehebu yanayopingana ya Suni na Shiya yote hayataki nyadhifa hizo zimilikiwe na upinzani wake. Katika kipindi cha mpito, waziri wa mambo ya ndani Bw. Bayan Jabr alikuwa mtu wa madhehebu ya Shiya, dhehebu la Suni lilimshutumu kuwa wizara yake ilikuwa ni idara ya kunyanyasa watu wa Suni na kutaka kubadilisha uongozi wa wizara hiyo uliodhibitiwa na dhehebu la Shiya, na kuwatimua askari wa dhehebu la Shiya kutoka jeshi la ulinzi lililokuwa chini ya wizara ya mambo ya ndani. Kadhalika, waziri wa ulinzi wa taifa katika kipindi cha mpito, Bw. Saadoun al-Duleimi, ingawa alikuwa ni mtu huru wa dhehebu la Suni, lakini alionekana kuwa ni mdhaifu katika utendaji mambo, hata hivyo, katika mwezi Oktoba mwaka jana alipopambana na kundi lenye silaha la dhehebu la Shiya lililokuwa linalipinga jeshi la Marekani katika jimbo la Anbar alisema, "Tutawaangamiza wao wote pamoja na wake zao, watoto wao na nyumba zao." Kauli hiyo ilisababisha hasira kubwa miongoni mwa watu wa dhehebu la Shiya. Katika kipindi hicho cha mpito wizara hizo mbili hazikuwajibika ipasavyo, bali zilikosolewa kwamba zilishiriki kwenye migogoro ya madhehebu na kuwa chanzo cha machafuko.

Kwa hiyo, katika hali ambayo migogoro ya kikabila na migongano kati ya madhehebu ya dini bado inaendelea hadi sasa, uamuzi wa kuwapa watu wasio na chama nyadhifa za uwaziri wa wizara hizo mbili za mambo ya ndani na ulinzi wa taifa unachukuliwa kama ni msingi wa kuunganisha makundi yote na kuunda serikali inayounganisha vyama na makundi, madhehebu na makabila, na pia ni msingi wa kujenga imani kati ya vyama na makundi na kutuliza migogoro, na mwishowe kutimiza utulivu wa kitaifa.

Lakini baadhi ya wachambuzi wanaona vingine, kwamba ingawa nafasi hizo mbili muhimu za uwaziri wa mambo ya ndani na ulinzi wa taifa zimeamuliwa zitachukuliwa na watu wasio na chama, lakini haimaanishi kwamba migogoro kati ya madhehebu imeisha. Na nafasi za uwaziri wa wizara za biashara, mafuta na mawasiliano ambazo ni muhimu kwa maslahi ya madhehebu yote na makabila hazijaamuliwa, hakika migongano kati ya madhehebu na makabila itaendelea. Katika hali hiyo, kama makundi mbalimbali hayatatanguliza mbele maslahi ya kitaifa na kuendelea kugombea madaraka kwa ajili ya maslahi binafsi, mchakato wa kuunda serikali mpya utakumbwa na matatizo.

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-10