Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-10 20:27:01    
Jinsi utamaduni wa Mswahili unavyozidi kukuzwa katika kisiwa cha Lamu nchini Kenya.

cri

Msomi-mtaalamu-mtafiti wa Kiswahili Bw. Ahmed Shekhe Nabahan, ni miongoni mwa wasomi adimu na tunu kubwa katika eneo la Afrika Mashariki na Afrika nzima kwa ujumla, ambaye kila leo hutafutwa kwa udi na uvumba na wapenzi wa lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Mswahili.

Sio Waamerika, Wachina, Wajapani, Wairan, Wajerumani, Waingereza, bali kila mtafiti wa Kiswahili anapotua barani Afrika, basi moja kwa moja humtafuta msomi huyo, mzawa wa kisiwa cha Lamu mkoani Pwani nchini Kenya, kwa ajili ya kujua mambo mbalimbali ya Kiswahili. Idhaa za Kiswahili za kitaifa na kimataifa kama vile BBC, Deutsche Welle, Radio Iran, VOA, Oman na nyenginezo chungu nzima; na sasa Redio China Kimataifa, pia zimemfuatilia Bw. Nabahan kwa mahojiano ili kujua asili ya mswahili.

Haijawahi kutoka makongamano, warsha na semina za Kiswahili kufanyika bila kumhusisha Shekhe Nabahan.

Redio China Kimataifa ilipotembelea ofisi ya msomi huyo katika mji wa Kale wilayani Mombasa, ilimkuta akiwa anajiandaa kwa sherehe za Utamaduni wa Mswahili zitakazoandaliwa jijini Tanga nchini Tanzania, mbali na kusubiri kuwapaokea wanafunzi wanaofanya utafiti wa Kiswahili kutoka Marekeni kwenye mwezi Juni.

Bw. Nabahan ni mwasisi wa kituo cha kufundisha lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Mswahili, maarufu kama "Kituo cha Uchunguzi wa mambo ya Kiswahili." na huwapokea wageni wengi kila leo. Aidha, kwa sasa Bw. Nabahan anawasubiri mwanafunzi wake kutoka nchini Ujerumani anayesomea shahada ya uzamili katika mchepuo maalum wa utafiti kuhusu Mswahili na utamaduni wake.

Shekhe Nabahan ametunga na kuchapisha vitabu kadha vya Kiswahili vikiwemo: Sambo ya Kiwandowe, Umbuji wa Kiwandowe, Umbuji wa mnazi, mbali na kuandika makala ndefu yenye kusimulia historia ya majahazi ama mitepe iliyotumiwa na Waswahili tangu zama za mababu, na vitabu vinginevyo vingi.

Kuhusu historia ya mashairi, Bw. Nabahan anasema:

"Kinyume na mashairi nionayo mimi yakichapishwa zama za leo katika magazeti, ni kuwa malenga wa kileo kidogo wamepoteza mwelekeo. Hawa wana-mashairi chipukizi hawazingatii kikamilifu bahari za Kishairi inavyopasa. Lazima mashairi kwa jinsi ilivyokuwa historia ya ushairi katika visiwa vya Uswahilini kama Lamu, Pate, Siwu, Ngazija na Unguja, yawe na mafumbo, ujumbe mzito na lugha nzito yenye kueleweka tu kikamilifu na walengwa wake."

Bw. Nabahan ameongeza kuwa ni sharti malenga na manju mzuri akue hatua kwa hatua katika fani ya ushairi, wala sio kujikweza tu ubingwa na daraja la ushairi mwenyewe kama ilivyo leo.

Ni kwa uzingativu wa masharti yote hayo katika utunzi wa mashairi ndipo Kiswahili na utamaduni wa Mswahili waweza sio kuhifadhiwa tu, bali pia kurithishwa kwa vizazi na vizazi vya karne zijazo za Waswahili na watafiti-watalamidhi wa Kiswahili.

Kutokana na mahojiano yetu na Malenga Nabahan, ndipo tulipobaini kuwa zipo bahari 13 maalum za Ushairi. Bahari hizo ni pamoja na Ushairi, Utenzi, Wimbo, Dura (Mandhuma), Wajiwaji, Hamziya, Utumbuizo, Sama (Mahadhi, Sauti), Ukawafi, Fatiha, Wawe, Kimayo na Zivindo.

Msomi huyo anasema kuwa bahari zote hizo 13 zina malengo na madhumuni yake mahsusi kabisa. "Mathalan, bahari ya Wimbo hutumiwa katika kuwakaribisha na kuwaaga wageni, ama kuwatakia heri maharusi, wakati bahari ya Zivindo hulenga hasa kuhifadhi misamiati ya Kiswahili hasa ile yenye maana zaidi ya moja kama vile kaa, tanga, jua, na mingi mingineyo." Alisema msomi huyo.

Mchango mwingine mkubwa katika lugha ya Kiswahili aliofanya msomi Nabahan ni pamoja na kuanzisha baadhi ya Istilahi maarufu ambazo zimezoeleka mno za Kiswahili. Miongoni mwa istilahi zilizobuniwa na Shekhe Nabahan ni kama vile runinga (televisheni), rununu (simu ya mkononi), barua-pepe (e-mail), pepesi (fax) na kadhalika.

Kulingana na Bw. Nabahan ni kuwa, zaidi ya watu milioni moja kote duniani sasa wanaweza kuwasiliana kikamilifu kupitia lugha ya Kiswahili. Ishara kuwa Kiswahili kinazidi kukua kwa wepesi na kufanyiwa utafiti mno.

"Sasa hivi kuna vyuo vya kujifunzia Kiswahili vipatavyo 35 nchini Marekani pekee, vikitoa nchini Japani, China, Ufaransa, Italia na kwengineko ulimwenguni." Akaongeza Bw. Nabahan kama ithibati ya kukua kwa haraka kwa lugha ya Kiswahili na kusambaa kwa kasi kwa utamaduni wa Mswahili.

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-10