Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-11 16:33:42    
Gu Xiulian, Mwanamke mwenye madaraka makubwa zaidi nchini China

cri

Watu wanasema Bibi Gu Xiulian ni mwanamke mwenye madaraka makubwa zaidi nchini China kutokana na sababu mbili, kwanza, yeye ni naibu spika wa Bunge la umma la China, ambacho ni chombo chenye madaraka ya juu hapa nchini. Na pili ni kiongozi wa Shirikisho kuu la wanawake la China, ambacho ni chombo cha umma kinachoshirikisha wanawake wa hali mbalimbali wa China.

Hivi karibuni Bibi Gu Xiulian alihojiwa na mwandishi wetu wa habari. Siku hiyo alikuwa amevaa suti safi yenye rangi nzito, bibi huyo mwenye nywele fupi na umbo la wastani, alimpa mwandishi wetu sura ya mchapa kazi.

Bibi Gu ameshika nyadhifa kadhaa katika serikali, ambapo aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Jiangsu zaidi ya miaka 20 iliyopita, na baadaye aliteuliwa tena kuwa waziri wa viwanda vya kemikali zaidi ya miaka 10 iliyopita, na sasa ni naibu spika wa Bunge la umma la China na mwenyekiti wa Shirikisho kuu la wanawake la China. Hivi sasa Bibi Gu Xiulian amejikita katika shughuli zinazohusu akina mama na watoto.

Alisema "Serikali ya China inatilia maanani sana shughuli zinazotuhusu sisi wanawake. Imechukua mfululizo wa hatua ambazo zinalenga kuhimiza usawa kati ya wanawake na wanaume na maendeleo ya akina mama, na imepata mafanikio."

Bibi Gu Xiulian aliongeza kuwa, China imejenga mfumo wa sheria zinazolenga kulinda haki na maslahi ya wanawake na kuhimiza maendeleo ya wanawake, ambao katiba ya taifa ni msingi wake na sheria ya kulinda haki na maslahi ya wanawake ndiyo sheria kuu. Mbali na hayo, vyombo vya kulinda akina mama na watoto vimeanzishwa katika asilimia 90 ya miji na wilaya za China, na serikali za ngazi mbalimbali zimetunga mipango ya kuleta maendeleo ya wanawake. Alisema hali hii inaifanya China iongoze katika kazi ya wanawake miongoni mwa nchi zinazoendelea, na China pia ina sifa maalumu ikilinganishwa na nchi zilizoendelea.

Bunge la umma la China ni chombo cha madaraka ya juu hapa nchini, vilevile ni chombo cha juu cha utungaji sheria. Kwa ajili ya kusukuma mbele ukamilishaj wa sheria za kulinda wanawake na watoto, Bibi Gu Xiulian anatembelea mara kwa mara sehemu mbalimbali za China kufanya utafiti. Mjumbe wa Bunge la umma la China Bibi Mo Wenxiu alisema, "Katika kulinda haki na maslahi ya wanawake kwa sheria, Bibi Gu Xiulian ana upeo wa mbali na mtizamo wa kisasa. Kwa mfano, kuhusu kurekebisha sheria ya kulinda haki na maslahi ya wanawake, kuanzia mwaka 2002 yeye mwenyewe alitembelea mikoa mbalimbali kuchunguza hali ya utekelezaji wa sheria hiyo, baadaye alithibitisha kanuni na mwongozo wa marekebisho ya sheria hiyo."

Kuhusu mafanikio yaliyopatikana nchini China katika kutekeleza usawa kati ya wanawake na wanaume, ambayo ni sera ya kimsingi ya taifa, Bibi Gu Xiulian alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hivi leo miongoni mwa kila wafanyakazi 100 katika miji ya China, zaidi ya watu 40 ni wanawake. Lakini akizungumzia hali ya maendeleo ya wanawake na watoto wa sehemu za vijijini, Bibi Gu alieleza maoni yake kuwa, bado kuna mtizamo mzito wa kuwathamini watoto wa kiume zaidi kuliko wa kike katika baadhi ya sehemu za vijijini, ambapo watoto wa kike wanashindwa kupata fursa ya kusoma shuleni kutokana na umaskini, na wanawake wanaoishi katika sehemu zenye uhaba wa maji za magharibi ya China wanakabiliwa na hali duni ya maisha. Hayo yote anayakumbuka moyoni.

Bibi Gu Xiulian anajulikana kama ni mwanamke mwenye tabia ya kujitegemea. Lakini alitoa ombi kwa ajili ya kukusanya fedha za hisani za kujenga "malambo ya maji ya mama", ambayo ni kampeni iliyopendekezwa na Shirikisho kuu la wanawake la China mwaka 2000 ya kujenga malambo ya kukusanya na kuhifadhi maji ya mvua kwa wakulima wanaoishi katika sehemu zenye ukame za magharibi ya China. Katika sehemu hizo, kutokana na upungufu mkubwa wa maji, wanaume wengi wanaondoka makwao kufanya kazi za vibarua, na wanawake na watoto wanabaki vijijini ambapo hali ya maisha na afya ni duni kupita kiasi. Kwa kutumia fedha za hisani kiasi cha Renminbi Yuan elfu 1, inaweza kujenga lambo moja la kukusanya maji ya mvua, na maji hayo yakatosheleza familia ya watu wanne kuishi na kuzalisha.

Katika kipindi cha kukusanya fedha za hisani, Bibi Gu Xiulian alipohudhuria maonesho ya viwanda vya kemikali, aliwaambia viongozi wa viwanda mbalimbali vya kemikali kuwa, "Naomba pesa kwenu, kwa ajili ya kujenga malambo ya maji katika sehemu kame ya magharibi, naomba uungaji mkono wenu." Viongozi hao wa viwanda waliguswa na maneno yake, wakaahidi kufadhili pesa.

Tangu Bibi Gu Xiulian kushika wadhifa wa mwenyekiti wa Shirikisho kuu la wanawake la China, shirikisho hilo limetenda kazi kadhaa zinazowanufaisha wanawake, zikiwa ni pamoja na harakati za kujenga "malambo ya maji ya mama", "treni ya kasi ya afya ya mama" inayotoa huduma za matibabu na dawa bila malipo kwa wanawake wa vijijini, "mradi wa chipukizi" unaowasomesha watoto wa kike kutoka familia maskini, na mradi wa ushirikiano wa kimataifa wa kuwatolea wasichana mafunzo ya kiufundi.

Ofisa wa Shirikisho kuu la wanawake la China Bibi Wang Naikun alieleza kuwa, safari moja walipotembelea Guizhou, mkoa wa kusini magharibi ya China, mzee mlemavu aliyenufaika na harakati ya "malambo ya maji ya mama", machozi yalijaa macho, alimshika mkono wa Bibi Gu Xiulian, akamwambia, "siwezi kukuona, hebu nipapase mkono wako." Baadaye mzee huyo akapiga magoti na kutoa shukrani.

Bibi Gu Xiulian ana mume anayemwunga mkono wakati wote. Mume wake ni mtaalamu wa hisabati. Bibi Gu alieleza kwa furaha kuwa, "Katika familia yangu, mume wangu ni hodari zaidi kuliko mimi katika kupika chakula. Ninamsifu siku zote kuwa yeye ni mpishi wa ngazi ya kwanza katika familia, kwa hiyo naweza kutopika chakula mara kwa mara. Hivi sasa wako wanaume wengi ambao ni hodari wa kupika chakula."

Kabla ya kumuaga, Bibi Gu Xiulian alimsimulia mwandishi wetu wa habari hadithi moja, akisema, mtoto mmoja alikutwa na simba katika jangwa, hakika neno la kwanza analosema ni "Mama nisaidie", hawezi kumtaja baba. Bibi Gu alisema hadhithi hii inatuelezea umuhimu wa wanawake. Aliongeza kuwa, serikali ya China inatilia maanani sana maendeleo ya wanawake, akina mama wanaweza kupata mafanikio makubwa zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-11