Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-11 16:27:32    
Msomi wa Tibet Bw. Puqiong na wanafunzi wake wa kigeni

cri

Mwezi Machi mwaka jana, watu 6 kutoka Japan, Italia, Marekani na Korea ya Kusini waliwasili katika Chuo kikuu cha Tibet, huko Lhasa, mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa Tibet, na kuanza masomo ya fasihi ya lugha ya Kitibet yatakayochukua muda wa miaka miwili. Mwalimu wao ni kijana mwenye umri wa miaka 38, anayeitwa Puqiong Tsering. Wanafunzi hao walifahamu kuwa wana bahati, kwa vile kati ya watu wanaotaka kufundishwa na mwalimu Puqiong, wengi wanaweza tu kushiriki kwenye darasa la masomo la majira ya joto linalokuwepo kwa miezi miwili kati ya mwezi May na mwezi Julai kila mwaka katika Chuo kikuu cha Tibet.

Bw. Puqiong aliyezaliwa mkoani Tibet ni msomi wa utamaduni wa Kitibet mwenye akili nyingi, sasa ni mhadhiri katika kitivo cha lugha ya Kitibet katika Chuo kikuu cha Tibet. Miaka 14 iliyopita, Bw. Puqiong alihitimu kutoka Chuo kikuu cha taifa cha makabila kilichopo Beijing, akapata shahada ya kwanza ya fasihi ya Kitibet. Na miaka 8 iliyopita alikwenda Norway, kuendelea na masomo ya shahada ya pili katika Chuo kikuu cha Oslo, ambapo alifanya utafiti juu ya historia ya dini ya Kibudha ya tawi la Tibet.

Bw. Puqiong alirudi nyumbani mwezi Juni mwaka 2001. Na kuanzia hapo, wanafunzi wengi wa China na wa kigeni walikuwa wanamwomba awe mhadhiri.

Msichana kutoka Finland Bibi Katarina Turpeinen na wanafunzi wa kigeni wengine 20 walishiriki kwenye darasa la majira ya joto mwaka jana. Msichana huyo mwenye umri wa miaka 31 sasa anasomea shahada ya udaktari ya utamaduni wa Kitibet katika Chuo kikuu cha Virginia cha Marekani. Aliona kuwa ili kutimiza ndoto ya kuwa msomi wa utamaduni wa Kitibet, anapaswa kwenda Tibet ambapo kuna mazingira pekee ya lugha na utamaduni yanayosaidia kufanya utafiti unaohusika.

Alisema, "Nilikwenda kusoma huko Tibet kwa lengo la kuinua kiwango cha kuongea lugha ya Kitibet, ili niweze kuongea Kitibet sanifu. Pia navutiwa na utamaduni wa kabila la Watibet na dini ya Kibudha ya Kitibet. Najitahidi kuwa msomi wa taaluma hiyo."

Kwa wanafunzi wa kigeni wenye viwango tofauti vya lugha ya Kitibet, mwalimu Puqiong anazingatia kuinua kiwango cha kusikiliza. Darasani anashikilia kuwafundisha kwa Kitibet, pia anawataka wanafunzi hao wa kigeni waongee kwa Kitibet badala ya Kiingereza. Mbali na hayo, aliwaonesha filamu na vipindi vya televisheni kwa lugha ya Kitibet ili wanafunzi wanaosoma darasa la muda mfupi wawe na mazingira ya kufanya mazoezi ya kuongea na kusikiliza lugha ya Kitibet.

Bibi Katarina alikumbusha kuwa, wakati wa mapumziko alikuwa anazungumza na wenyeji wa kabila la Watibet. Na alipomaliza darasa hilo la miezi miwili, alipata maendeleo makubwa katika kuongea Kitibet.

Katika juhudi za kuwasaidia wanafunzi kuinua kiwango cha Kitibet, mwalimu Puqiong pia aliandaa masomo ya historia na fasihi ya kabila la Watibet, ambayo wanafunzi wanaweza kuchagua kulingana na uwezo wao. Bw. Puqiong alichagua riwaya maarufu iitwayo "Wasifu wa Milarepa na Nyimbo zake" (The Songs and Biography of Milarepa) iliyoandikwa kwa lugha ya Kitibet ya kale kuwa kitabu cha kujifunza. Alifafanua akisema, "Nimeichagua riwaya hiyo kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi waweze kuongeza uwezo wa kusoma na kutafiti lugha ya Kitibet ya kale, na pia kuongeza idadi ya maeneo wanayoyafahamu."

Bw. Zoran Lazovic mwenye umri wa miaka 43 atokaye Yugoslavia ya zamani pia ni mwanafunzi wa Bw. Puqiong. Yeye alivutiwa sana na utamaduni na dini ya Tibet. Alisema "Nilipokuwa na umri wa miaka kati ya 14 na 15, nilisoma riwaya ya Wasifu wa Milarepa na Nyimbo zake kwa tafsiri ya Kiyugoslavia. Milarepa alikuwa mtu maalumu, alikuwa anafanya mambo yanayowanufaisha wengine katika maisha yake. Niliguswa na kuhamasishwa na maadili yake."

Bw. Zoran alianza kujifunza Kitibet miaka 9 iliyopita nchini Marekani. Alieleza kuwa hakuwahi kuongea Kitibet, kwani aliposoma katika chuo kikuu nchini Marekani alifundishwa maneno ya dini ya kibudha yaliyotumika hasa katika lugha ya Kitibet ya kale, ambapo alikuwa hafahamu maneno yanayotumika sana katika maisha ya kila siku kama vile, madirisha, ukuta na barabara. Kwa hiyo alithamini sana nafasi hii ya kusoma huko Tibet.

Alisema, "Tibet tuna nafasi nyingi za kutumia lugha ya Kitibet. Tunaweza kusikiliza vipindi vya Kitibet vya radio, kutazama michezo ya kuigiza ya Kitibet inayooneshwa kwenye televisheni, kusoma magazeti ya Kitibet, pia tunaweza kujifunza sarufi ya lugha ya Kitibet ya kale na ya kisasa."

Mwanafunzi huyo ambaye ni mkubwa kuliko mwalimu wake Puqiong kwa miaka minne alieleza kuwa, amepata ujuzi na urafiki huko Lhasa, kwa vile wakati wa mapumziko mwalimu Puqiong alikuwa ni rafiki wa wanafunzi, ambaye mara kwa mara aliwaongoza wanafunzi kwenda kwenye sehemu ya kitongoji cha mji wa Lhasa yenye mandhari nzuri.

Bw. Gesang Duoji wa ofisi ya ushirikiano na maingiliano ya kimataifa ya Chuo kikuu cha Tibet alisema, katika miaka ya hivi karibuni idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaokuja kusoma katika Chuo kikuu cha Tibet inaongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo mwaka 2004 ilifikia wanafunzi 90.

"Kati ya wanafunzi wa kigeni waliokuja kusoma katika chuo kikuu chetu wengi walikuwa Wamarekani, na wanafunzi kutoka nchi nyingine pia waliongezeka. Kwa mfano hapo awali ilikuwa nadra kuonekana wanafunzi kutoka New Zealand, Afrika Kusini na Uswisi. Lakini sasa wanafunzi wa nchi hizo wameanza kuongezeka."

Idhaa ya kiswahili 2006-05-11