Waziri mkuu wa Uingereza Bw. Tony Blair tarehe 8 kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, iwapo baraza la mawaziri la waziri mkuu mpya Bw. Nouri al-Maliki litakuwa tayari kuchaguliwa, nchi zilizopeleka majeshi nchini Iraq zitajadiliana jukumu la kila nchi, na wakati huo serikali ya Uingereza itapunguza askari wake nchini humo, na kusema kwamba kuhusu jambo hilo serikali ya Uingereza litafanya mpango kamili ndani ya wiki kadhaa. Vyombo vya habari vinaona maneno hayo aliyosema Bw. Tony Blair yanatokana na hali mbaya ya jeshi la Uingereza nchini Iraq na malalamiko ya wananchi wa Uingereza yanayozidi kulaani serikali ya Tony Blair kuingiza Uingereza kwenye vita dhidi ya Iraq.
Kabla ya hapo, tarehe 6 mwezi Mei helikopta moja ya jeshi la Uingereza iliangushwa mjini Basra, kusini mwa Iraq, watu mia kadhaa wa Iraq walifanya maandamano kwenye helikopta hiyo, na mgongano mkali ukatokea kati ya askari wa Uingereza na waandamanaji. Tukio hilo kwa mara nyingine tena limeonesha kwamba ingawa serikali ya Sadaam ilipinduliwa miaka mitatu iliyopita, lakini hali ya usalama nchini Iraq inaendelea kuwa mbaya, kama ilivyo jeshi la Marekani na jeshi la Uingereza pia limezongwa na matatizo mengi, suala la Iraq limekuwa "mzigo" mzito kwa serikali ya Tony Blair. Hivi sasa watu wa Iraq wanakasirika na kupinga kukaliwa na majeshi ya nchi za nje. Gazeti la "Uhuru" la Uingereza lilisema, vita vya Iraq ni "urithi mbaya aliopokea Tony Blair".
Kapteni wa jeshi la nchi kavu la Marekani, Tim Collins, siku chache zilizopita alisema, kuangushwa kwa helikopta hiyo kumedhihirisha masuala mawili kwa pamoja, kwamba uwezo wa kupigana vita wa jeshi la Uingereza umepungua, na zana za kijeshi hazitoshi. Kutokana hali ilivyo sasa, maneno ya kapteni hiyo sio ya kutisha. Hivi sasa kuna masuala matatu yanayolikumba jeshi la Uingereza. Kwanza, zana za kijeshi hazitoshi, hasa baadhi ya zana zinakosa vipuri. Kwa mfano, hivi karibuni vyombo vya habari vya Uingereza vilitangaza kwamba ndege moja kubwa ya mizigo ya Uingereza wakati inafanya kazi kazi yake nchini Iraq tangi lake la mafuta halikuwa na kinga ya moto na mlipuko. Mwezi Januari mwaka jana, ndege nyingine kubwa ya mizigo ilianguka karibu na Baghdad na kusababisha vifo vya askari kumi wa Uingereza. Pili, utunzaji wa zana za kijeshi umesimamishwa, na zana zilizokuwa na dosari haziwezi kupata utunzaji ila tu zinapohatarisha usalama. Tatu, muda wa mafunzo umefupishwa, kwa hiyo uhodari wa askari umekuwa duni, muda wa mazoezi ya baharini kwa jeshi la wanamaji umefupishwa, na hata jeshi la wanaanga ambalo ni fahari ya Uingereza, saa za mazoezi ya kuruka angani pia zinapungua mfululizo.
Wataalamu wanafafanua kwamba sababu za jeshi la Uingereza kuzama katika matatizo ni kupeleka askari wake katika nchi nyingi. Waraka wa wizara ya ulinzi ya Uingereza unaeleza, uwezo wa jeshi la Uingereza, kwa sasa unaweza kupigana vita viwili vikubwa kiasi na vita moja ndogo kwa wakati mmoja. Lakini Bw. Tony Blair hakujali hayo, bali alipeleka na kuongeza askari wake nchini Iraq, Afghanistan na nchi nyingine ili kushirikiana na mkakati wa kivita duniani wa Marekani, matokeo yake uwezo wake wa kijeshi umezidiwa.
Hivi sasa, Tony Blair amelishwa tunda baya. Tarehe 4 mwezi huu, chama chake cha leba kilishindwa katika uchaguzi wa mitaa. Vyombo vya habari vya Uingereza vinaona kwamba ni yeye tu ndiye aliyezamisha jeshi la Uingereza ndani ya matope nchini Iraq na kusababisha kushindwa kwa chama chake. "Usipoziba ufa utajenga ukuta", kutokana na hali ilivyo sasa, Tony Blair anataka kuziba ufa kwa kupunguza askari wake nchini Iraq, lakini je, amechelewa? Tusubiri matokeo.
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-11
|