Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-12 16:41:52    
Ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika waleta faida kwa pande zote

cri

Mwishoni mwa mwaka jana, boma la kuzuia maji la Mailowi lililojengwa na kampuni ya China kwenye mto Nile lilizuia maji kwa mafanikio. Ukiwa mradi mkubwa wa matumizi ya maji, boma la Mailowi bila hakika litawanufaisha wakazi wa huko.

Boma la Mailowi la Sudan lililojengwa na kampuni ya China ni mfano mmoja tu wa miradi ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na nchi za Afrika. ilipofika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka 2005, thamani ya miradi iliyojengwa na makampuni ya China katika nchi za Afrika kutokana na mikataba ilizidi dola za kimarekani bilioni 38.7. Mwaka 2005, thamani ya biashara kati ya China na nchi za Afrika pia iliongezeka kufikia dola za kimarekani bilioni 40, na ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika unaendelea kwa kasi na kwa njia mbalimbali.

Mwandishi wetu wa habari alipowatembelea baadhi ya wakazi wa huko Kenya, alioneshwa bidhaa zilizotengenezwa nchini China. Bidhaa za China zenye sifa bora na bei rahisi zinapendwa sana na watu wa Afrika. Mkuu wa benki ya maendeleo ya Afrika Bw. Donald Kaberuka alisema kuwa, hivi sasa nchi za Afrika bado zinakosa uwezo wa kuzalisha bidhaa za viwandani, hivyo kuna fursa nyingi za kufanya ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika.

Nchini Kenya, inasimuliwa hadithi moja kuhusu dawa za kichina. Mwaka 1994, mjamzito mmoja aliyekuwa na tatizo la mimba kuharibika mara kwa mara kutokana na kuugua malaria, baada ya kutumia dawa za kichina za kutibu ugonjwa huo ziitwazo "Cotecxin", si kama tu alinusurika mwenyewe, bali pia alifaulu kuzaa mtoto. Alifurahi sana, akaamua kumpa mtoto wake jina la "Cotecxin", ili kukumbuka daima fadhili ya China.

Bwana Luo Xunwen aliyefanya kazi kwa miaka mingi nchini Kenya alisema kuwa, tangu kampuni ya ujenzi wa barabara na daraja ya China kuingia nchini Kenya mwaka 1985, imekamilisha miradi 11 ya kimkataba, kutimiza thamani ya dola za kimarekani milioni 200 ya kimkataba, kampuni hiyo imesifiwa sana na watu wa Afrika kutokana na kukamilisha miradi kwa wakati na kwa sifa bora, na bila kuzidi bajeti iliyowekwa.

Makampuni ya China kuwekeza katika nchi za Afrika si kama tu yameleta ajira mpya na kuongeza mapato kwa nchi husika, bali pia yamesaidia kuingiza teknolojia mwafaka kwa nchi za Afrika, kuwaandaa watu wengi wenye ustadi maalum, kuinua uwezo wa uzalishaji wa nchi za Afrika, na kuhimiza maendeleo ya pamoja ya China na nchi mbalimbali za Afrika. Mwezi Mei mwaka jana, kampuni moja ya Beijing iliwekeza dola za kimarekani milioni 3.04 kuanzisha kiwanda cha kutengeneza nguzo za saruji za waya wa umeme na simu nchini Kenya na kufungua ukurasa mpya katika historia ya nchi za Afrika mashariki iliyotumia tu nguzo za miti. Imefahamika kuwa, kampuni hiyo inapanga kuanzisha miradi mingi zaidi itakayoleta mambo ya kisasa katika sekta ya matumizi ya umeme katika Afrika mashariki, ili kuzisaidia nchi za Afrika zitokomeze tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Chini ya uungaji mkono wa serikali ya China, kampuni ya mawasiliano ya simu ya Huawei mwaka 2005 kwa nyakati tofauti ilisaini mikataba yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 44.2 na nchi tatu za Kenya, Zimbabwe na Nigeria, na kuzisaidia nchi hizo kuboresha vifaa vya mawasiliano ya simu. Kampuni hiyo pia imewekeza dola za kimarekani zaidi ya milioni 7 nchini Nigeria kujenga kituo cha mafunzo, ambacho kimeisadia Nigeria kuwaandaa mafundi wengi wa sekta ya mawasiliano ya simu.

Msemaji wa serikali ya Kenya alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, serikali ya Kenya inatilia maanani kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na China. Uwekezaji wa makampuni ya China si kama tu umeleta nafasi nyingi za ajira, bali pia umehimiza maendeleo ya uchumi wa huko. Makampuni ya China yamekuwa na sifa kubwa katika nchi za Afrika, na serikali ya China kamwe haihusishi misaada na shughuli za kiuchumi na mambo ya kisiasa.

Meneja mkuu wa kampuni ya Afrika ya Zhongyuan Bwana Lin Qing alisema, tokea mwaka 1994, kampuni hiyo ilikuwa imeifanya bandari ya Durbon, Afrika Kusini kuwa kituo chake cha kimsingi, na kuanzisha njia nyingi baharini za kusafirisha makontena kuelekea nchi mbalimbali za Afrika, kampuni hiyo inashughulikia hasa usafirishaji wa madini, mbao za Afrika zinazosafirishwa nje na zana za ujenzi na bidhaa nyingine zinazoagizwa kutoka nje, biashara ya kampuni hiyo inaongezeka mwaka hadi mwaka. Bw. Lin alisema kuwa, kutokana na ongezeko la kasi la biashara kati ya China na nchi za Afrika, na kuongezeka kwa miradi ya ujenzi, mahitaji ya uchukuzi katika nchi mbalimbali za Afrika yanaongezeka siku hadi siku.

Kwa ujumla, China na nchi za Afrika zina uwezo mkubwa wa kushirikiana kiuchumi, China itaendelea kukuza uhusiano mpya wa kimkakati na kiwenzi na nchi za Afrika ulio na usawa na kuaminiana, kushirikiana na kunufaishana ili kuhimiza ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika uendelezwe zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-12