Baada ya nchi tano za kudumu za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani kushindwa kuafikiana pendekezo la Uingereza na Ufaransa la kuchukua hatua kali dhidi ya Iran, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi.Condoleezza Rice hivi karibuni amesema, Umoja wa Ulaya utaanza tena juhudi za mazungumzo ya kidiplomasia kuhusu utatuzi wa suala hilo na utatoa mlolongo wa mapendekezo ndani ya wiki moja au mbili, na kabla ya hapo, Marekani na Umoja wa Ulaya zitaweka kando azimio lao ambalo linataka kupitishwa katika Baraza la Usalama. Wachambuzi wanaona kuwa hali hii inamaanisha kwamba suala la nyuklia la Iran limeingia katika kipindi kipya cha mazungumzo ya kidiplomasia.
Bi. Condoleezza Rice alisema, mlolongo wa mapendekezo yataipa Iran machaguo ya aina mbili: ama Iran iendelee kwenda kinyume na matumaini ya jumuyia ya kimataifa na kukabiliwa na hali ya kutengwa na hatua zitakazochukuliwa na Baraza la Usalama; au ishike njia ya mpango wa kinyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia, njia ambayo inakubaliwa na jumuyia ya kimataifa.
Ukweli ni kwamba, kwa kukabiliwa na shinikizo kubwa, rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran ameanza mapema juhudi zake za kidiplomasia. Kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tano za kudumu za Baraza la Usalama pamoja na Ujerumani kufanyika tarehe 8 huko New York kuhusu suala la nyuklia la Iran, ghafla Iran ilitangaza kuwa rais Mahmoud Ahmadinejad amemwandikia barua rais Bush wa Marekani na kutoa mapendekezo yake kuhusu namna ya kutatua masuala ya kimataifa na kupunguza hali ya wasiwasi duniani. Sambamba na hayo, katibu wa kamati kuu ya usalama ya Iran Bw. Ali Larijani alifanya ziara nchini Uturuki na Ugiriki tarehe 8 na 9 mwezi huu, nchi ambazo ni marafiki wa Marekani katika jumuyia ya Nato. Kisha rais Mahmoud Ahmadinejad alifanya ziara rasmi nchini Indonesia. Wachambuzi wanaona kwamba shughuli hizo za kidiplomasia za Iran ni kwa ajili ya kutafuta uungwaji mkono na kupata maelewano katika jumuyia ya kimataifa, na barua ya rais Mahamoud Ahmadinejad kwa Bw. Bush imedhihirisha wazi zaidi kwamba Iran inataka kulishawishi Baraza la Usalama lisichukue hatua kali dhidi yake.
Wachambuzi wanaona kwamba, kwa kukabiliwa na shughuli zote hizo za kidiplomasia za Iran, Marekani, nchi ambayo inahusika moja kwa moja na suala la nyuklia la Iran, inaishiwa na ujanja. Habari zinasema, barua ya rais Mahmoud Ahmadinejad yenye kurasa 18 haikutaja hata kidogo suala la nyuklia la Iran, bali ilieleza kirefu makosa ya sera za kidiplomasia za Marekani zikiwa ni pamoja na dini, historia na uhusiano wa kimataifa. Msemaji wa ikulu ya Marekani alisema, barua hiyo haikutoa mapendekezo yoyote ya maana kuhusu namna ya kupunguza wasiwasi wa jumuyia ya kimataifa juu ya suala la nyuklia la Iran. Wanasema, mbele ya Iran, nchi ambayo inakubali tu "karoti" wala sio "fimbo", kama Marekani haitakuwa na ushawishi mkubwa zaidi kuliko Iran katika diplomasia, matumaini yake ya kuiadhibu Iran kwa kutegemea Baraza la Usalama yatakuwa bure.
Kadhalika, wachambuzi pia wanaona mustakbali wa mazungumzo ya kipindi kipya kuhusu suala la nyuklia la Iran pia ni kitandawili. Tarehe 11 mwezi huu rais Mahmoud Ahmadinejad kwenye ziara yake nchini Indonesia alisema, "nchi fulani za Magharibi zinatumia vigezo viwili tofauti katika suala la nyuklia" na alishutumu "Baadhi ya mataifa makubwa yanafanya ukiritimba wa teknolojia na sayansi na kujaribu kutawala mataifa mengine." Kwa hiyo msimamo wa Iran bado ni mgumu. Wachambuzi wamesema, katika muda wa mwezi mmoja au miezi miwili ijayo, Umoja wa Ulaya utafanya juhudi gani za kidiplomasia na utatoa mlolongo wa mapendekezo gani ambayo yanaweza kukubaliwa na pande zote mbili, Marekani na Iran, huo utakuwa ni mtihani mkubwa wa kiakili kwa Umoja wa Ulaya katika uwezo wa kidiplomasia.
Hivi sasa, nchi zilizo nyingi zinaunga mkono kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia. Na mpaka sasa Marekani haijasema kama lazima itachukua hatua za kijeshi. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice tarehe 10 mwezi huu alisema, ingawa barua ya Mahmoud Ahmadinejad haikutoa mapendekezo yoyote mapya, lakini kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia bado ni chaguo la kwanza. Sambamba na hayo, Iran pia haijaacha nia ya kufanya mazungumzo. Tarehe 11 mwezi huu Ahmadinejad alisema, mpango wa nyuklia wa Iran haulengi silaha za kijeshi, na kwamba Iran iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani na nchi za Magharibi ili kuondoa mzozo katika suala hilo la nyuklia.
Ni dhahiri kwamba mazungumzo hayatakuwa shwari, migongano ya kidiplomasia kati ya pande mbili hakika itaendelea. Suala la nyuklia la Iran litatatuliwaje? Tutafuatilia.
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-12
|