Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-15 15:30:27    
Mhifadhi wa utamaduni wa jadi wa China Bw. Feng Jicai

cri

Bw. Feng Jicai ni mwandishi wa vitabu na mchoraji mashuhuri nchini China. Katika miaka ya karibuni, kwa moyo wote anajishughulisha na kazi ya kuokoa na kuhifadhi utamaduni wa jadi unaokaribia kutoweka na ameanzisha "mradi wa kuhifadhi utamaduni wa jadi wa China". Juhudi zake zinaungwa mkono na sekta mbalimbali za jamii, watu wanamsifu kuwa ni "mhifadhi wa utamaduni wa jadi wa China".

Bw. Feng Jicai sio tu ni mwandishi wa vitabu, mchoraji, lakini pia ni mtu anayethamini sana utamaduni wa jadi wa China.

Bw. Feng Jicai alizaliwa mwaka 1942 katika mji wa Tianjin, mji uliopo karibu na Beijing. Alipokuwa mtoto alipenda sana uchoraji, fasihi, muziki na mpira wa kikapu. Baada ya kuhitimu sekondari alichaguliwa kuwa mchezaji wa mpira wa kikapu kwa sababu ya urefu wake mkubwa. Lakini muda si mrefu aliachana na timu hiyo kutokana na kuumia. Hatimaye alipata kazi ya kuchora picha kwa kuiga picha za kale za China katika shirika moja la picha mjini Tianjin, licha ya kuiga pia alichora picha nyingi zenye mtido wa uchoraji wa Kichina na wa Kimagharibi. Katika kipindi hicho Feng Jicai alishikwa na upendo mkubwa na sanaa za jadi, mila na desturi. Katika miaka ya sabini ya karne iliyopita, Bw. Feng Jicai alianza kushughulika na maandishi na amekuwa mwandishi mashuhuri wa vitabu nchini China. Kati ya maandishi yake, yaliyo mengi yanaeleza maisha ya wasomi na riwaya za historia. Maandishi yake yanasomwa sana kwa kuwa na elimu nyingi za utamaduni wa mila na desturi za Wachina, na yametafsiriwa kwa Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kijapan na Kirusi, zaidi ya maandishi 30 yalichapishwa katika nchi za nje.

Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, China imeingia katika kipindi cha maendeleo ya haraka, utamaduni wa China wenye historia ndefu umekabiliwa na changamoto kubwa. Katika miaka ambapo watu wengi walikuwa hawajaona hatari ya kutoweka kwa utamaduni wa jadi Bw. Feng Jicai alikuwa amenusa harufu ya hatari hiyo na kuitahadharisha jamii, alisema, "Hivi sasa utamaduni wetu wa jadi wenye thamani kubwa umekuwa ukimomonyoka wakati wananchi wanapokimbilia maisha ya aina mpya. Mwaka 1994 nilipata habari kutoka gazeti moja likisema kwamba majengo yote ya zamani mjini Tianjin yatabomolewa na badala yake yatajengwa majengo ya kisasa. Mji wa Tianjin umekuwa na miaka 600, majengo ya zamani ni makumbusho ya historia ya mji huo. Wakati huo kwa pesa zangu za uchapishaji wa vitabu niliwaalika wanahistoria, wasanifu wa majengo, wapiga picha zaidi ya sabini wafanye ukaguzi na kupiga picha kote mjini ili kubakiza kumbukumbu za mji huo. Tokea hapo nimedhamiria kuokoa utamaduni wetu."

Bw. Feng Jicai na wataalamu hao walifanya ukaguzi na kupiga picha kwenye kila barabara na kichochoro. Katika muda wa nusu mwaka hivi walipiga picha zaidi ya elfu 30 na kuchapisha vitabu vinne vya picha hizo kwa jina la "Mji Unaopenda". Kutokana na juhudi zao, majengo mengi yamebakizwa.

Tokea hapo Bw. Feng Jicai amezama katika shughuli za kuokoa na kuhifadhi utamaduni wa jadi. Kwa msisimko aliandika makala nyingi za kuomba jamii ihifadhi urithi wa utamaduni ukiwemo utamaduni wa jadi wa opera, uchoraji na picha za karatasi za kukatwa, mila ya sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina, kwa sababu utamaduni huo umekuwa ukiyeyuka pole pole. Bw. Feng Jicai anaona kuwa hifadhi hiyo inatokana na upendo wake wa utamduni wa jadi, na kusema fikra sahihi kuhusu utamaduni huo ndio msukumo wa juhudi zake.

Mwaka 2001 wakati Bw. Feng Jicai akiwa mwenyekiti wa Shirikisho la Wasanii wa Sanaa za Jadi za China alifanya uchunguzi kila sehemu nchini China. Feng Jicai, mtu wa kupenda kuongea akawa kimya kwa kuwa na moyo mzito baada ya kuona hali ya utamaduni wa jadi ulivyopotea. Alieleza hali hiyo kwa mfano, kwamba sehemu ya Yangjiabu mkoani Shandong hapo zamani ilikuwa ni sehemu muhimu ya kuchora na kuchapisha picha za jadi za mwaka mpya wa Kichina, hivi sasa uchoraji wa picha za aina hiyo umekuwa na mrithi mmoja tu. Sanaa ya jadi ya Kichina imekaribia kutoweka kabisa. Alisema, "Utamaduni wetu wa jadi unategemea warithi wa kizazi hadi kizazi wakiwemo waimbaji, wanamuziki na wasimulizi wa fasihi, watu hao wenye sanaa za aina mbalimbali za jadi wakitoweka utamatuni wa jadi utakwisha."

Mwaka 2003 kwa kusukumwa na Feng Jicai, Shirikisho la Wasanii wa Utamaduni wa Jadi lilianzisha mradi wa miaka 10 wa kuokoa utamaduni wa jadi kwa kufanya uchunguzi, kurekodi, kuratibu na kuchapisha vitabu. Lakini kutokana na uhaba wa fedha, ilimpasa Feng Jicai afanye kazi mchana na kuchora picha usiku na kuziuza, alifanya hivyo kwa miezi kumi mfululizo, mwishowe alianzisha mfuko wa hifadhi ya utamaduni wa jadi kwa pesa alizopata kutoka mauzo ya picha zake. Kwa sababu ya uchovu mkubwa wa kuchora picha kiwiko cha mkono wake wa kulia kimevimba.

Juhudi za Feng Jicai na wenzake bila kulegea zilivutia vyombo vya habari na zimepata uungaji mkono kutoka kwa serikali na raia wengi wa kawaida, matokeo yake yakawa mradi huo wa kuokoa utamaduni wa jadi umeorodheshwa katika mfuko wa taifa wa sayansi ya jamii hata serikali imeamua kila J'mosi ya pili ya mwezi Juni iwe "siku ya urithi wa utamaduni" nchini China.

Katika kipindi cha miaka zaidi ya kumi Feng Jicai amekuwa "mhifadhi wa utamaduni wa jadi". Alisema kwa masikitiko kuwa tumaini lake ni kuandika riwaya, lakini shughuli za kuhifadhi utamaduni wa jadi zilimnyima wakati asiweze kuandika, na mbele ya hatari ya kumomonyoka kwa utamaduni wa jadi hana chaguo lingine ila kuhifadhi. Alisema, "Utamaduni wa taifa ni kitu muhimu kuliko chochote kingine. Utamaduni ni mali zetu tulizolimbikiza kwa miaka mingi na unaendelea na uhai wake kwa kurithisha vizazi vya baadaye. Bila ya kubakiza utamaduni wetu sisi wenyewe tutapotea."

Idhaa ya kiswahili 2006-05-15