Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-15 20:05:53    
Mwongo mmoja baada ya mauaji ya halaiki, Rwanda yaanza mkakati kabambe wa kuvutia idadi kubwa ya watalii

cri

Ni miaka 12 imepita sasa tangu kumalizika kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyosababisha vifo vya watu wengi nchini Rwanda, vita ambavyo vilidumu kwa muda wa siku 100.

Vita hivyo vilivyohusisha makabila ya wahutu na watutsi vilitokea mwaka wa 1994, na kusababisha mauaji ya kinyama ya watutsi wapatao laki 8, ambao ndio kabila lenye watu wachache nchini humo. Aidha, mauaji hayo ya kinyama pia yaliwakumba baadhi ya wahutu walioonesha kuwaonea huruma watutsi, wakikatwa katwa kwa mapanga na silaha nyinginezo hatari. Hivi sasa Rwanda iko mbioni kujikwamua kutokana na umaskini na shida nyingine ambazo zinawakumba wananchi, hasa baada ya kipindi cha vita.

Ugumu huo wa maisha hasa katika nchi kama Rwanda ambayo imeathiriwa na maafa ya vita vya kikabila, unaongezwa na tatizo la uhaba wa ajira linaloletwa na kurudi nyumbani kwa raia waliokimbilia katika nchi za kigeni. Hata hivyo, Rwanda imevumbua mbinu nyingine mwafaka ya kuongeza pato la fedha za kigeni. Njia hiyo ni kuendeleza sekta ya utalii.

Rwanda kama mataifa kadhaa barani Afrika, imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii. Miongoni mwa sehemu hizo zenye kuwavutia watalii ni pamoja na ziwa Ihema lililoko katika bustani ya Akagera. Ziwa hilo lina bwawa moja la aina yake ambalo si kama tu linawavutia watalii, bali pia wanyama kama ndovu, ambao pia ni kivutio kingine kwa watalii.

Kadhalika, Rwanda inajivunia kuwa na vivutio vingine vya utalii ikiwemo milima. Mandhari ya Rwanda inavutia sana ikizingatiwa kuwa hali ya hewa nchini humo huwa ya fufutende. Kwa maana hii ni kuwa hakuna joto kali wala baridi kali kupita kiasi nchini humo. Pamoja na maziwa yenye mandhari ya kupendeza, Rwanda pia inajivunia kuwa na mbuga za wanyama kama punda milia, twiga na ndovu.

Mbuga za Nyungwe na Volcanoes zimeanza kuwavutia watalii wengi, hasa wale wanaotaka kuangalia sokwe na nyani. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa ofisi ya Utalii na Mbuga za wanyama za taifa, nchini humo Rosette Rugamba, sasa kiasi kikubwa cha fedha kinatumika katika kuvitangaza vituo vya utalii vilivyoko nchini Rwanda.

Mkurugenzi huyo amesema, hivi sasa wanafanya juhudi kuutangazia ulimwengu kuwa Rwanda ya sasa ni tofauti kabisa na Rwanda ya zamani iliyokumbwa na mapigano ya kikabila. Kwa sasa wanalenga siku za usoni na kuipa nchi yao sura mpya kabisa.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa watalii watakaotembelea mbuga za kitaifa za nchi hiyo, hawatafurahia tu kuwaona wanyama wa mbugani, bali pia watatumbuizwa kwa utamaduni na ngoma za kienyeji, na kufurahia hewa safi.

Mamia ya watalii huiingizia Rwanda zaidi ya dola za kimarekani milioni 300 kwa kila mwezi, na hivyo kuinua kwa kiasi kikubwa uchumi wa taifa hilo. Mwaka jana pekee, mbuga za wanyama za Rwanda zilishuhudia kiasi cha watalii wapatao elfu 50 kutoka nchi za nje, na wengine wakiwa watalii wenyeji, yaani wanyarwanda wenyewe wakitembelea nchi yao na kufurahia mandhari yao.

Takwimu za utalii nchini Rwanda zinaonesha kuwa idadi kubwa ya watalii kuwahi kuitembelea nchi hiyo ilikuwa mwaka 1989, kabla ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Wakati huo watalii wapatao elfu 23 waliitembelea Rwanda.

Hivi sasa dalili za kukua kwa sekta ya utalii nchini Rwanda zimeanza kuonekana. Kwa mujibu wa taarifa ya Bwana Rugamba, mwaka jana pekee, utalii wa Rwanda ulikuwa kwa asilimia 18, wengi wa watalii walitoka katika mabara ya Amerika na Ulaya.

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-15