Tarehe 15 mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya walifanya mkutano huko Brussels na kujadili mapendekezo mapya ya nchi tatu Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la Iran. Ingawa mapendekezo hayo bado hayajatangazwa, lakini imefahamika kuwa yana ushawishi mkubwa kiasi ambacho Iran itakuwa vigumu hata kwa Iran kukataa.
Wakati wa mkutano huo, mjumbe mwandamizi wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya nje na usalama Bw. Javier Solana alizungumza na wajumbe wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani peke yao, kisha kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, mapendekezo hayo "yamezingatia pande nyingi zaidi na yana ukarimu mkubwa zaidi" kuliko mapendekezo yaliyotolewa mwezi Agosti mwaka jana, ikiwemo ruhusa ya Umoja wa Ulaya kuisaidia Iran kupata teknolojia ya kisasa kabisa ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Habari zinasema, mapendekezo hayo yatakamilishwa kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kufanyika tarehe 19 na kuyakabidhi kwa Iran mwishoni mwa mwezi huu.
Katika siku hiyo, mkutano wa mawaziri wa nchi 25 za Umoja wa Ulaya pia walipitisha azimio likisema kwamba, iwapo Iran itachukua hatua za kuondoa wasiwasi jumuyia ya kimataifa, Umoja wa Ulaya ungependa kuunga mkono Iran kuendeleza mpango wake wa nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia kwenye msingi wa mapendekezo yaliyotolewa mwezi Agosti mwaka jana. Pamoja na hayo, Umoja wa Ulaya utaendelea kutafuta njia ya kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo na kuendeleza uhusiano kati yake na Iran kwa msingi wa kuaminiana na ushirikiano. Azimio hilo pia lilisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Iran na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na kusimamisha shughuli za kusafisha uranium, na kusema kwamba hili ni sharti kabla ya kurudisha mazungumzo ya suala la nyuklia.
Maneno ya Javier Solana na azimio la mkutano wa mawaziri wa nchi za Umoja wa Ulaya, yote yamehakikisha haki ya Iran ya kutumia nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia katika msingi wa "mkataba wa kutoenza silaha za nyuklia", lakini yamesisitiza kwamba mpango wa nyuklia lazima uwe wazi. Bw. Solana alisema, hawapingi Iran kuwa na uwezo wa kuzalisha nyuklia kwa lengo tu la mtumizi ya kiraia na kushirikiana nayo. Lakini shughuli za kusafisha uranium hata kwa lengo la utafiti pia hawatakubali.
Lakini kutokana na jinsi Iran ilivyoonekana hivi karibuni, mapendekezo ya Umoja wa Ulaya pengine hayatakubaliwa na Iran. Wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ulipofanyika, waziri wa mambo ya nje wa Iran Manouchehr Mottaki huko Tehran aliwaambia mabalozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwamba matakwa yoyote ya kuitaka Iran isimamishe shughuli za kusafisha uranium hayatakuwa ya haki na yatakataliwa katakata na Iran. Siku moja kabla ya hapo, rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran alisema, Iran inakataa mapendekezo yoyote yanayotaka Iran isimamishe shughuli za kusafisha uranium.
Kwa mujibu wa hali ilivyo sasa, kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya amani ni njia inayokubaliwa na jumuyia ya kimataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan anayefanya ziara nchini Korea ya Kusini, tarehe 15 huko Seoul alisema, Umoja wa Ulaya una imani na kipindi kipya cha mazungumzo ya kidiplomasia, na kwa mara nyingine tena ametoa wito kwa pande mbalimbali zichukue hatua za kupunguza mgogoro. Wachambuzi wanaona kwamba hivi sasa suala la nyuklia la Iran pia lina uwezekano wa kutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia, lakini si rahisi kuzipatanisha pande zote. Je, mapendekezo ya Umoja wa Ulaya yatakayotolewa yatapokelewa na pande mbalimbali, hasa Iran na Marekani? Hatima yake inaathiri moja kwa moja ufanisi wa kipindi kipya cha juhudi za kideplomasia.
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-16
|