Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-16 18:26:23    
Shindano la chemsha bongo la "Mimi na Radio China Kimataifa"

cri

Makala ya kwanza: Kumbukumbu za kihistoria?Kipindi cha mwanzo tangu Radio China kimataifa ianzishwe

Wasikilizaji wapendwa, mwaka huu ni mwaka wa 65 tangu Radio China kimataifa ianzishwe. Ikiwa radio pekee ya taifa la China inayotangaza kwa nchi za nje, Je, Radio China kimataifa ilianzishwa kwa namna gani? Ilipitia njia gani ya maendeleo?

Kabla ya kusikiliza makala hii, tafadhali sikilizeni maswali mawili: La kwanza, Je, mtangazaji wa kwanza wa Radio China kimataifa jina lake ni nani? Swali la pili: Mwezi Aprili mwaka 1950, radio ya China ilipoanza kurusha matangazo yake kwa nchi za nje ilijulikana kwa jina gani?

Mwanzoni mwa miaka ya 40 ya karne iliyopita ya 20, China ilikuwa iko katika kipindi cha kupambana na uvamizi wa kijeshi wa Japan, ambapo chama cha kikomunisti cha China na jeshi lililoongozwa na chama hicho vilikuwa uti wa mgongo katika mapambano dhidi ya uvamizi wa Japan. Ili kufahamisha mapambano yaliyofanywa na wananchi wa China dhidi ya uvamizi wa Japan, Chama cha kikomunisti cha China kilianzisha Radio ya Xinhua huko Yanan, kaskazini magharibi ya China, ambapo ndipo kulipokuwa makao makuu ya Kamati kuu ya Chama cha kikomunisti cha China. Radio hiyo ilieleza hali ya nchini China na duniani ya wakati huo, na kuwaita watu wa sekta mbalimbali za jamii ya China na jumuia ya kimataifa kupambana kwa pamoja na uvamizi wa Japan. Tarehe 3 Desemba mwaka 1941, Radio hiyo ya China ilipotangaza kwa mara ya kwanza kwa lugha ya kipajan, ilijulikana kwa jina la XNCR, ambapo iliwalenga askari wa jeshi la uvamizi la Japan waliokuwa nchini China, na mtangazaji wa kwanza wa radio hiyo ya China alikuwa mpiganaji wa kike wa Japan aliyepinga vita, jina lake ni Hara Kiyoshi. Ingawa wakati huo studio ya radio hiyo ilikuwa ndani ya pango lenye hali duni, hata uwezo wa mitambo ya kurusha matangazo ulikuwa volt 300 tu, lakini kuanzia siku hiyo China ilianza kurusha matangazo ya lugha ya kigeni kwa watu wa nchi za nje. Baadaye, tarehe 3 Desemba mwaka 1941 ilithibitishwa kuwa siku ya kuanzishwa kwa matangazo ya China kwa nchi za nje.

Bwana Lu Rufu aliyeishi Japan na kurudi nyumbani China katika miaka ya 50 ya karne iliyopita, alifanya kazi kwa miaka mingi katika Idhaa ya kijapan ya Radio China kimataifa. Naye alielewa zaidi hali kuhusu Idhaa ya Kijapan iliyoanzisha matangazo yake kwa Japan. Bwana Lu mwenye umri wa miaka 70 mwaka huu alisema, mtangazaji huyo Bibi Hara Kiyoshi alitangaza ndani ya pango la Yanan, matangazo yake yalikuwa kama silaha kubwa ya kusambaratisha askari wa jeshi la Japan katika mapambano yaliyofanywa na wachina dhidi ya uvamizi wa kijeshi wa Japan. Bwana Lu akisema:

Mtangazaji huyo alitumia sauti yake kuwaambia wajapan ukweli wa mambo wa vita ya uvamizi, na kuwaambia kuwa upande gani ulifanya mapambano ya haki. Matangazo yake yaliwasaidikisha watu wengi. Katika Idhaa ya Kijapan ya Radio China kimataifa, wataalamu wengi waliofanya kazi pamoja na mimi walikuwa askari wa jeshi la Japan. Baadhi yao walisalimu amri katika vita, halafu walibaki China kufanya kazi, wengine walifika idara yetu bila kuaga katika jeshi lao. Mwalimu wangu aitwaye Michiyuki Ogi alikuwa askari mmoja wa jeshi la Japan, lakini badaye alifanya kazi kwa miaka mingi katika idhaa yetu ya kijapan.

Mwaka 1946 baada ya kupata ushindi katika mapambano dhidi ya uvamizi wa Japan, chama cha Guomintang kilichowahi kufanya ushirikiano an chama cha kikomunisti cha China katika vita dhidi ya uvamizi wa Japan, kilikataa kuunda serikali ya muungano, na kilifanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya chama cha kikomunisti cha China, kikijaribu kuanzisha serikali ya kidikteta, ambapo chama cha kikomunisti cha China kiliwaongoza wananchi kuanzisha mapambano ya kujipatia ukombozi wa kidemokrasia. Kutokana na maendeleo ya hali ya vita, mwanzoni mwa mwaka 1947, Radio Xinhua ya Yanan ilihamia Wilaya ya She mkoani Hebei ambayo ni ipo karibu sana na Beijing. Mwezi Septemba mwaka huo, Radio Xinhua ya Yanan ilianzisha matangazo yake ya kiingereza. Na mtangazaji wa kwanza wa kiingereza alikuwa Bibi Wei Lin ambaye ana umri wa miaka 82 mwaka huu. Alipokumbusha hali ya mwaka ule, mzee Wei alisema:

Mwaka ule studio yetu ilikuwa katika pango moja lililoko kusini mwa kijiji cha Shahe wilayani She mkoani Hebei, zana za studio yetu zilikuwa za hali duni, hata mlango wa studio yetu ulikuwa pazia moja la sufi lililotengenezwa na wenyeji wa huko, hivyo wakati fulani tulipotangaza hata sauti ya wachungaji na milio ya kondoo nje ya mlango zilisikika kwenye matangazo yetu. Wakati huo tulikuwa hatuna chombo cha kurekodi muziki, tulipotaka kuwaburudisha wasikilizaji wetu kwa nyimbo, tulikialika kikundi cha nyimbo na muziki kije studioni kuimba nyimbo moja kwa moja.

Matangazo ya kiingereza yaliporushwa hewani, uwezo wa kurusha matangazo ya Radio Xinhua ya Yanan ulifikia kilowati 10, ambapo nchi za Asia ya kusini na Asia ya kusini mashariki zilikuwa zimeweza kupata usikivu mzuri wa matangazo ya Radio Xinhua ya Yanan, katika hali mwafaka ya hewa, hata sehemu za Ulaya, na Amerika ya kaskazini ziliweza kusikia matangazo ya radio hiyo ya China, ambapo watu wengi wa nchi za nje walipata habari halisi kuhusu hali ya China wakati huo.

Wasikilizaji wapendwa, Jamhuri ya watu wa China ilizaliwa Mwaka 1949, ambapo Radio Xihua ya Yanan ilihamia mji mkuu Beijing, na kubadilika jina kuwa Radio Xinhua ya Beijing. Uliyosikia sasa hivi ni sauti ya Radio ya Xinhua Beijing wakati ilipotangaza moja kwa moja sherehe ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya watu wa China.

Baada ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya watu wa China, Radio ya China ilifanya juhudi za kujulisha siasa na sera za serikali ya China na mabadiliko yaliyotokea katika maendeleo ya siasa, uchumi na jamii nchini China, pamoja na mawasiliano na ushirikiano kati ya China na nchi mbalimbali duniani, radio hiyo imekuwa daraja la kuongeza maelewano na urafiki kati ya wananchi wa China na wananchi wa nchi mbalimbali duniani. Katika mchakato wa kutekeleza jukumu lake, matangazo ya China kwa nchi za nje yalipata maendeleo makubwa zaidi, hasa yalianza kutangaza kwa lugha mbalimbali kwenye msingi wa lugha tatu tu za kichina, kijapan na kiingereza.

Mwezi Aprili mwaka 1950, Radio Peking ilikuwa jina rasmi ya radio China iliyotangaza kwa nchi za nje, mliosikia ni muziki wa uanzilishi wa matangazo ya radio hiyo, muziki huo ni wimbo uitwao "Mashariki kwekundu" uliojulikana sana nchini China, takriban kila mchina alijua kuimba wimbo huo. Mwezi Aprili mwaka 1950, Radio Peking ilianza kutangaza kwa lugha za kivetnam, kithalend, kindonesia na kimyamar ikiwajulisha watu wa sehemu ya Asia ya kusini mashariki sera ya kidiplomasia ya amani ya China iliyo ya kujitawala na kujiamulia, kuwajulishia watu wa nchi za sehemu hiyo uzoefu wa mapinduzi ya China na kuwaongeza nia ya kujipatia uhuru wa kitaifa.

Kutokana na upendo walio nao kwa China mpya, wachina wengi walioishi katika nchi za nje walirudi nchini China kuishi na kufanya kazi. Bwana Wang Shanzhong mmoja wa watu hao ambaye alishiriki kazi ya maandalizi ya matangazo ya lugha ya Myanmar ya mwaka ule. Alikumbusha kuwa, wakati walipoanzisha matangazo ya lugha ya kimyanmar, hali ya ofisi ilikuwa ya duni, lakini alipata furaha kwenye kazi yake. Bwana Wang alikumbuka kuwa, aliwahi kutangaza makala moja iliyosimulia hadithi kuhusu jinsi wakulima walivyopambana na unyonyaji wa wamiliki mashamba, na makala hiyo ilipotangazwa iliambatana na sauti ya milio ya kuku na mbwa, sauti hiyo ilisimuliwa na mtangazake peke yake. Alisema:

Niliposoma hadithi hiyo, nilipaswa kuiga sauti ya milio ya kuku na mbwa, kwa kuwa wakati ule tulitangaza moja kwa moja, nilipata muda wa dakika 10 kusoma hadithi hiyo, hivyo ilinibidi nisome moja kwa moja hata kucheka na kulia, ama kuiga sauti ya milio ya kuku na mbwa, nilipaswa kukamilisha moja kwa moja, hivyo kabla ya kuingia studio, nilifanya maandalizi na kukariri moyoni mara kwa mara.

Baadaye, matangazo ya kiajemi, kiarabu, kiswahili na kihispania yalianza kurushwa hewani kwa nchi za kiarabu, kiafrika na kilatin amerika, ili kuwajulisha watu wa nchi na sehemu hizo kuhusu China ya ujamaa, na kuongeza urafiki kati ya wananchi wa China na watu wa nchi za dunia ya tatu. Katika kipindi hicho, matangazo ya kiingereza yaliyorushwa hewani kwa nchi za Ulaya, Afrika ya kaskazini na sehemu nyingine duniani pia yaliongezwa muda siku hadi siku.

Ilipofika mwaka 1965, Radio ya China ilitangaza kwa lugha 27 za kigeni na lugha 4 za kichina kwa nchi za nje kwa saa 98 kwa siku, ambapo vituo kadhaa vyenye uwezo mkubwa wa kurusha matangazo hewani pia vilianzishwa kimoja baada ya kingine. Na ilipofika katikati ya miaka ya 70 ya karne ya 20, Radio China kimataifa ilitangaza kwa lugha 43 kwa siku.

Wasikilizaji wapendwa, mwaka 1978, kutokana na mageuzi na ufunguaji mlango wa China, matangazo ya China kwa nchi za nje pia yalingia katika kipindi kipya cha maendeleo. Wiki ijayo wakati kama huu mtakaribishwa tena kusikiliza makala ya pili ya chemsha bongo isemayo: Kuelekea kipindi kipya cha maendeleo.

Sasa tunarudia maswali mawili: La kwanza, Je, mtangazaji wa kwanza wa Radio China kimataifa jina lake ni nani? Suali la pili: Mwezi Aprili mwaka 1950, radio ya China ilipoanza kurusha matangazo yake kwa nchi za nje ilijulikana kwa jina gani?

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-16