Tarehe 16 Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio la kutuma jeshi lake kwenye sehemu ya Darfur. Azimio hilo limesema, katika muda wiki moja Umoja wa Mataifa utatuma kikundi cha uchunguzi katika sehemu ya Darfur ili kuweka msingi wa kupeleka jeshi lake la kulinda amani katika sehemu hiyo.
Sehemu ya Dafur iko magharibi mwa Sudan. Mwezi Februari mwaka 2003 makundi ya "the Sudan Liberation Movement" na "the Justice and Equality Movemen" yalifanya uasi dhidi ya serikali. Kutokana na usuluhishi wa Umoja wa Afrika na jumuyia ya kimataifa, mwezi Aprili mwaka 2004 serikali ya Sudan na makundi hayo ya upinzani yalifikia makubaliano ya kusimamisha vita. Mwezi Agosti mwaka huo jeshi la Umoja wa Afrika kwa mara ya kwanza lilitumwa huko ili kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Lakini kutokana na uhaba wa fedha na vifaa, jeshi la Umoja wa Afrika lilikumbwa na shida nyingi, na wafanyakazi wa kimataifa waliondoka kutokana na kutokuwa na usalama. Kwa hiyo Umoja wa Mataifa umeongeza ufuatiliaji na kuwa tayari kutuma jeshi lake huko Darfur ili kulinda amani.
Katika siku ambayo azimio hilo lilipitishwa, baraza la usalama la Umoja wa Afrika lililofanya mkutano huko Addis Ababa, pia lilitoa taarifa likitumai kuwa Umoja wa Mataifa utatuma askari wa kulinda amani huko Darfur mapema iwezekanavyo badala ya jeshi la Umoja wa Afrika. Kwa sababu jeshi la Umoja wa Afrika litakamilisha muda wake mwishoni mwa mwezi Sptemba mwaka huu.
Lakini hadi sasa serikali ya Sudan inakataa kuruhusu jeshi lolote la nje litumwe kwenye sehemu ya Darfur. Waziri wa mambo ya nje wa Sudan, Bw. Lam Akol kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika alisisitiza, serikali ya Sudan inashikilia suala la Darfur litatuliwe na Umoja wa Afrika na kupinga kulikabidhi jukumu la jeshi la Umoja wa Afrika kwa jeshi lolote la kimataifa. Serikali ya Sudan inaona, kuruhusu jeshi la nje kuingia nchini Sudan ni kukiuka mamlaka ya nchi. Hata hivyo serikali ya Sudan haikatai kufanya mazungumzo na Umoja wa Mataifa na kufanya ushirikiano nao. Kutokana na hayo, azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 16 lilizitaka pande mbalimbai za Sudan ziharakishe mchakato wa kupeleka jeshi lake wa kulinda amani badala ya jeshi la Umoja wa Afrika na kuitaka serikali ya Sudan litoe jibu ndani ya wiki moja na kuruhusu wataalamu wa kijeshi wa Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi katika sehemu ya Darfur. China, Russia na Qatar zinaona kwamba nia ya Umoja wa Mataifa ya kutuma askari wake kwenye Darfur ingekubaliwa na serikali ya Sudan, kwani hili ni sharti la kimsingi kabla ya Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kulinda amani.
Tarehe 5 mwezi huu, serikali ya Sudan na kundi la "the Sudan Liberation Movement" imefikia makubaliano ya amani, lakini kikundi cha Nur cha "the Sudan Liberation Movement" na kikundi cha "the Justice and Equality Movement" vilikataa kusaini makubalino hayo. Kutokana na hali hiyo azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema, litachukua hatua kali kwa mtu yeyote na kindi chochote kiitakachoharibu makubaliano hayo. Kadhalika, Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika pia lilihimiza vikundi hivyo viwili visaini makubaliano ya amani kabla ya tarehe 31 mwezi huu. Taarifa inasema, ikiwa vikundi hivyo havitasaini katika muda huo uliowekwa, Umoja wa Afrika utajitahidi kulihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lipitishe azimio na hatua za kuzuia mali na kupiga marufuku ya usafirishaji wa silaha.
Wachambuzi wanaona, msimamo mkali wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwa vikundi vya upinzani umeonesha nia thabiti ya jumuyia ya kimataifa ya kutatua suala la Darfur. Na jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa linasaidia kuleta usalama na kupunguza hali mbaya ya kibinadamu huko Darfur.
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-17
|