Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-17 18:13:06    
Hadithi ya mtangazaji mmoja wa radio, ambaye pia ni mwanamuziki

cri

"Mimi naitwa Lolani Kalu, mimi ni mwanahabari katika kituo kimoja cha Radio hapa Nairobi, nilianza kufanya kazi kama mwanahabari tangu 1985 KBC, naandika habari kwa lugha ya Kiswahili. Vilevile, natengeneza vipindi vya radio, kuandika makala na kusoma taarifa ya habari. Mbali na hayo pia mimi nafanya mambo ya usanii, uandishi wa michezo ya radio, naandika michezo hiyo na kushiriki kwenye uigizaji."

Ilikuwaje n ukaanza mambo ya usanii mbali na uandishi wa habari?

Ni kupenda tu. Tangu nilipokuwa shule nilikuwa napenda sana mambo ya kuigiza jukwaani, niliigiza hadithi za vitabu vya shule, ili wanafunzi wapate urahisi wa kuelewa fasihi kwenye vitabu. Nilipenda sana fasihi simulizi.

"Tangu utotoni nilipenda sana muziki, baba yangu alikuwa ni mwanamuziki na alikuwa akipiga gitaa tangu miaka ya 40, na mama yangu mpaka sasa bado anaimba, na huwa anarekodi nyimbo. Nilipomaliza shule miaka ya 80, nilijiunga na vikundi mbalimbali vya muziki hapa Nairobi, nilikuwa mwanamuziki kabla sijaingia kwenye mambo ya utangazaji, na pia nilicheza ngoma. Zamani kulikuwa hakuna kompyuta na CD, nilikuwa nakwenda studio kucheza kwenye kaseti tu, na tulikuwa tunaenda klabu tofauti kucheza muziki. Halafu nilivutiwa sana na mambo ya utangazaji, hivyo nilikuwa sina wakati mwingi wa kujiendeleza katika mambo ya muziki. Siku moja nilijiuliza mbona niliacha fani ya muziki ambayo nina kipaji, kwa hivyo nilienda studio na kutengeneza Album?nilianzia mambo ya utamaduni, nilitangeneza nyimbo za kitamaduni."

"Nilipenda sana kujifunza lugha za kigeni, na ufasaha wa lugha mbalimbali za kigeni, kama Kifaransa, kijerumani na kiarabu, wakati wa kujifunza lugha hizo, nilijiendeleza na kujua utamaduni wa watu wengine na maisha yao."

Inaoneka kuwa unajishughulisha na mambo mengi, na siku inaonekana fupi kwako, unagawanya vipi muda wako ili kukamilisha mambo yote hayo?

Siku moja ni muda mrefu, ukipanga vizuri unaweza kufanya vyovyote unavyotaka, na usiku unaweza kujiendeleza kabla hujashikwa na usingizi.

Bw. Lolani Kalu anajishughulisha utangazaji, uigizaji na utungaji wa muziki, anagawanya vipi muda wake? Na je ana maoni gani juu ya muziki wa sasa? Na anatoa mapendekezo gani kwa vijana wanaopenda muziki na wanaotaka kuwa wasanii? Tuendelee kumsikiliza Bw Kalu.

Unaionaje fani ya uigizaji hapa Kenya? Je, pato la mwigizaji ni zuri?

Bado, halitoshelezi. Kwa sababu wasanii hasa wa upande huo wa michezo ya kuigiza hawalipwi vizuri, naona hilo ni jambo ambalo limeachwa nyuma kidogo katika sera za serikali. Kwa hivyo ningependa kutoa mwito hasa kwa wabunge wetu kutafuta njia za kutunga sheria ili waigizaji wafahamu haki zao na malipo wanayostahili kupewa. Ikilinganishwa na waigizaji wa mataifa mengine, waigizaji wa Kenya wameachwa nyuma kidogo katika mapato.

Nyimbo zako zinalenga nini ni kuwalenga vijana, wazee au kundi fulani, ni nyimbo zenye ujumbe au ni za kupiga ngoma tu?

Nilijaribu kuleta kumbukumbu za nyimbo za zamani tu, lakini kwa mtindo wa kisasa. Nataka kuleta hali halisi ya watu walivyokuwa wakiishi zamani katika utamaduni wetu, na jinsi walivyokuwa wanaeneza ujumbe fulani.

Nyimbo zako zina ujumbe wa mbalimbali, na unazichukuliaje nyimbo za kisasa hasa hizi zinazopigwa nchini Kenya hivi sasa?

Wasanii wengi wa sasa wanazingatia hasa biashara, hawapendi usanii wa kweli. Siku hizi ni rahisi kuimba, mtu yeyote akipata kundi fulani anaweza kwenda studio; akipata msimamizi na kuweza kupiga ngoma, basi anaendelea. Watu wengi wanatengeneza nyimbo za mapenzi mapenzi ili wajipatie umaarufu haraka.

Una ushauri gani kwa watu wenye kipaji cha usanii na watu wanaopenda muziki?

Nawashauri kuwa wakipenda muziki wafanye utafiti kwanza na kuiga uzoefu wa kufanya mambo hayo, ili wazoee hatua kwa hatua halafu ndio waanze kufanya kazi. Mimi mwenyewe nilipenda sana vichekesho na hadithi fupi za kuchekesha, mtu anaweza kuanzia hapo. Akisoma hadithi moja ya kuchekesha, anapaswa kufikiria kwanza hadithi hiyo ina mafunzo gani kwa jamii. Ushauri mwingine ni kujifunza mambo ya uandishi.

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-17