Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran tarehe 17 alikataa hadharani mapendekezo mapya ya Umoja wa Ulaya ambayo bado yanajadiliwa. Msimamo huo mgumu umeyafanya mapendekezo hayo yanayosifiwa na Umoja wa Ulaya kuwa ni mapendekezo yenye "ushawishi mkubwa" yazame katika hali mbaya kabla hayajatangazwa rasmi.
Kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika siku hiyo mjini Arak, Rais Mahmoud Ahmadinejad alisisitiza kwamba Iran itakataa katakata mapendekezo yoyote yanayotaka Iran isimamishe shughuli za kusafisha uranium. Aliuasa Umoja wa Ulaya "usilazimishe nchi iliyosaini 'mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia' ijitoe kutoka kwenye mkataba huo." Na aliuonya Umoja wa Ulaya usijitie hasara kwa ajili ya lengo lingine." Hotuba yake ilishangiliwa sana na watu elfu kadhaa waliomsikiliza.
Katika siku hiyo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Bw. Hamid Reza Asefi alipogusia upendeleo wa mapendekezo mapya ya Umoja wa Ulaya alisema, Iran pia iko tayari kuutolea upendeleo wa kiuchumi Umoja wa Ulaya ili Iran ipate haki yake ya kusafisha uraium. Alisema, "Soko lenye idadi ya watu milioni 70 wa Iran hakika ni kishawishi kikubwa kwa Umoja wa Ulaya."
Mapendekezo mapya yaliyotolewa kwenye mkutano wa mawaziri wa nchi za Umoja wa Ulaya tarehe 15, yalitoa "ukarimu" mkubwa katika utatuzi wa suala la nyuklia la Iran, ikiwa ni pamoja na kuipatia Iran manufaa mengi ya kiuchumi na kisiasa, kuunga mkono Iran kuendeleza mpango wa nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia ili kuifanya Iran iache kabisa shughuli za kusafisha uranium. Ili kuunga mkono Iran iendeleze mpango wake wa nyuklia, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinafikiria kuipatia Iran kinu cha maji mepesi lakini sharti lake ni kwamba Iran isifanye shughuli za kusafisha uranium nchini humo na kusimamisha mradi wake wa kinu cha maji mazito na kukubali shughuli za kusafisha uranium kwa ajili ya nishati inayotumika katika kinu kipya zifanyike nchini Russia.
Vyombo vya habari vimegundua kwamba mapendekezo mapya hayana tofauti na mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa Ulaya mwezi Agosti mwaka jana. Sababu ya mapendekezo ya awali kukataliwa na Iran ilikuwa ni kuwa Umoja wa Ulaya ulitaka Iran isimamishe shughuli za kusafisha uranium, na Iran ilishikilia haki yake ya kufanya shughuli hizo. Kabla ya mapendekezo mapya kutolewa rasmi, kwa mara nyingi rais na viongozi wakuu wa Iran walisisitiza kwamba Iran kamwe haitakubali mapendekezo yoyote yanayoinyima haki ya kufanya utafiti wa nyuklia. Isitoshe, mapendekezo mapya pia hayakuzungumiwa lolote na Washington. Msemaji wa Marekani tarehe 16 hakuonesha msimamo wowote kuhusu mapendekezo hayo ila tu alisisitiza msimamo wa siku zote wa Marekani, kwamba Iran lazima iache kwanza mpango wake wa nyuklia.
Kwa mujibu wa ratiba, mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani watafanya mkutano tarehe 19 huko London na kujadili suala la nyuklia la Iran, na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zitakamilisha mapendekezo mapya kabla ya hapo na kuwasilisha kwenye mkutano huo ili yajadiliwe. Lakini kutokana na wasiwasi wa mapendekezo hayo, mkutano hauna budi kuahirishwa. Waziri anayeshughulikia mambo ya siasa wa Marekani, Bw. Nicholas Burns tarehe 17 aliwaambia waandishi wa habari akisema, kwa sababu mapendekezo mapya bado hayajakamilishwa, mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi sita pengine utaahirishwa hadi wiki ijayo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Uingereza pia alisema, yumkini mkutano huo utafanyika ndani ya siku kumi zijazo.
Wachambuzi wanaona kwamba mapendekezo mapya yanahusika moja kwa moja ufanisi wa kipindi kipya cha mazungumzo kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la Iran. Kama tatizo lenyewe likikwama kwenye suala nyeti la "kusimamisha au kutosimamisha shughuli za kusafisha uranium", basi mapendekezo hayo hata yatakuwa na ushawishi mkubwa namna gani, suala la nyuklia la Iran litakuwa na utatanishi mkubwa. Bila shaka kama mgongano wa sasa unatokana na mbinu tu za kideplomasia, basi upo uwezekano wa pande mbili kupatana mwishowe. Lakini vyovyote matokeo yatakavyokuwa, mgogoro huo hautamalizika kwa urahisi bila pande zote kufanya juhudi kubwa.
Idhaa ya kiswahili 2006-05-18
|