Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-19 17:02:56    
Bw. Xu Hui azungumza uzoefu wa kufanya biashara katika nchi za Afrika

cri

Kutokana na maendeleo ya uhusiano wa kiuchumi kati ya China na nchi za Afrika, wachina wengi zaidi wanazingatia kwenda katika nchi za Afrika kufanya biashara na kuwekeza vitega uchumi. Bwana Xu Hui ambaye ni meneja mkuu wa kampuni ya elektroniki ya Changhong ya Afrika Mashariki alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari muda si mrefu uliopita alizungumza uzoefu wake kuhusu jinsi ya kutafuta fursa za uwekezaji katika nchi za Afrika. Akisema:

"Nchi za Afrika zina fursa nyingi za kujiendeleza kwa wafanyabiashara wa China. Maendeleo ya uchumi wa nchi za Afrika kwa hivi sasa yanalingana na hali ya nchini China katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, hivyo hatua zilizochukuliwa na China na uzoefu wa China wa kukuza uchumi unafaa kwa nchi za Afrika."

Bwana Xu Hui alitoa mfano akisema, katika sekta ya kutengeneza televisheni, mwanzoni China iliingiza mstari wa uzalishaji wa televisheni kutoka nchi za nje, na kuunda televisheni nchini. Hivi sasa mchakato huo wa kutengeneza televisheni unaendelea nchini vivyo hivyo barani Afrika.

Kwa upande mwingine, hivi sasa ustadi wa nchi nyingi za Afrika wa kutengeneza bidhaa za viwandani na bidhaa za matumizi ya kila siku bado si wa juu, hivyo bidhaa zilizotengenezwa nchini China zinapendwa sana na wakazi wa nchi za Afrika kutokana na sifa bora na bei nafuu. Zamani bidhaa zilizotengenezwa nchini China ziliagizwa na wafanyabiashara wa India na wa nchi za Afrika kwa kupitia soko la Dubai au nchi nyingine, wala siyo moja kwa moja kutoka China. Bw. Xu Hui alisema:

"Wachina wenyewe wakisafirisha bidhaa zilizotengenezwa nchini China na kufanya biashara moja kwa moja katika nchi za Afrika, bila shaka watapata manufaa makubwa zaidi."

Lakini katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na wachina wengi kumiminikia katika nchi za Afrika kufanya biashara, ushindani wa kibiashara kati ya wachina na wafanyabiashara wa nchi nyingine, na kati ya wachina wenyewe umekuwa mkali siku hadi siku. Bw. Xu Hui alisema, si rahisi kwa wanakampuni wa China kuendeleza biashara barani Afrika. akisema:

"Matatizo makubwa yanayowakabili wafanyabiashara wa China ni kuwa wengi hawafahamu vizuri sheria na utaratibu wa masoko ya nchi za Afrika, hawajui kusema lugha za huko, na hawaelewi utamaduni na desturi za kimaisha za wakazi wa huko."

Baadhi ya wachina walipofanya ukaguzi wa kibiashara katika nchi za Afrika waliona kuwa soko la Afrika ni nzuri zaidi kuliko soko la nchini China kutokana na bei kubwa ya bidhaa, lakini baada ya kusafirisha bidhaa kutoka China wakaanza kugundua kuwa, soko la aina moja ya bidhaa ni dogo sana, ambapo bidhaa haziwezi kuuzwa kwa kiasi kikubwa.

Ili kufanya biashara vizuri katika nchi za Afrika, wafanyabiashara wa China wanapaswa kufahamu sheria na utamaduni wa nchi za Afrika. Bw. Xu Hui alisema:

"Nilikutana na tatizo kama hilo nilipoanza kufanya biashara ya televisheni nchini Kenya. Nilifikiri kuwa, watu wa China na nchi nyingi walikuwa wanapenda rangi ya fedha, hivyo niliagiza televisheni nyingi za rangi ya fedha kutoka China, lakini ukweli ni kwamba, watu wa Kenya wanapenda zaidi televisheni za rangi nyeusi."

Ingawa wafanyabiashara wa China wamekutana na matatizo mbalimbali, lakini bado wanaweza kupata faida katika soko la barani Afrika. Akiwa mwekezaji wa mwanzoni nchini Kenya Bw. Xu Hui alijumuisha kuwa, Kenya ni nchi nzuri kuwekezwa vitega uchumi kutokana na hali tulivu ya kisiasa, hali nzuri ya kijiografia na kuwa na mafundi wa aina mbalimbali wenye sifa bora.

Bw. Xu Hui ana umri wa miaka 36, lakini ameishi nchini Kenya kwa miaka zaidi ya 10. Baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu alipata fursa ya kufanya kazi nchini Kenya, baada ya kumaliza zamu yake akaamua kubaki na kuanzisha kampuni yake nchini Kenya.

Bw. Xu Hui anapenda kuishi nchini Kenya, ana marafiki wengi wa sekta mbalimbali, lakini akiwa mchina, bado anasikia upweke wakati wa mapumziko. Akisema:

"Maisha yangu ya hapa Kenya ni tofauti na maisha ya nchini China, wakati wa mapumziko siwezi kukutana na jamaa, marafiki na wanafamilia, tena hakuna vituo vinavyoonesha vipindi vya televisheni kwa lugha ya Kichina kama ilivyokuwa nchini China."

Bw. Xu Hui alisema kuanzishwa kwa kituo cha FM cha Radio China Kimataifa kweli kumemfurahisha sana yeye na wachina wengine waishio nchini Kenya, hasa matangazo ya lugha ya Kichina, anasikiliza karibu kila siku.

Kwenye meza ya Bw. Xu Hui iliwekwa bendera ndogo ya taifa la China, alisema bendera ya taifa la China inaonesha hisia zake za kuipenda China."

Idhaa ya kiswahili 2006-05-19