Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-19 15:55:35    
Waziri wa mambo ya nje wa Iran afanya ziara ya ghafla nchini Syria

cri

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Bw. Manouchehr Mottaki tarehe 18 alifanya ziara ya ghafla nchini Syria bila taarifa, na kufanya mazungumzo na rais wa Syria Bashar al-Assad. Kwenye mazungumzo walibadilishana maoni na kusawazisha misimamo kuhusu hali ya hivi sasa ya Iraq, Marekani na nchi nyingine za Magharibi kuendelea kuzishinikiza Iran na Syria katika suala la Iran na uhusiano kati ya Syria na Lebanon.

Baada ya mazungumzo, waziri wa mambo ya nje wa Iran Manouchehr Mottaki pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al-Muallem walifanya mkutano na waandishi wa habari. Bw. Mottaki alisema, sababu ya yeye kufanya ziara ya ghafla bila kutangaza ni mahitaji ya mabadiliko ya hali ya kikanda. Habari kutoka vyombo vya habari vya serikali ya Syria zinasema, kwenye mazungumzo Bw. Mottaki alimpa Bashar barua kutoka kwa rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad kuhusu "Hali ya hivi sasa ya kikanda na ya kimataifa", lakini maudhui ya barua hiyo hayajafahamika.

Wachambuzi wanaona kwamba ziara ya ghafla ya Bw. Mottaki nchini Syria ilifanyika katika wakati usio wa kawaida, ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la 1680 lililotolewa na Marekani, Uingereza na Ufaransa likiwa ni pamoja na "kuhimiza" Syria na Lebanon kuanzisha uhusiano wa kibalozi, kuweka bayana mpaka kati ya hizo mbili na kuzuia magendo ya silaha mpakani, na Marekani inailazimisha Iran kusimamisha shughuli za kusafisha uranium, na kulisukuma Baraza la Usalama lipitishe mapendekezo mapya ambayo yanapingwa na Iran. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba ziara hiyo ya Bw. Mottaki inalenga kuongeza mshikamana na Syria na kusawazisha misimamo ili kukabiliana kwa pamoja na shinikizo la Marekani na nchi nyingine za Magharibi.

Kwanza, kwa kulenga shutuma za Marekani kuhusu Iran na Syria kuruhusu watu wenye silaha wanaoipinga Marekani kupita kwenye mipaka ya nchi hizo na kuingia nchini Iraq, kuharibu usalama na utulivu wa Iraq, Bw. Mottaki na Bashar kwenye mazungumzo walisema, Iran na Syria, zote ni nchi muhimu jirani ya Iraq, nchi hizo mbili zinaunga mkono Iraq kufanya juhudi za kujenga taifa, na kwamba serikali ya Iraq inapaswa kuchukua yenyewe jukumu la kulinda usalama na kuweka ratiba ya kuyaondoa majeshi yote ya nchi za nje yanayoongozwa na Marekani kutoka Iraq. Kadhalika, pande mbili pia zimesema, nchi hizo mbili Iran na Syria zitaimarisha zaidi uhusiano na Iraq. Ni dhahiri kwamba msimamo wa Iran na Syria unapingana moja kwa moja na Marekani bila hofu yoyote.

Pili, kutokana na Marekani na nchi nyingine za Magharibi kuendelea kulihimiza Baraza la Usalama kupitisha azimio la kuilazimisha Iran isimamishe shughuli za kusafisha uranium. Iran na Syria zimesisitiza kuwa Iran ina "haki isiyopingika" ya kuendeleza mpango wa nyuklia kwa ajili ya amani. Bw. Mottaki alisisitiza kuwa mazungumzo na majadiliano kati ya Iran na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki ni njia pekee ya kutatua suala la nyuklia la Iran. Kwenye mazungumzo Bw. Bashar alisema wazi kwamba Syria inaunga mkono Iran kuendeleza mpango wa nyuklia.

Tatu, kuhusu azimio la 1680 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Iran na Syria zina msimamo wa namna moja. Bw. Mottaki alikosoa azimio hilo kuwa ni "azimio la ajabu na linakwenda kinyume na sheria ya kimataifa", na kusisitiza kwamba Iran inapinga vitendo vyovyote vinavyoongeza hali ya wasiwasi ya kikanda. Bw. Bashar anaona kwamba hatua za Marekani za kutia mkono katika maamuzi ya Baraza la Usalama na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki zimekuwa zikidhoofisha usawa na uhalali wa mashirika ya kimataifa.

Habari zinasema, kabla ya ziara hiyo Bw. Mottaki alitembelea Jordan, na baada ya ziara ya Syria atafanya ziara nchini Kuwait. Ziara zake hizo zinaonesha kwamba Iran inajitahidi kupata maelewano na uungaji mkono wa nchi za Kiarabu kuhusu mpango wake wa nyuklia, na ziara yake ya ghafla nchini Syria imedhihirisha wazi kwamba nchi hizo mbili zitashirikiana pamoja katika mapambano dhidi ya Marekani na nchi nyingine za Magharibi.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-19