Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-22 15:47:03    
Hekalu la Famensi

cri

Katika zaidi ya miaka 3000 iliyopita, miji mkuu ya madola ya kifalme katika enzi 12 za China ya kale ilikuwepo mkoani Shanxi. Mpaka sasa mkoani humo yanahifadhiwa majengo mengi ya zama za kale na mabaki mengi ya utamaduni. Miongoni mwao, Hekalu la Famensi lenye historia zaidi ya miaka 1700 linawavutia sana watalii.

Hekalu la Famensi lilijengwa katika Enzi ya Wei Kaskazini nchini China, yaani mwaka 499 hivi. Hekalu hilo liko katika wilaya ya Famensi mjini Baoji, magharibi ya Mji wa Sian ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Shanxi. Tukipanda gari kutoka Mji wa Sian tutafika kwenye Hekalu la Famensi baada ya saa 3 tu, Hekalu hilo lina eneo la hekta zisizofika 7 za mraba, hili ni hekalu maarufu sana kwa sababu ndani ya hekalu hilo, chini ya pagoda kilizikwa kipande cha mifupa ya mwanzilishi wa dini ya kibuddha, Sakyamuni.

Mwezi Aprili mwaka 1987, wataalamu wa mambo ya kale wa China walipokarabati pagoda ya Buddha lililoporomoka, bila makusudi waligundua ukumbi mmoja ulio chini ya msingi wa pagoda ya zamani, vitu ndani ya ukumbi huo vilistaajabisha watu duniani. Ugunduzi wake unathaminiwa kuwa moja ya magunduzi makubwa zaidi nchini China katika karne ya 20.

Kutokana na vidokezo vya dini ya kibuddha, ili kuenzi dini ya kibuddha, mfalme mmoja wa India ya kale ambaye aliifanya dini hiyo iwe ya kitaifa aliigawa mifupa ya mwanzilishi wa dini ya kibuddha, Sakyamuni, kwa vipande vipande na kuvizika chini ya pagoda 84,000 duniani. Pagoda kama hizo 19 zilijengwa nchini China, na pagoda ndani ya hekalu la Famensi ni moja kati ya hizo.

Kwa kuwa kipande cha mfupa wa mwanzilishi wa dini ya kibuddha kimezikwa kwenye hekalu hilo, hekalu hilo linapata waumini wengi na umaarufu duniani. Kwa mujibu wa vitabu vya zamani, jumla kulikuwa na wafalme wanane wa Enzi ya Tang waliowahi kuchukua sehemu za mwili wa Sakyamuni hadi kwenye kasri ya kifalme na kuabudu, na walitoa zawadi nyingi kwa hekalu hilo. Lakini kutokana na vita, matetemeko ya ardhi, hali ya ustawi wa hekalu hilo baadaye ikatoweka kabisa.

Mwaka 1981, pagoda yenye matabaka 13 iliporomoka kutokana na mvua. Mwaka 1987, mkoa wa Shanxi ulishirikisha wataalamu wa mambo ya kale kufanya uchunguzi juu ya msingi wa pagoda uliobaki, na wakagundua ukumbi huo uliokuwa chini ya ardhi kwa miaka 1,113.

Eneo la ukumbi huo ni mita za mraba 31.48, ndani yake kulikuwa na vitu vingi vya Enzi ya Tang, licha ya kipande cha mfupa wa Sakyamuni, pia kuna vyombo vya kauri, vitambaa vya hariri vya Enzi ya Tang. Kwa mujibu wa takwimu za historia, vitambaa vya hariri vilivyoko ndani ya ukumbi huo ni vya hali ya juu. Uzi wa dhahabu wa kushonea uliogunduliwa huko una unene wa milimita 0.1 na ulio mwembamba sana una milimita 0.66 tu ambao ni mwembamba kuliko unywele. Ndani ya sanduku lililosukwa kwa matawi ya miti kiliwekwa kitambaa cha hariri, ingawa unene wa kitambaa chenyewe kilichokunjuka una sentimita 23 tu lakini kina matabaka 780. Ndani ya ukumbi huo pia viligunduliwa vyombo vingi vya dhahabu na fedha, na vya kauri.

Kwanini ndani ya ukumbi chini ya msingi wa pagoda ya zamani kuna hazina hizo nyingi? Meya wa Mji wa Baoji Bwana Yao Yinliang alifahamisha kuwa, Hekalu la Famensi liliwahi kuwa na ustawi mkubwa katika Enzi ya Tang zaidi ya miaka 1300 iliyopita, Serikali ya Enzi ya Tang ilitumia pesa nyingi na watu wengi kuongeza majengo katika hekalu hilo mpaka likawa na nyua 24 za nyumba, na watawa elfu 5.

Wakati huo hekalu hili lilikuwa kubwa kabisa katika eneo la mji mkuu wa Enzi ya Tang, ambapo hekalu hilo lilichukuliwa kuwa hekalu la kifalme la enzi ya Tang, ambapo wafalme kadha wa kadha wa enzi ya Tang waliwahi kuabudu kipande cha mifupa ya mwanzilishi wa dini ya kibudha, hata waliwahi kukichukua kwenda kwenye kasri la kifalme kuabudiwa, ambapo wafalme walitoa sadaka za hazina nyingi kwa hekalu hilo.

Mwaka 874 mfalme mmoja wa Enzi ya Tang aliposindikiza kipande cha mifupa ya mwanzilishi wa dini ya kibudha Sakyamuni ndani ya Hekalu la Famensi, alihikifadhi kwenye ukumbi chini ya msingi wa pagoda la Hekalu la Famensi pamoja na vyombo vingi vya dhahabu na fedha, vyombo vya vioo, kauri, lulu na nguo, na kufunga mlango wa ukumbi huo chini ya hekalu. Mwaka hadi mwaka, hazina hizo na ukumbi ulioko chini ya hekalu zilisahauliwa na watu, mpaka mwaka 1987 zilipofukuliwa. Bwana Yao Yinliang alisema:

Utamaduni wa dini ya kibudha wa Hekalu la Famesi ni wenye mtindo pekee kote nchini China, kwani kipande cha mifupa ya mwanzilishi wa dini ya kibudha Sakyamuni kinaabudiwa ndani ya hekalu hilo, tena hazina nyingi za Enzi ya Tang zilifukuliwa kutoka kwenye hekalu hilo. Hivyo kila mwaka shughuli zinafanyika kwenye hekalu hilo ili kuvutia watalii.

Ili kutunza hekalu na vitu vyake vilivyofukuliwa, yamejengwa makumbusho. Kwa kushirikiana na wataalamu wa Ujerumani, wataalamu wa China wamefanikiwa kupata teknolojia ya juu kuhifadhi vitambaa vya hariri. Mwaka 2002 kipande cha mfupa wa mwanzilishi wa dini ya kibuddha, Sakyamuni, kilipelekwa Taiwan kwa lengo la kuabudiwa. Katika muda wa mwezi mmoja, waumini waliokwenda kuabudu walifikia milioni 4.

Kila mwaka ifikapo mwezi Aprili, inafanyika shughuli za siku ya utamaduni na utalii kwenye Hekalu la Famensi, ambapo shughuli za kidini hufanyika kwenye hekalu hilo, ambapo pia yanafanyika maonesho ya hazina za Enzi ya Tang. Mtalii kutoka Ujerumani Bibi Monika Westermann alivutiwa sana na utamaduni wa dini ya kibudha kwenye hekalu hilo, alisema shughuli za siku ya utalii ziliwafurahisha sana watu wa familia yake. Alisema:

Shughuli zote ziliandaliwa vizuri na kutufurahisha, kweli hatukuwahi kuziona katika sehemu nyingine duniani.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-22