Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-22 16:24:22    
Chen Yan, fundi wa kwanza mwanamke Mchina asiyeona wa kurekebisha sauti za piano

cri

Chen Yan alizaliwa mwaka 1973 na kukulia mjini Beijing. Kwa kuwa alizaliwa na tatizo la mtoto wa jicho, ingawa alifanyiwa upasuaji lakini jicho lake la kushoto linaweza tu kuona nuru kidogo na jicho la kulia haliwezi kuona kabisa. Kutokana na ulemavu huo alitelekezwa na wazazi wake na alilelewa na bibi yake mpaka alipokuwa mtu mzima.

Ili Chen Yan aweze kukua kama watoto wengine, nyanya yake alifanya juhudi kila awezavyo kumsaidia mjukuu wake kuimarisha usikivu na hisia ya kugusa kitu. Alipokuwa na umri wa miaka minne bibi yake alimzoesha kutembea kwa kutegemea usikivu. Bibi yake huyo alikuwa akitupa sakafuni sarafu zenye thamani tofauti na kumwambia Chen Yan atofautishe sauti. Na ili kuimarisha hisia yake ya kugusa, bibi yake alimzoesha kutunga uzi kwenye sindano. Ufundi huo ulikuwa unamsumbua sana hapo mwanzoni, vidole vyake vilikuwa vinachomwa mara nyingi. Lakini ni mazoezi hayo ndio yalimsaidia sana katika maisha yake, na yalimwekea msingi wa kuwa fundi wa kurekebisha sauti za piano baadaye. Mafanikio aliyonayo leo, yote yanatokana na uwezo aliopata kutoka kwa malezi ya bibi yake alipokuwa utotoni. Alipokumbuka jinsi bibi yake alivyojitahidi kumfundisha uwezo wa kuishi kwa kujitegemea, alisema, "Maishani mwangu mtu muhimu zaidi ni bibi yangu, nimekua kwa kutegemea matunzo yake. Nilipokuwa mtoto, bibi yangu alikuwa na wasiwasi sana akihofia kuwa nitakufa kwa njaa, kwa hiyo alijitahidi sana kunifundisha ili niwe na ufundi fulani kujitegemea, na alinielimisha niwe shupavu. Mara nyingi aliniambia kwamba lolote unalotaka kulifanya, shikilia ulifanye, usijali mafanikio utakayopata, muhimu ni mchakato wa kufanikisha jambo lako. Na kweli nilifanya hivyo toka utotoni mwangu hadi sasa. Pia bibi yangu aliniambia, duniani hakuna shida, chochote unachotaka kujifunza mwishowe hakika utakipata kwa kiasi fulani kama si kizima, pindi tu ukifanya juhudi bila kulegalega."

Kutokana na ulemavu wake, Chen Yan alikataliwa na shule nyingi hadi alipokuwa na umri wa miaka 13, lakini alijiunga na shule moja ya walemavu wa kutoona. Chen Yan alipenda muziki na aliwahi kujifunza kucheza ala nyingi za muziki. Mwanzoni mwa karne iliyopita, China iliingiza ufundi wa kisasa wa kurekebisha sauti za piano kutoka Ulaya, na Chen Yan alichagua ufundi huo katika shule hiyo. Kipindi hicho alijifunza ufundi huo kilimkaa sana kichwani. Alisema, "Mwanzoni sikufikiri kwamba ufundi huu ni mgumu kama vile, kwamba vipuri tu vya piano viko zaidi ya elfu nane, na lazima nifahamu kila kipuri kilipo, niweze kutenganisha kila sehemu na kuzifunga pam0oja, na kukarabati. Kitu muhimu ni kwamba kama kipuri fulani kikiharibika inanipasa nitengeneze mwenyewe. Somo gumu kabisa ni useremala, tulifanya mazoezi ya kugonga misumari, kisha kuing'oa na kutia parafujo, mikono yangu ilikuwa na majeraha siku zote."

Kazi ya kufahamu vipuri zaidi ya elfu nane ni ngumu hata kwa watu wa kawaida, mbali kwa walemavu wasioona, lakini Chen Yan hakurudi nyuma kwa kujiona kuwa ni mlemavu asiyeona. Alitumia muda wa saa 14 hadi 15 kila siku kufanya mazoezi ya kurekebisha sauti za piano. Kutokana na kujiamini na juhudi zake, mwishowe aliudhibiti ufundi huo.

Alipotimiza miaka 22, Chen Yan alihitimu somo lake la kurekebisha sauti za piano. Akiwa amejawa na uhakika mkubwa alijiunga na jamii, lakini aligonga mwamba bila huruma, idara zote za piano zilikataa kumwajiri. Baadaye alikuwa hana budi kujifunza tiba ya Kichina ya usingaji mwili na alipata shahada. Lakini siku moja kwa bahati tumaini liliwaka tena katika mazungumzo na msingaji mwenzake, na akarudi kwenye ufundi wa kurekebisha sauti za piano.

Baada ya juhudi mwishowe alifanikiwa kupata ajira kwenye duka moja kubwa la piano. Meneja wa duka hilo alimtahini kwa kurekebisha sauti za piano moja, kisha alichunguza kwa makini, aliridhika na kukubali kumwajiri. Ili kuwahudumia wateja wa duka hilo, alitumia mwezi mzima kufahamu ramani ya Beijing. Juhudi za kazi yake na umahiri wake ulisifiwa na wateja.

Baada ya kupata kazi ya uhakika Chen Yan hakusahau wenzake kama yeye, na kuona kuwasaidia ni furaha yake. Mwaka 2004, kwa kutumia kompyuta yenye sauti alimaliza kitabu chake cha maelezo binafsi "Dunia Masikioni Mwangu". Ndani ya kitabu hicho alieleza jinsi alivyopambana na shida na alivyozishinda, kitabu hicho kinalega kuwahamasisha walemavu wenzake. Katika mwaka huo Chen Yan alianzisha kampuni ya kurekebisha sauti za piano mjini Beijing, kampuni hiyo inatoa huduma kwa nchi nzima ya China. Chen Yan alisema, "Watu wengi wanafikiri kwamba nia ya kuanzisha kampuni ni kujitajirisha, lakini kwa kweli nalipuuza suala hilo, faida nilizopata zote nazigawa kwa warekebishaji wenzangu. Ulaya umekuwa na historia zaidi ya miaka mia moja ya ufundi wa kurekebisha sauti za piano, lakini nchini China kampuni yangu aambayo ni ya kwanza, imekuwa na miaka 12 tu, nina uhakika kwamba kwa kufanya juhudi pengine kampuni yangu pia itakuwa maarufu baada ya miongo kadhaa. Tumaini langu ni kuipatia kampuni yangu umaarufu nchini China."

Bi. Chen Yan sio tu ni mahiri wa kurekebisha sauti za piano, lakini pia ni mlemavu wa kwanza asiyeona katika mambo mengi, kwamba yeye ni mlemavu wa kwanza asiyeona kuandika tawasifu, na ni mlemavu wa kwanza asiyeona kupanda baiskeli ya gurudumu moja. Kadhalika pia anaweza kuendesha baiskeli, kuteleza sakafuni kwa viatu vya magurudumu. Cha ajabu ni kwamba mwaka 1987 alipata tuzo katika maonesho ya kimataifa ya picha za kuchorwa na watoto nchini Japan.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-22