Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-24 19:09:32    
Ziara ya chansela wa Ujerumani itasukuma mbele maendeleo ya uhusiano kati ya China na Ujerumani

cri

Chansela wa Ujerumani Bibi Angela Merkel alifanya ziara nchini China kuanzia tarehe 21 hadi 23 mwezi huu, ziara yake hiyo ilivutia macho ya watu wengi, kwani hii ni ziara ya kwanza ya chansela huyo nchini China tangu ashike madaraka mwezi Novemba mwaka jana. Watu wanafuatilia zaidi ziara yake kuona imepata mafanikio gani na itaonesha umuhimu gani kwa maendeleo ya uhusiano kati ya China na Ujerumani katika siku za baadaye.

Dokta Hu Dawei wa ofisi ya utafiti wa masuala ya Ulaya katika kituo cha utafiti cha masuala ya kimataifa cha china alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, ziara ya chansela Merkel nchini China ni ziara yenye mafanikio na ambayo itasukuma mbele maendeleo ya uhusiano kati ya China na Ujerumani. Alisema mafanikio ya ziara yake yameonekana katika mambo ya sekta mbili.

Kwanza katika mambo ya kisiasa, chansela Merkel alikuwa na mazungumzo na rais Hu Jintao wa China na waziri mkuu Wen Jiabao, viongozi wakuu hao wamedumisha mawasiliano barabara, hii inasaidia maelewano na uaminifu kati ya viongozi wa China na Ujerumani, hasa inasaidia chansela huyo aongeze uelewa juu ya China. Katika mazungumzo kati yao, pande mbili zimeahidi kuimarisha na kusukuma mbele zaidi uhusiano kati ya China na Ujerumani, na kuamua kuanzisha utaratibu wa mazungumzo ya kimkakati katika ya ngazi ya mawaziri wa China na Ujerumani mwaka huu, hatua hii hakika itaziwezesha China na Ujerumani zianzishe njia mpya ya kuimarisha mazungumzo na kuzidisha ushirikiano. Pili, ziara ya chansela huyo pia imepata matunda mengi katika sekta za uchumi na biashara, ambapo China na Ujerumani zilisaini makubaliano 19 yanayohusu sekta nyingi.

Tangu China na Ujerumani zianzishe uhusiano wa kibalozi mwaka 1972, uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea siku hadi siku, na matunda kemkem yamepatikana katika ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye sekta mbalimbali. Lakini baada ya Bibi Merkel kushika madaraka ya chansela, watu wengi walikuwa na wasiwasi kama chansela huyo atadumisha utekelezaji wa sera za Ujerumani kwa China au la. Dokta Hu Dawei alisema:

Mwanzoni watu walidhani Chansela Merkel anatilia maanani zaidi kuendeleza uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani, walihofia kuwa uhusiano kati ya China na Ujerumani utaathiriwa. Lakini kwa kweli uhusiano kati ya China na Ujerumani ni uhusiano uliopevuka na wenye utulivu, ambao ulianzishwa kwenye msingi wa maslahi mengi ya pamoja na maoni ya pamoja kuhusu mambo mengi ya kimataifa, siyo rahisi kuathiriwa na hali nyingine.

Wakati wa ziara yake nchini China, Bibi Merkel alieleza msimamo wake wa kudumisha na kuendeleza sera zilizofuatwa na serikali za awamu kadhaa za Ujerumani kwa China, ahadi yake imeondoa wasiwasi wa watu.

Bwana Hu Dawei anaona kuwa ziara yenye mafanikio ya chansela Merkel imeonesha kuwa, kuendeleza uhusiano kati ya China na Ujerumani kunalingana kabisa maslahi ya kimsingi ya nchi hizo mbili. Alisema:

Mwezi Machi mwaka 2004, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alipofanya ziara nchini Ujerumani, pande mbili zilitangaza kuwa zitaendeleza kwa pamoja uhusiano wa kimkakati na kiwenzi wa kuwajibika kwa dunia nzima kwenye msingi wa uhusiano huo kati ya China na Ulaya. Hii ilithibitisha kisahihi umuhimu wa uhusiano kati ya China na Ujerumani. Hali halisi ni kwamba, China na Ujerumani zote ni nchi kubwa zenye ushawishi katika mambo ya kimataifa. China inaunga mkono Ujerumani ioneshe umuhimu wake katika mambo ya kimataifa hasa katika jumuiya za kimataifa. Na Ujerumani pia inaiunga mkono China ioneshe umuhimu wake katika mambo ya kimataifa.

Lakini Bwana Hu Dawei pia alidhihirisha kuwa, hivi sasa bado kuna masuala kadhaa na maoni tofauti katika uhusiano kati ya China na Ujerumani kama vile uhifadhi wa hakimiliki, mazungumzo kuhusu suala la utekelezaji wa sheria kati ya China na Ujerumani na mengineyo.