Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-24 21:12:17    
Naibu waziri wa habari wa Kenya azungumzia uwezekano wa Kiswahili kutumika Umoja wa Mataifa

cri
Leo tumeweza kuzungumza na naibu waziri wa habari nchini Kenya mheshimiwa Koigi Wamwere ambaye alihudhuria kongamano moja nchini Marekani ambapo lugha ya Kiswahili ilizungumziwa. Kwanza anaeleza jinsi yeye mwenyewe anavyokikuza Kiswahili.

Kuna njia nyingi nazotumia kukikuza Kiswahili na wakati mimi mwenyewe nikizidi kujifunza Kiswahili. Kwanza niseme mkataa mila yake ni mtumwa, kwa hiyo ninapotumia Kiswahili ninakuwa huru kwa sababu hata nikitumia Kiingereza kwa ufasaha namna gani hakuna wakati waingereza wataheshimu, na kwa jinsi unavyozidi kuongea Kiingereza kwa ufasaha zaidi ndivyo unavyozidi kuonekana kuwa mtumwa. Kwa hiyo kama mtu unataka kuonekana mtu huru ni vyema ukazungumza lugha yako ya asili, unayoweza kujivunia. Tunajitahidi kuongea sana Kiswahili bungeni ili watu wengi zaidi watuelewe. Pia nasoma magazeti hasa gazeti la Tanzania Rai, riwaya za aina mbalimbali na kufikiri kwa Kiswahili.

Kongamano hilo lilikuwa mkutano wa kamati ya habari ya Umoja wa Mataifa, ambayo Kenya ni mwanachama. Kazi kubwa ya kamati hiyo ni kutambua na kuamua ni nyenzo gani zitakazotumiwa kueneza habari juu ya kazi za Umoja wa Mataifa na idara zake. Wakati nikitoa ripoti ya Kenya katika mkutano huo nilishawashika kuhoji kwa nini Afrika haina lugha hata moja inayotumika katika Umoja wa Afrika, kwani lugha nyingi ni kutoka bara la Ulaya kama vile Kiingereza, Kihispania, Kifaransa. Na nje ya hizo lugha kuna Kiarabu na Kichina. Sasa kama dunia haitaki kukandamizwa kimawazo kwa nini basi Umoja wa Mataifa usichague lugha moja kutoka Afrika na kuifanya lugha yake rasmi? Nikasema hili ni kosa na ni jambo linalitakiwa kusahihishwa kwa haraka. Na kwa bahati nzuri tukaungwa mkono na wanachama wengi kuhusu kukifanya Kiswahili moja ya Afrika kuwa lugha rasmi katika Umoja wa Mataifa. Na ujumbe wa Tanzania uliwasilisha hoja hiyo kwenye kamati ya nchi ambazo zilikuwa zinaongea juu ya maamuzi ya kamati hayo na yatawasilishwa katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ili uweze kufanyiwa uamuzi. Kwa ufupi niseme kama nchi za Afrika zikiungana basi, Kiswahili kitakubalika na kuwa lugha rasmi ya Umoja wa Mataifa.

Kama Waarabu walivyopigania Kiarabu hadi kikawa lugha rasmi katika Umoja wa Mataifa, Waafrika pia inatubidi tuache uzembe, tushirikiane na tupigane kwa dhati ili Kiswahili kiweze kuwa lugha ya Umoja wa Mataifa. Ni lazima tuondokane na utumwa wa kifikra na kujivunia kuongea lugha za kigeni na tupende lugha zetu.

Kama serikali zetu za Afrika zitakuwa makini na zitasukuma hoja hiyo basi natumai kuwa Kiswahili kitakuja kuwa lugha rasmi ya Umoja wa Mataifa.