Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-25 16:51:11    
Madhara ya afya yanayotokana na chakula cha haraka cha kimagharibi yafuatiliwa nchini China

cri

Hivi sasa nchini China chakula cha haraka cha kimagharibi, mfano kinachopatikana katika mikahawa ya Mcdonalds na KFC, kinawavutia watu wengi na wakati huo huo kinapingwa na watu wengi. Mkahawa wa Mcdonalds unajitetea kuwa, unawaandalia watoto chakula kizuri na kitamu. Lakini watu wengine wanasema, chakula kinachotolewa na Mcdonalds kimeleta siku za utoto zenye unene na maradhi. Kwa kukabiliana na matatizo ya afya yanayosababishwa na chakula cha haraka cha kimagharibi, baadhi ya Wachina wameeleza wasiwasi wao mkubwa na kutoa wito wa kuchukua hatua za kuzuia maendeleo ya mikahawa ya chakula cha namna hii.

Katika mkahawa mmoja wa Mcdonalds mjini Beijing, mwandishi wetu wa habari aliona kuwa miongoni mwa wateja wa mhakawa huo, watoto walikuwa wengi zaidi. Watoto wawili walipohojiwa walieleza maoni yao. (sauti 1) "Napenda kumfuata baba yangu kwenda Mcdonalds, chakula cha huko ni kizuri na kina ladha nzuri, pia naweza kupata zawadi." "Naipenda. Kwa sababu kuna vipapatio vya kuku, napenda sana kuvila, pia kuna siagi. Ni vipapatio vya kuku na siagi ndivyo vinanivutia."

Mbali na watoto, vijana pia ni wateja wa kawaida katika mikahawa ya chakula cha haraka cha kimagharibi, wanafunzi wa sekondari wa vyuo vikuu na wapenzi wanakutana katika mihakawa hiyo, hali ambayo inafanya mikahawa hiyo mingi nchini China kuwa na biashara nzuri.

Takwimu zinaonesha kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, kampuni ya Mcdonalds imekuwa na mikahawa 700 nchini China, ambapo kampuni ya KFC ilikuwa na mikahawa 1,200 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2004. Na idadi ya mikahawa ya kampuni nyingine za chakula cha haraka cha kimagharibi kama vile Pizzahut na Original, pia inaendelea kuongezeka nchini China.

Sambamba na hali ya kupamba moto kwa chakula cha haraka cha kimagharibi nchini China, katika Marekani ambayo ni maskani ya Mcdonalds, kijana mmoja wa Marekani aitwaye Morgan Spurlock alianza kuchukua hatua ya kupinga chakula cha haraka. (sauti 2)

Katika kipindi cha mwezi mzima mwaka 2004, Bw. Morgan alikuwa anakula chakula na kunywa vinywaji vya Mcdonalds tu. Kipindi hicho kilipomalizika, aliongeza uzito wa kilo 12, na zaidi yake, mwili wake ukaanza kuwa na dalili za kuumwa. Bw. Morgan aliweka rekodi kwa video mabadiliko ya mwili wake katika kipindi hicho cha mwezi mmoja, na kutengeneza filamu moja, akilenga kuwaambia wengine kuwa, chakula cha haraka kinachotolewa na kampuni kadhaa maarufu duniani kinaathiri afya ya watu.

Nchini China wanaopinga chakula cha Mcdonalds kama alivyofanya Bw. Morgan wanaongezeka, ambao ni pamoja na Bw. Zhang Jiao na Bibi Yang Yuexin.

Bw. Zhang Jiao ni katibu mkuu wa kamati kuu ya Chama cha kidemokrasia cha kujenga taifa, ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la taifa. Alianza kufuatilia suala la chakula cha haraka cha kimagharibi mwaka 2003, kutokana na kipindi kimoja cha televisheni kuhusu mtoto mdogo wa kike, ambaye alikuwa anakula hambug kwa mwezi mzima kwa ajili ya kushinda zawadi ya Mcdonalds. (sauti 3) "Hii ni mbinu ya kukuza biashara ya mikahawa ya chakula cha haraka. Ukigharimikia kwa kiasi fulani kununua chakula, unapewa zawadi ya mkanda wa saa ya mkononi, na baada ya kulimbikiza mikanda kadhaa ya saa, unaweza kupata saa ya mkononi. Mtoto huyo alikuwa na hamu ya kupata saa moja ya mkononi, kwa hiyo alikula chakula kingi cha haraka cha kimagharibi. Lakini alipewa tu mikanda kadhaa ya saa za mikononi mwishowe, akakata tamaa. Katika kipindi hicho kisichozidi mwezi mmoja, alinenepa na kuongezeka uzito wa kilo zaidi ya 10."

Bibi Yang Yuexin ambaye ni mtaalamu wa taaluma ya viinilishe alieleza maoni yake kuwa, chakula cha haraka cha kimagharibi kweli ni chakula kisichosaidia afya ya watu. (sauti 4) "Kwa nini kinapewa jina la chakula kisichosaidia afya ya watu? Kwa sababu chakula kinachoandaliwa na kampuni za chakula cha haraka cha kimagharibi, mfano wa Mcdonalds, KFC na Pizzahut, ni chakula chenye asilimia kubwa ya joto, mafuta na protini. Mbali na hayo mikahawa hiyo inatoa vyakula vya aina chache tu. Mtu anayekula mara kwa mara mikahawa ya chakula cha haraka cha kimagharibi, atakabiliwa na hatari kubwa ya kuongezeka uzito."

Mtaalamu huyo alifafanua kuwa, mtoto huwa anahitaji joto la kalori 1,300 kila siku, lakini seti moja ya kawaida ya chakula inayotolewa na Mcdonalds imezidi kiwango hicho. Joto la ziada hulimbikizana mwilini na kusababisha unene, ambao hatari yake kwa afya ya watoto imejulikana.

Takwimu kutoka Wizara ya afya ya China zinaonesha kuwa, asilimia ya watu wanene miongoni mwa watu wa China inaongezeka. Hapa mjini Beijing, watoto wenye unene wa kupita kiasi wanaonekana mara kwa mara barabarani, ambao wanatembea kwa shida. Bibi Yang Yuexin alieleza wasiwasi wake kuwa, chakula cha haraka cha kimagharibi huenda kitawatawala watoto na vijana, na kuwafanya washindwe kuondokana na tatizo la unene.

Mwaka 1995 bibi huyo alichapisha makala yake ya kwanza ya kukosoa chakula cha haraka cha kimagharibi. Katika miaka 11 iliyopita, ameshikilia msimamo wake wa kukipinga chakula cha namna hiyo. Kwa maoni yake, ni lazima kukamilisha sheria zilizopo katika mapambano hayo. Alieleza kuwa, nchini Australia na Uiingereza, zimetangazwa sheria za kupiga marufuku matangazo ya kibiashara ya chakula cha haraka chenye joto jingi na mafuta mengi yasitangazwe katika televisheni katika muda ambao watu wengi wanavitazama vipindi vya televisheni. Lakini sheria ya namna hii bado haipo nchini China. (sauti 5) "Ukila chakula kisicho safi, unapata ugonjwa wa kuhara, na sheri zipo za kusimamia shughuli za namna hii. Lakini kwa chakula chenye matatizo ya uwiano wa viinilishe, hakuna watu wanaokisimamia, ndiyo maana inabidi kutunga sheria husika."

Katika miaka miwili ya hivi karibuni, matatizo mbalimbali yanayotishia usalama wa chakula ambayo yanasababishwa na chakula cha haraka cha kimagharibi yamejitokeza nchini China. Kwa mfano, ndani ya viazi vya kukaangwa vinavyouzwa na Mcdonalds huenda vina vitu vinavyosababisha ugonjwa wa saratani, na chakula cha KFC kimechanganywa viungo vinavyoweza kusababisha ugonjwa wa saratani.

Habari zinasema kuwa, hivi sasa idara husika za China zinafanya kazi ya kurekebisha sheria ya usalama wa chakula, na mswada wa marekebisho ya sheria hiyo unatarajiwa kuwasilishwa mwezi Decemba, mwaka huu kwa chombo cha utungaji sheria ili upitishwe.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-25