Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-25 20:03:46    
Mkutano kuhusu suala la nyukilia la Iran wafanyika mjini London

cri

Maofisa wa ngazi ya juu wa nchi 6 zikiwemo nchi 5 za wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Russia na China, pamoja na Ujerumani, walikuwa na mkutano wa faragha tarehe 24 huko London, wakijadili mpango mpya uliopendekezwa na nchi 3 za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wenye lengo la kuihimiza Iran iache mpango wake wa nyukilia. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uingereza baada ya mkutano huo kumalizika alisema, mkutano huo umepata maendeleo ya kufurahisha na ni mkutano wenye maana kubwa; Mkutano huo unataka mawaziri wa nchi 6 wawe na mkutano haraka iwezekanavyo ili kutoa uamuzi kuhusu suala la nyukilia la Iran.

Msemaji huyo alikataa kutoa maelezo kamili kuhusu majadiliano yao ila tu alisema, mkutano huo umeonesha ufuatiliaji wa jumuiya ya kimataifa kuhusu mpango wa nyukilia wa Iran. Baadhi ya maofisa wa kidiplomasia walidokeza kuwa mpango mpya wa nchi 3 za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusu utatuzi wa suala la nyukilia la Iran ulikuwa mambo muhimu yaliyojadiliwa kwenye mkutano. Kutokana na mpango huo mpya unaoitwa kuwa "karoti na kiboko", endapo Iran inarejea kwenye mazungumzo ya suala la nyukilia, kuacha kusafisha uranium na kutozuia tena shirika la nishati ya atomiki duniani kufanya ukaguzi wa nyukilia, basi nchi zote zitakubali kusimamisha majadiliano ya baraza la usalama kuhusu suala la nyukilia la Iran. Licha ya hayo, Umoja wa Ulaya utaisaidia Iran kujenga kinu cha nyukilia cha maji mepesi na kuthibitisha kuwa utaipatia Iran nishati ya nyukilia kwa miaka 5. Aidha, mpango huo unataka Iran ifanye usafishaji wa uranium nchini Russia ili kuondoa mashaka ya nchi mbalimbali ya kuishuku kuendeleza silaha za nyukilia.

Mbali na hayo, mpango huo pia umeweka adhabu kuwa baraza la usalama litaiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi kufuata kifungu cha 41 cha ibara ya 7 ya katiba ya Umoja wa Mataifa, endapo Iran itashikilia kuendeleza shughuli za nyukilia. Lakini tofauti na mpango ule wa awali kuwa mpango mpya haukutaja kuiadhibu kijeshi Iran kwa kufuata kifungu cha 42 cha katiba ya Umoja wa Mataifa. Hii ni kama kusema kuwa mpango mpya umeondoa uwezekano wa kuchukua hatua za kuishambulia kijeshi Iran. Wachambuzi wanaona kuwa mpango mpya wa Umoja wa Ulaya haukusema kutumia kifungu cha kutumia nguvu za kijeshi kutokana na kuweko tofauti kubwa za misimamo ya nchi wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama, na pia ni matokeo ya juhudi za Russia na China, ambazo zinashikilia kutatua suala la nyukilia la Iran kwa njia ya mazungumzo. Toka zamani, China inapinga kuweka vikwazo au kutoa vitisho vya kijeshi katika shughuli za kimataifa, lakini hapo awali Marekani, Uingereza na Ufaransa zilishikilia kutoondoa uwezekano wa kutumia kifungua cha 42 cha katiba ya Umoja wa Mataifa. Wachambuzi wanaona marekebisho hayo ya mpango mpya ya Umoja wa Ulaya ni kutaka kuondoa migongano ya pande mbalimbali, hususan ni kutaka kupata uungaji mkono wa Russia na China kuhusu mpango mpya.

Hivi sasa, Iran imetaka kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani. Iran inafahamu kabisa, ingawa Umoja wa Ulaya ni upande muhimu unaotaka kuwa na mazungumzo na Iran, lakini Marekani ni nchi yenye uamuzi wala siyo Umoja wa Ulaya na shirika la nishati ya atomiki duniani. Lakini toka zamani Marekani haikutaka kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Iran kuhusu suala la nyukilia. Ingawa hivi sasa Marekani inasema inauunga mkono Umoja wa Ulaya kuzindua upya harakati za kidiplomasia, lakini kwa undani haiamini kama kuna uwezekano wa njia ya mazungumzo wa kuweza kuilazimisha Iran kuacha mpango wake wa nyukilia, bali inataka kuchukua hatua za nguvu zikiwemo kuweka vikwazo na kuishambulia kijeshi. Katika siku ya kuanzisha mkutano wa London, msemaji wa Ikulu ya Marekani Tony Snow aliviambia vyombo vya habari kuwa, Marekani kamwe haitakuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Iran, hadi Iran itakapoacha kwa muda shughuli za kusafirisha uranium. Wachambuzi wanaona kuwa, hali ya hivi sasa inaonesha kuwa si Iran wala Marekani zote hazijaonesha dalili ya kulegeza misimamo yao, na bado hakijafahamika kiwango cha kukubaliwa na pande mbalimbali kwa mpango huo mpya wa Umoja wa Ulaya.