Tarehe 25 Mei ya miaka 43 iliyopita, wakuu wa nchi zaidi ya 30 za Afrika walisaini Katiba ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika, na kuanzisha jumuiya ya nchi huru za Afrika, hivi sasa Umoja huo umebadilishwa kuwa umoja wa Afrika AU. Ili kuadhimisha tukio hilo, tarehe 25 Mei imethibitishwa kuwa Siku ya Afrika. Mwaka huu mabalozi wa nchi za Afrika nchini Zimbabwe na Chuo Kikuu cha Harare walifanya kongamano kwa pamoja ili kuadhimisha siku hiyo.
Kongamano hilo lilifunguliwa kwa wimbo uitwao "Mungu abariki Afrika". Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Harare Bwana Austin Chivinge alipotoa risala kwenye ufunguzi huo alimkariri mwanzilishi wa "Umoja wa Nchi Huru za Afrika", ambaye pia ni rais wa zamani wa Ghana Bwana Kwame Nkrumah akisema, nchi za Afrika zinapaswa kuungana la sivyo zitaangamizwa. Bwana Austin Chivinge alisema, kuhimiza mshikamano wa nchi za Afrika ni moja ya malengo ya kuanzishwa kwa "Umoja wa Nchi Huru za Afrika". Akisema:
"Nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto nyingi, ni muhimu sana kwa nchi za Afrika kuungana ili kukabiliana na changamoto hizo. Nchi mbalimbali zinapaswa kushirikiana katika juhudi zao za kupunguza umaskini, kuhakikisha usalama wa chakula, na kuboresha hali ya afya ili kuleta maendeleo."
Waliohudhuria kongamano hilo waliona kuwa, "Umoja wa Nchi Huru za Afrika" na "Umoja wa Afrika" wa baadaye umepata maendeleo kadha wa kadha katika sekta mbalimbali ni pamoja na kuinua hadhi ya wanawake, lakini nchi za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto kubwa ya kuendeleza uchumi. Japokuwa bara la Afrika ni bara lenye rasilimali nyingi zaidi duniani, ambapo nchi 10 zinazalisha mafuta, na miongoni mwao nchi tatu ni nchi wanachama wa shirika la nchi linalosafirisha mafuta duniani OPEC; asilimia 95 ya almasi, asilimia 30 ya Chromium na asilimia 22 ya aluminum duniani zinazalishwa barani Afrika. Lakini kwa upande mwingine, idadi ya watu maskini barani Afrika ni kubwa zaidi kuliko sehemu nyingine duniani. Zaidi ya nusu ya watu wa Afrika wanaishi maisha duni. Katika miaka ya karibuni wastani wa miaka ya maisha wa watu wa Afrika umepungua na kufikia miaka 40 kutoka ule wa miaka 60 wa zamani, ni asilimia 3 tu ya watu wa nchi za Afrika wanaweza kupata elimu ya chuo kikuu.
Waliohudhuria kongamano hilo waliona kuwa, nchi za Afrika zinapaswa kuendeleza uchumi wao kwa kujitegemea na kuungana, na wala siyo kwa kutegemea misaada kutoka nje. Mwanafunzi wa shahada ya pili wa Chuo Kikuu cha Zimbabwe Bwana Fortune Gwaze alisema:
"Nchi za Afrika zinapaswa kutimiza utandawazi wa uchumi. Nchi nyingi za Afrika ni nchi ndogo, kama zitaweza kuungana na kuanzisha utandawazi wa uchumi kwa kutumia rasilimali zao kwa pamoja, basi zitaweza kupata manufaa makubwa zaidi katika mazungumzo ya mashirika ya kimataifa likiwemo shirika la biashara duniani kuliko yale yaliyopatikana katika mazungumzo kati ya nchi moja moja."
Bw. Gwaze alisema si kama tu serikali na viongozi wa nchi za Afrika wanawajibika kuhimiza utandawazi wa uchumi, watu wa fani mbalimbali wakiwemo wanawake na vijana wote wanatakiwa kutoa mchango katika harakati hiyo.
Kiongozi wa kundi la mabalozi wa nchi za Afrika nchini Zimbabwe, ambaye pia ni balozi wa Libya nchini Zimbabwe Bwana Mahmoud Yousef Azzabi alisema, hiyo ndiyo sababu ya kundi hilo la mabalozi na Chuo Kikuu cha Zimbabwe kufanya kongamano hilo. Ametumai kuwa wanafunzi walioshiriki katika kongamano hilo watafahamu changamoto zinazolikabili bara la Afrika, kuelewa msimamo wa Afrika kuhusu maswala mbalimbali, na kufahamu vizuri lengo la maendeleo ya nchi za Afrika.
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-26
|