Baada ya tetemeko la ardhi kutokea katika Mkoa wa Java ya Kati wa Indonesia na kusababisha vifo na majeruhi ya watu elfu kadhaa, jumuiya ya kimataifa imeanzisha kwa haraka harakati za uokoaji na utoaji misaada, nchi mbalimbali ikiwemo China na jumuiya kadhaa za kimataifa zimewapa pole wananchi wa Indonesia na kutoa misaada ya fedha na vifaa au kuwatuma waokoaji kwenda kwenye nchi hiyo kuisaidia kuokoa maafa.
Wizara ya mambo ya jamii ya Indonesia tarehe 28 usiku ilidokeza kuwa, tetemeko hilo la ardhi lililotokea tarehe 27 katika sehemu zilizoko pembezoni mwa Yohyakarta mkoani Java limesababisha vifo vya watu 5,100. Ofisa wa shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa nchini Indonesia alisema, takwimu zisizokamilika zinaonesha kuwa, watu elfu kadhaa wamejeruhiwa, na watu zaidi ya laki moja wamepoteza makazi yao. Hayo ni maafa makubwa zaidi ya kimaumbile nchini Indonesia tokea tsunami itokee kwenye bahari ya Hindi mwishoni mwa mwaka 2004 nchini Indonesia.
Serikali ya Indonesia imejulisha kuwa, hivi sasa sehemu zilizokumbwa na tetemeko la ardhi zinakabiliwa na taabu kama zifuatazo: kwanza, tetemeko la ardhi limeharibu njia ya uwanja wa ndege na barabara kubwa mjini Yohyakrta, limewafanya waokoaji na vifaa vya misaada wasiweze kuingia kwenye sehemu zilizokumbwa na maafa, hivyo sehemu hizo zinahitaji msaada wa dharura wa helikopta; pili, tetemeko la ardhi limebomoa nyumba nyingi kabisa za sehemu hizo, hivyo sehemu hizo hazina mashine makubwa za kuchimba udongo na vyombo vya kisasa vya kuwaokoa watu. Hakuna vifaa hivyo watu waliofukiwa chini ya kifusi huenda hawataweza kunusurika ndani ya siku moja au mbili; tatu, watu waliojeruhiwa ni wengi, sasa hospitali za huko zimejaa watu, na hospitali hizo hazina dawa za kutosha, hivyo huenda watu wengi waliojeruhiwa watakufa kwa sababu ya kutoweza kupata matibabu kwa wakati; nne, hivi sasa sehemu zilizokumbwa na maafa zimekuwa na ukosefu mkubwa wa chakula na maji ya kunywa, watu wengi walitafuta chakula kutoka kwenye kifusi, maofisa wa chama cha msalaba mwekundu cha Indonesia wanahofia kuwa hali hii itasababisha magonjwa ya maambukizi ambayo yataleta balaa kubwa zaidi; tano, umeme na huduma za mawasiliano ya habari zote zimekatwa katika sehemu zilizokumbwa na maafa, ambapo watu hawawezi kupata habari kuhusu jamaa zao na wameongeza wasiwasi moyoni, hali hii imeleta matatizo makubwa kwenye kazi ya uokoaji wa maafa na uratibu wa kazi ya uokoaji.
China na nchi mbalimbali za sehemu iliko Indonesia ya kusini mashariki ya Asia zimetoa misaada kwa haraka. Tarehe 27 serikali ya China ilipopata habari kuhusu maafa yaliyotokea nchini Indonesia ilitoa mara moja msaada wa fedha taslimu za dola za kimarekani milioni 2 kwa sehemu zilizokumbwa na maafa, ili kuwasaidia kuondoa taabu za dharura, na kutokana na hali ya maafa, serikali ya China itazingatia kutuma waokoaji na vifaa kwa nchi hiyo. Waziri mkuu wa muda wa Thailand Bw Thaksin Shinawatra tarehe 28 alitoa taarifa ya kuwapata pole wananchi wa sehemu zilizokumbwa na maafa nchini Indonesia, na kuahidi kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Asia ya kusini mashariki kutoa misaada kwa sehemu hizo. Waziri mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong tarehe 27 alimtumia salamu rais wa Indonesia akiahidi kuwa Singapore itatoa misaada ya dharura ya vifaa vyenye thamani ya dola za kimarekani elfu 50 kwa sehemu zilizokumbwa na tetemeko la ardhi nchini Indonesia. Tarehe 28 Singapore imetuma vikundi viwili vya uokoaji kwa sehemu zilizokumbwa na maafa za Indonesia. Rais Gloria Arroyo wa Philipims ameiagiza kamati ya uratibu wa maafa ya nchi hiyo iunde kikundi cha madaktari na wauguzi kwenda haraka iwezekanavyo kuwasaidia watu wa sehemu zilizokumbwa na tetemeko la ardhi nchini Indonesia. Na Malaysia pia imetuma kikundi cha wataalamu, madaktari na wauguzi kwenda Indonesia na kutoa misaada ya chakula na vifaa vingi vya mahitaji ya dharura kwa sehemu zilizokumbwa na maafa.
Wakati huo huo nchi mbalimbali na jumuiya mbalimbali duniani pia zimeanza kutoa misaada ya dharura kwa sehemu zilizokumbwa maafa nchini Indonesia.
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-29
|