Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-30 10:14:49    
Shindano la chemsha bongo la "Mimi na Radio China Kimataifa" ( 3 )

cri

Siku mpya za mbele

Wasikilizaji wapendwa, karibuni katika Shindano la chemsha bongo kuhusu "Mimi na Radio China kimataifa". Katika makala mbili tulizosoma katika wiki mbili zilizopita, tuliwafahamisha historia ya maendeleo ya miaka 65 ya Radio China kimataifa. Leo tunapenda kuzungumzia maendeleo ya siku za baadaye ya Radio China kimataifa.

                                                                       Bw. Wang Gengnian

Kabla ya kuwasomea makala ya tatu ya shindano la chemsha bongo, tunatoa kwanza maswali ya makala hiyo. Swali la kwanza: Radio China kimataifa imeanzisha kituo cha kwanza cha FM katika nchi gani? Swali la pili: Je, Tovuti ya Radio China kimataifa kwenye mtandao wa internet inajulikana kwa jina gani?

Wasikilizaji wapendwa, baada ya kusikiliza makala mbili tulizosoma wiki zilizopita, mmeshaelewa kuwa Radio China kimataifa ni radio pekee ya serikali ya China inayotangaza kwa nchi za nje. Tokea kuanzishwa kwake, Radio China kimataifa siku zote inabeba jukumu la kuijulisha dunia hali ya China, kwa kupitia matangazo ya radio yetu, wasikilizaji wengi wanaifahamu China siku hadi siku, na kuielewa Radio China kimataifa. Katika siku zilizopita, wasikilizaji wetu wengi walisikiliza matangazo yetu kwenye masafa mafupi, lakini hali hiyo imebadilika katika miaka ya hivi karibuni.

Tarehe 27 Februari mwaka 2006 ni siku moja inayostahili kukumbukwa katika historia ya matangazo ya China kwa nchi za nje. Katika siku hiyo, kituo chq CRI 91.9 FM kilianza kurusha rasmi matangazo yake huko Nairobi Kenya.

CRI 91.9 FM Nairobi ni kituo cha kwanza cha Radio China kimataifa kutangaza kwenye wimbi la FM katika nchi ya nje, siku ya kutangaza rasmi kwa radio hiyo, mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gengnian aliongoza ujumbe kwenda Nairobi kushiriki kwenye sherehe uzinduzi. Kuanzishwa kwa kituo hicho cha FM kumetimiza ndoto kwa wafanyakazi wa Radio China kimataifa wa vizazi kadhaa. Katika miaka 65 iliyopita, Radio China kimataifa iliendelea siku hadi siku na ilitangaza kwa lugha 38 za kigeni, na lugha nyingine 4 za kichina, lakini usikivu wa matangazo yake ulizuiliwa kila mara kutokana na njia ya urushaji wa matangazo na hali ya ufundi. Kuanzishwa kwa matangazo ya Radio China kimataifa kwenye wimbi la FM huko Nairobi Kenya kumeyafanya matangazo ya Radio China kimataifa yawakaribie zaidi wasikilizaji wake, ambapo Radio China kimataifa inatekeleza hatua kubwa ya mkakati wa maendeleo, kwamba inajitahidi kuyafanya matangazo yake yarushwe hewani moja kwa moja kutoka kwenye nchi wanapoishi wasikilizaji wake. Mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gengnian amedokeza kuwa, katika miaka mitano ijayo, Radio China kimataifa itapitia njia mbalimbali kuhimiza utekelezaji wa mradi wa kurusha matangazo yake moja kwa moja kwenye nchi wanapoishi wasikilizaji wake. Alisema:

Katika miaka mitano ijayo, Radio China kimataifa inapanga kujenga vituo 100 vya matangazo kwenye wimbi la FM au kwenye masafa ya kati katika nchi za nje, ili kuboresha usikivu wa matangazo yake katika nchi zinazoendelea za sehemu za Asia, Afrika na Latin Amerika na nchi za Amerika ya kaskazini na Ulaya; wakati huo huo itainua zaidi sifa ya vipindi vyake na kuvifanya vilingane na hali halisi ya nchi mbalimbali na kuwafurahisha zaidi wasikilizaji wake. Kwa kupitia hatua hiyo, Radio China kimataifa itapanua usikivu wa matangazo yake kwa wasikilizaji wa nchi mbalimbali, na kukaribia zaidi wasikilizaji wake, ili watu wa nchi nyingi duniani waweze kuifahamu na kuielewa China kwa hali yake halisi kwenye sekta mbalimbali.

Wakati huo huo, Radio China kimataifa pia ikifuata mkondo wa maendeleo ya vyombo vya habari duniani, inafanya juhudi kuendeleza matangazo yake kwenye mtandao wa internet. Hivi sasa wasikilizaji wetu wa nchi mbalimbali wakitembea mtandao wa internet kwa anuani ya CRI Online, wataweza kusikiliza kila wakati vipindi vyetu, ambapo pia wanaweza kupata habari mbalimbali kuhusu China kwa kupitia vipindi mbalimbali vya habari, michezo na maisha vilivyowekwa kwenye tovuti za lugha mbalimbali za mtandao wa CRI Online.

Hivi sasa vipindi vinavyoweza kusikika ambavyo vinawekwa kila siku kwenye CRI Online vimefikia zaidi ya saa 210, na vipindi hivyo vya kila lugha vinakuwepo kwenye tovuti kwa wiki moja, wasikilizaji wa kila siku wa vipindi hivyo wamefikia milioni 8. Kuanzia mwezi Julai mwaka jana, kwenye mtandao wa CRI Online umeanzisha INTERNET RADIO inayotangaza kwa lugha za kichina, kijerumani na kijapan, vipindi vya radio hiyo vinahusu habari, muziki na mafunzo ya lugha, radio hiyo inawafurahisha sana wasikilizaji wa Radio China kimataifa kwenye mtandao wa internet.

                                                                         Bw. Ma Weigong

Naibu mhariri mkuu wa Radio China kimataifa ambaye pia ni mhariri mkuu wa mtandao wa CRI Online Bwana Ma Weigong alisema, lengo la siku zijazo la mtandao wa CRI Online ni kuendeleza matangazo yake kwenye mtandao wa internet ambapo vipindi vyake vinapatikana kwa sauti, picha na maandishi kwa wakati mmoja. Alisema:

Tunapoendelea kudumisha nguvu na umaalum wa matangazo yetu ya lugha mbalimbali kwenye mtandao wa internet, pia tutaongeza kazi zetu mbalimbali, kama vile kufungua kurasa za Blog ambapo watu wanaweza kuandika maandishi yao kuhusu mambo mbalimbali, maandishi hayo yanaweza kuwa ya kichina, kiingereza, kijapan na lugha nyingine. Baadaye Radio China kimataifa itatumia teknolojia mpya kuanzisha kazi yake ya kutoa matangazo ya radio kwenye simu za mkononi, na matangazo ya televisheni kwenye simu za mkononi. Aidha, itatoa mafunzo ya lugha ya kichina kwenye mtandao wa internet ili kuwahudumia wasikilizaji wetu wanaotaka kujifunza kichina kwa kupitia mtandao wetu wa internet.

Wasikilizaji wapendwa, kadiri mambo ya uchumi na jamii ya China na mawasiliano ya China na nchi za nje yanavyoongezeka siku hadi siku, ndivyo wageni kutoka nchi za nje wanaokuja China kusoma, kutalii na kuanzisha biashara wanavyoongezeka siku hadi siku. Radio China kimataifa ikiwa radio pekee ya serikali ya China inayotangaza kwa nchi za nje, inabeba jukumu la kuwawezesha wachina wayaelewe mambo ya dunia. Hivi sasa CRI NEWS RADIO, EASY FM na HIT FM zilizoanzishwa na Radio China kimataifa pamoja na vipindi vya mafunzo ya lugha za kigeni vinatangaza kwa nyakati tofauti mijini Beijing, Shanghai, Guangzhou na kwenye miji mingine, ambapo wasikilizaji wa China wanaweza kupata kwa wakati habari za duniani, na muziki wa nchi mbalimbali, vipindi hivyo vinapendwa sana na wasikilizaji wetu wa nchini China.

Wakati huo huo, Radio China kimataifa kila siku inatengeneza vipindi zaidi ya saa 5 vya televisheni vya habari duniani, vipindi hivyo vinawasilishwa kwa kupitia satlaiti kwenye channel na radio zaidi ya 300 za sehemu mbalimbali nchini China. Gazeti la "Habari duniani" linalochapishwa na Radio China kimataifa linatoa habari nyingi mbalimbali kuhusu mambo ya siasa, uchumi, utamaduni, michezo, elimu, sayansi na teknolojia na jamii, gazeti hilo linachapishwa kwa sehemu mbalimbali nchini China.

Katika siku zijazo Radio China kimataifa itafanya juhudi kubwa za kutafuta nafasi nyingi za maendeleo. Mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gengnian alipozungumzia malengo ya maendeleo ya siku za baadaye ya Radio China kimataifa alisema:

Malengo ya Radio China kimataifa ya siku za mbele ni kuendeleza radio yetu kuwa chombo cha habari cha kisasa chenye matangazo ya radio, matangazo kwenye mtandao wa internet na matangazo kwenye televisheni ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu wa nchini na nchi za nje juu ya habari za China. Radio China kimataifa ikiwa dirisha moja la mawasiliano kati ya China na duniani, si kama tu itawasaidia wasikilizaji wake wa nchi za nje waijue na kuielewa China, pia itawasaidia wasikilizaji wa nchini China wajue vizuri zaidi mambo ya nchi mbalimbali duniani.

Bwana Wang Gengnian alisema ifikapo mwaka 2010, Radio China kimataifa itajizatiti kwa teknolojia na zana za kisasa zaidi, na kuwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza vipindi na kurusha matangazo kwa saa nyingi zaidi katika sehemu mbalimbali duniani, ambapo vituo vya waandishi wa habari vya Radio China kimataifa katika sehemu mbalimbali duniani pia vitaongezeka. Na itajitahidi kupunguza pengo kati yake na vyombo vya habari vya nchi kubwa kadhaa duniani katika ujenzi wa zana na vifaa vya radio na mvuto wake wa matangazo. Kwenye msingi huo, Radio China kimataifa itaendelea na juhudi kwa miaka kadhaa ili kujiendeleza kuwa radio ya kimataifa ya kiwango cha kisasa ambayo inaweza kulingana na nguvu za jumla za China na inaweza kuonesha umuhimu wake duniani.

Wasikilizaji wapendwa, sasa tunarudia maswali ya makala hiyo ya tatu ya shindano la chemsha bongo kuhusu "Mimi na Radio China kimataifa". Swali la kwanza: Radio China kimataifa imeanzisha kituo cha kwanza cha FM katika nchi gani? Swali la pili: Je, Tovuti ya Radio China kimataifa kwenye mtandao wa internet inajulikana kwa jina gani?

Wiki ijayo wakati kama huu mtakaribishwa kusikiliza makala ya 4 kuhusu Hadithi za wasikilizaji wa Radio China kimataifa. Msikose kutusikiliza.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-30