Wawakilishi wa nchi 5 wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na mwakilishi wa Ujerumani watakuwa na mkutano tarehe 1 mwezi Juni kuhusu mpango mpya wa utatuzi wa suala la nyukilia la Iran uliotolewa na Umoja wa Ulaya. Hii ni juhudi mpya ya jumuiya ya kimataifa ya kutatua suala la nyukilia la Iran kwa njia ya kidiplomasia.
Habari zinasema wazo la Umoja wa Ulaya ni kutaka Iran ichague moja ya njia mbili unazotoa: endapo Iran itaacha shughuli za kusafisha uranium, itapata manufaa mengi zaidi kutokana na mpango wa Umoja wa Ulaya kuliko manufaa uliyoiahidi hapo awali; La sivyo, itakabiliwa hatari ya kuwekewa vikwazo. Kutokana na mpango huo, ikiwa Iran itaacha shughuli za kusafisha uranium nchi mbalimbali zitaihakikishia Iran usalama; licha ya hayo zitaipatia Iran kinu cha nyukilia cha maji mepesi na nishati ya nyukilia. Lakini ikiwa Iran itashikilia kutoacha shughuli za kusafisha uranium, baraza la usalama litaiwekea vikwazo kutokana na kifungu cha 41 cha ibara ya 7 ya Katiba ya Umoja wa Mataifa vikiwa ni pamoja na kusimamisha utoaji viza kwa maofisa wa Iran ili kuwazuia kushiriki kwenye mikutano ya kimataifa, kuzuia fedha zake ilizoweka katika akaunti zake za nje, kupiga marufuku usafirishaji silaha na mafuta ghafi ya petroli. Lakini mpango huo haukutaja kuchukua hatua za uwekaji vikwazo kutokana na kifungu cha 42 cha Katiba ya Umoja wa Mataifa. Kifungu hicho kinasema, kama kukiwa na haja, inaruhusiwa kuchukua hatua ya kijeshi, hivyo mpango wa Umoja wa Ulaya umeondoa uwezekano wa kuishambulia Iran kijeshi.
Hivi sasa mpango huo unajadiliwa na utaamuliwa na maofisa waandamizi wa wizara za mambo ya nje za nchi wanachama wa kudumu wa baraza la usalama na ya Ujerumani, hatimaye utatolewa rasmi na Umoja wa Ulaya kwa Iran. Baadhi ya vyombo vya habari vimeainisha kuwa, mpango huo wa Umoja wa Ulaya utaweza kufikiwa mwafaka baada ya kujadiliwa kwa muda fulani kutokana na kuweko migongano kuhusu lengo la mpango na hatua zinazochukuliwa, kwani misimamo ya Umoja wa Ulaya, Marekani pamoja na Russia na China kuhusu utatuzi wa suala la nyukilia la Iran ni tofauti. Ofisa mmoja wa Umoja wa Ulaya alisema, kusuluhisha misimamo ya pande mbalimbali kunahitaji muda, pengine wiki kadhaa.
Hivi karibuni baadhi ya migongano ya misimamo ya Umoja wa Ulaya na Marekani ilifuatiliwa na vyombo vya habari. Habari zinasema, Marekani bado haijakubali kuacha haki ya kutumia nguvu ya kijeshi, na haitaki kutoa dhamana ya usalama kwa Iran, tena haipendi wito uliotolewa na Umoja wa Ulaya wa kufanyika mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Marekani na Iran. Marekani pia inapinga hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuzilinda kampuni na viwanda vya nchi za Umoja wa Ulaya vyenye uhusiano wa biashara na Iran. Gazeti la "Washington Post" lilichapisha habari tarehe 29 zikisema, Marekani inakosa zaidi na zaidi uvumilivu wa kutatua mgogoro wa nyukilia wa Iran kwa njia ya kidiplomasia. Serikali ya Marekani imebuni mpango wa kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi. Pindi Iran itakaposema "hapana" kuhusu mpango mpya wa utatuzi wa Umoja wa Ulaya, Marekani itatekeleza mara moja mpango wake wa kuweka vikwazo, tena itautaka Umoja wa Ulaya ushirikiane nayo. Lakini Umoja wa Ulaya haujaonesha juhudi kuhusu mpango wake, kwa sababu utekelezaji wake licha ya kuiumiza Iran, pia utaufanya Umoja wa Ulaya uingie hasara kubwa.
Msimamo wa Iran kuhusu mpango mpya wa Umoja wa Ulaya ni suala nyeti linalofuatiliwa na vyombo vya habari. Hivi sasa mpango huo mpya bado unajadiliwa, rais Mahmoud Ahmadi Neijad wa Iran alifananisha kitendo hicho cha Umoja wa Ulaya ni kutaka "kubadilisha chocolate kwa dhahabu". Waziri wa mambo ya nje wa Iran Bw. Manouchehr Mottaki, ambaye hivi sasa anafanya ziara nchini Malaysia, tarehe 29 alisisitiza kuwa kazi za haraka kwa Iran hivi sasa ni kulinda haki yake ya kuwa na teknolojia ya nyukilia. Hata hivyo, Iran haijafunga kabisa mlango wa mazungumzo na inaendelea kuwa na mazungumzo na Russia kuhusu kufanya shughuli za kusafisha uranium nchini Russia.
Suala la nyukilia la Iran litaweza kutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia, ila jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuwa na uvumilivu na busara na kuzingatia ufuatiliaji wa haki wa Iran.
Idhaa ya Kiswahili 2006-05-30
|